Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Ali al-Fatlawi, msemaji wa Harakati ya Ansarullah al-Awfiya nchini Iraq, amesisitiza kuwa; Kamati ya Pande Nne iliyoundwa na Mfumo wa Uratibu kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Muqawama wa Kiislamu inakabiliwa na hali ngumu katika kutekeleza masharti yaliyowekwa na Muqawama huo. Ugumu huo unatokana na kushindwa kamati hiyo kuishurutisha Marekani kusitisha ukiukaji wake dhidi ya anga ya Iraq.
Al-Fatlawi alisema kuwa masharti muhimu zaidi yaliyowasilishwa na Muqawama wa Kiislamu yanahusu kuhakikisha kuwa Serikali ya Iraq inakuwa na mamlaka kamili juu ya ardhi yake, bahari yake na anga yake.
Aidha, alibainisha kuwa kushindwa Kamati ya Pande Nne kuweka wazi maelezo ya makubaliano yaliyofikiwa na Muqawama, yawe ni ya siri au ya wazi, kunaonesha kuwa upande wa Marekani haujajitolea kutekeleza wajibu wa kusitisha ukiukaji wake unaoendelea.
Al-Fatlawi aliongeza kuwa; Muqawama wa Kiislamu umewaomba mara kadhaa viongozi wa Mfumo wa Uratibu kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili na kuweka wazi vipengele vyake.
Ikumbukwe kuwa Abu Mujahid al-Assaf, afisa wa masuala ya usalama wa Brigedi za Hizbullah, usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita alisisitiza kupitia ujumbe wake kwamba; Muqawama wa Kiislamu unasubiri kupatiwa nakala ya makubaliano yaliyosainiwa baina ya Muqawama wa Kiislamu uliopata ushindi na Kamati ya Mfumo wa Uratibu. Katika ujumbe huo, aliuliza kwa kejeli: “Je, Mkurugenzi Mkuu ameihifadhi nakala hiyo mfukoni mwake, au mna mtazamo mwingine?”
Maoni yako