Ijumaa 6 Novemba 2026 - 13:41
Hizbullah; Hakuna mtaalamu wala mshauri yeyote wa chama hiki aliyeko nchini Yemen

Hawza/ Idara ya Mahusiano na Vyombo vya Habari ya Hizbullah, kupitia taarifa rasmi, imekanusha kwa msisitizo madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya kile kinachoitwa “Baraza la Mpito la Yemen”, kuhusu madai ya kuwepo wataalamu wa Hizbullah nchini Yemen na kushiriki kwao katika kusimamia operesheni za kijeshi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Idara ya Mahusiano na Vyombo vya Habari ya Hizbullah imetoa taarifa ya kukanusha vikali madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa kile kinachoitwa “Baraza la Mpito la Yemen”, kuhusu kuwepo wataalamu wa chama hicho nchini Yemen, kushiriki kwao katika kusimamia operesheni za kijeshi, pamoja na kuendeleza uwezo wa kijeshi, silaha na mafunzo ya ndugu zao katika Harakati ya Ansarullah.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa; tuhuma hizo hazina msingi wowote tangu mwanzo, ni za uongo kabisa na hazina uhusiano wowote na uhalisia.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa; wananchi wapendwa wa Yemen wana uwezo, rasilimali na uzoefu wa kutosha unaowawezesha kuilinda nchi yao na mamlaka yake dhidi ya uchokozi wowote, vitisho au mzingiro. Hivyo, hawahitaji msaada wala uingiliaji wa mtu yeyote katika kulinda nchi yao.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa; wananchi wa Yemen wamethibitisha uwezo huo kupitia mapambano yao dhidi ya uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya nchi yao, pamoja na msimamo wao wa kuiunga mkono Ghaza.

Vilevile, taarifa hiyo imesisitiza kuwa; mazungumzo ya dhati na yenye kuwajibika baina ya Wayemeni ndiyo suluhisho la kweli la kutatua tofauti au matatizo yoyote. Mazungumzo hayo yanapaswa kufanyika kwa namna itakayohifadhi umoja, mamlaka ya kitaifa na utulivu wa Yemen, na wakati huohuo kuzima njama za maadui wa Umma wa Kiislamu zinazolenga kuchochea mapigano baina ya mataifa na kuzisambaratisha nchi za eneo hili.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha