Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake alioutoa kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa, aliitaja siku hiyo kuwa ni ishara ya “kupambana ana kwa ana kwa kambi ya haki dhidi ya kambi ya batili”, na kusisitiza kuhusu “kuweka wazi zaidi msimamo wa taifa la Iran dhidi ya Marekani ya kihalifu”.
Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei, kwa kurejelea upya “miongo kadhaa ya uadui wa wazi wa Marekani dhidi ya wananchi wa Iran katika vipindi mbalimbali”, aligusia “kufanywa siku za kusimama kidete na mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya Shetani mkubwa kuwa ni siku za kudumu na za kila siku”. Aidha, alisisitiza kwamba; adui katika kila hatua amekuwa akikabiliwa na ukuta imara wa uhalisia wa medani na miamba imara ya azma ya wananchi jasiri wa Iran.
Vilevile, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi alieleza kuwa; njia pekee ya kufikia kiwango cha juu kabisa cha uwezo wa kujikinga dhidi ya mashambulizi ya adui ni kuendeleza mkakati wa “Iran yenye nguvu zaidi” katika njia ya maendeleo ya pande zote. Pia, kwa mara nyingine alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuungwa mkono pande zote kati ya “wananchi” na “viongozi wa serikali”.
Ujumbe wa Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Leo ni Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa; siku ambayo inajumuisha matukio kadhaa muhimu ya kihistoria yanayoakisi mapambano ya kambi ya haki dhidi ya kambi ya batili, pamoja na kambi ya wanyonge dhidi ya kambi ya madhalimu.
Huenda ikasemwa kuwa tarehe 13 Aban ya mwaka huu, taifa la Iran limeuelewa wajibu na msimamo wake dhidi ya Marekani ya kihalifu kwa uwazi zaidi kuliko miaka yote iliyopita. Hata hivyo, kurejelea mizizi, sababu na matukio muhimu yaliyochochea kuongezeka uadui wa Marekani, pamoja na msimamo thabiti wa wananchi wa Iran dhidi yake, ni mwongozo wa kuangaza njia ya mustakabali wa mapambano haya.
Mwanzo wa dhuluma ya Marekani dhidi ya taifa la Iran ulianza zaidi ya miongo saba iliyopita, pale ilipotekeleza mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 28 Mordad (19 Agosti 1953), kwa lengo la kuendeleza uporaji wa rasilimali na mitaji ya taifa, hususan mafuta.
Miongo iliyofuata hadi ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilikuwa ni kipindi ambacho watawala wa Marekani walifanya juhudi kubwa za kupora mali na utajiri wa taifa la Iran. Katika njia hiyo, kwa kuanzisha Shirika la Usalama wa Taifa (SAVAK) na kuifanya jamii iingie katika mazingira mazito ya kiusalama, waliipa serikali dhalimu ya wakati huo uhuru mpana zaidi wa kukandamiza kila harakati ya upinzani. Katika kipindi kilichotangulia ushindi mtukufu wa Mapinduzi ya Kiislamu, pia walitumia mbinu na hila za aina mbalimbali kwa ajili ya kuilinda serikali yao iliyowekwa madarakani kwa kutegemea nguvu za kigeni. Kuhusu mwenendo wao wa uadui katika kipindi kilichofuata ushindi wa Mapinduzi makubwa ya wananchi wa Iran, tunaweza kuwasilisha orodha ndefu ya hatua zao zilizokuwa dhidi ya wananchi. Hatua hizo ni pamoja na:
Kuyasaidia moja kwa moja makundi yaliyokuwa yakitaka kuigawa Iran, wale waliopanga mapinduzi ya kijeshi na wanafiki waliokuwa na upofu wa moyo, ambao mbali na kuwaua kikatili wasomi na viongozi wa kisayansi, kisiasa na kijamii, waliwaua pia kwa wingi wananchi wa kawaida na kuwafanya mashahidi.
Kutoa msaada wa moja kwa moja na wa pande zote kwa Chama cha Baath katika vita vya kwanza vya kulazimishwa dhidi ya Iran; kuwaua raia wasiokuwa na hatia waliokuwa ndani ya ndege ya abiria; kuiwekea Iran vikwazo vikubwa vya kiuchumi, vya muda mrefu na vizito; kupanga na kuunga mkono machafuko na njama mbalimbali, na hata kuyapatia silaha; kumuuwa Shahidi Jenerali Qassem Suleimani, shujaa wa kitaifa wa Iran na wa Umma wa Kiislamu; kupora mali na utajiri wa wananchi wa Iran katika nchi mbalimbali; na hatimaye, kufanya mashambulizi ya kijeshi ya moja kwa moja katika vita vya pili na vya tatu vya kulazimishwa dhidi ya Iran, na kuwaua kishahidi idadi kubwa ya wasomi, wanasayansi, makamanda na umati mkubwa wa wananchi wanyonge wa Iran, kuanzia watoto wachanga, watoto wadogo, vijana hadi wazee, na juu ya wote hao ni Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mwenyezi Mungu autakase moyo wake mtukufu.
Katika hatua zote hizi, viongozi wakuu wa Marekani ya kibeberu na vibaraka wake wamekuwa wakilenga kulazimisha utawala wao juu ya Iran na kuifanya ijisalimishe. Hata katika matoleo yao ya hivi karibuni ya sera hizo za mabavu, wameachana na taratibu zote na sura za kimataifa za uongo na udanganyifu, na sasa kwa jeuri na bila haya wanataka kuigawa nchi, kuwalazimisha wananchi wapige magoti, kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuangamiza ustaarabu halisi na wa kale wa Iran.
Hata hivyo, katika kila hatua wamekuwa wakikabiliwa na ukuta imara wa uhalisia wa medani na miamba imara ya azma ya wananchi jasiri wa Iran. Matokeo ya hesabu zao potofu na fikra zao za kibabe yamekuwa ni gharama kubwa walizozibebesha wananchi wa Marekani na serikali zinazoutegemea utawala wa Marekani.
Kwa sasa, simulizi ya uadui wa muda mrefu wa Marekani dhidi ya taifa la Kiislamu la Iran, pamoja na muqawaa wa kishujaa wa wananchi wote wa Iran dhidi ya adui huyo, imefikia hatua ambayo si tarehe 13 Aban pekee, bali siku na saa zote zimekuwa siku za kusimama kidete na kupambana dhidi ya Shetani mkubwa.
Kwa sasa, eneo la Ghuba ya Uajemi, hususan Mlango-Bahari wa Hormuz, limekuwa likithibitisha ubatili wa simulizi ya kutoshindwa Marekani. Vilevile, limeonesha udhaifu na unyonge wa serikali zinazotegemea nguvu nyingine badala ya wananchi wao wenyewe, pamoja na ukosefu wa uaminifu na kushindwa madola makubwa kulinda serikali zinazotegemea kuungwa mkono.
Utekelezaji wa mamlaka ya Iran katika kusimamia Mlango-Bahari wa Hormuz na kuangamiza kambi za kijeshi za Marekani katika nchi za eneo hili, ingawa ulikuwa ni mwitikio dhidi ya uvamizi na jinai za Marekani katika vita vya tatu vya kulazimishwa, lakini wakati huohuo pia unahesabika kuwa ni Jihadi ya kuanzisha mapambano dhidi ya ubeberu katika wigo wa kikanda, endapo uvamizi huo utajirudia, mapambano hayo yatachukua wigo mpana zaidi.
Ishara hii ya nguvu, sambamba na umoja wa pande zote za kambi ya haki na mashujaa wa kimkakati na wenye nguvu wanaoandaliwa na Kambi ya Muqawama kuanzia Palestina na Lebanon hadi Iraq na Yemen, ni mwanzo wenye matumaini na mwangaza wa kuinuliwa bendera ya kambi ya haki na kuweka mazingira ya kuanzishwa mfumo mpya wa dunia.
Hii ni kwa sababu kila wakati kambi ya haki inapomtegemea Mwenyezi Mungu, subira, msimamo thabiti na kujitolea, basi kambi ya batili, bila kujali nguvu na uwezo wake, au ni nani na ni kitu gani, haiwezi kuhimili mbele yake. Hatima yake ya hakika ni kurudi nyuma na kushindwa, kwani:
“Hakika batili ni yenye kutoweka.” (Suratul Israa: 81).
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, taifa la Iran limejifunza vizuri mafunzo makubwa kutoka katika mafundisho ya Uislamu halisi wa Muhammad (s.a.w.w.), maarifa ya Mapinduzi ya Kiislamu na mwenendo wa viongozi wake wenye hekima, Imam Khomeini Mkuu na Shahidi Khamenei, Mwenyezi Mungu azitukuze daraja zao.
Siku baada ya siku, kupitia kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu, imani ya taifa hili kuhusu haki na ukweli wa njia hii imezidi kuwa imara na yenye kina zaidi.
Leo, kutokana na fedheha waliyojisababishia wenyewe watawala wa kibeberu, nguvu na mamlaka ya Marekani yanazidi kudhoofika, wamekumbwa na anguko lisiloweza kurekebishika katika nyanja zote mbili za nguvu za kijeshi na nguvu laini za kimataifa. Aidha, mchakato wa kusambaratika kwake ni wa haraka zaidi.
Ikiwa bado kuna watu wenye matumaini hata madogo ya kubadilika mwenendo wa Marekani au mabadiliko ya vyama na makundi ya kisiasa ndani ya mfumo wa utawala wa kibeberu, au wanaodhani kuwa kwa kuipa Marekani makubaliano ya upendeleo wanaweza kuifanya iachane na uadui wake dhidi ya taifa la Iran, basi wamekosea sana.
Mawazo haya potofu ni kutokuwa na shukrani kwa ushindi mkubwa ambao taifa la Kiislamu la Iran limeupata kwa kivuli cha kumtegemea Mwenyezi Mungu, kusimama imara na kufanya juhudi kubwa za kujitolea.
Matamanio ya Shetani mkubwa ni taifa la Iran kujisalimisha kwake bila masharti yoyote. Hivyo, mwelekeo wowote mdogo wa kujisalimisha mbele ya adui mwenye kutaka kutawala wengine utasababisha kupotea hazina kubwa iliyopatikana kwa baraka ya damu za mashahidi na kujitolea kila mwananchi. Vilevile, utamfanya adui huyo wa kibeberu azidi kuwa na ujasiri wa kutaka zaidi na kufanya vita na vitendo vingine vya uchokozi hapo baadaye.
Njia pekee ya kufikia kiwango cha juu kabisa cha uwezo wa kujikinga dhidi ya mashambulizi ya adui ni kuendeleza mikakati ya “Iran yenye nguvu zaidi” katika njia ya maendeleo ya pande zote.
Umoja, mshikamano na mshikano wa kijamii ni kipengele kikuu cha mafanikio katika njia hii, ambacho kinapaswa kutawala kila kauli na tendo la mtu mmoja mmoja na la kijamii, kwa wananchi na viongozi wa serikali. Katika suala hili, kama ambavyo wananchi kuwaunga mkono viongozi wa serikali ni jambo la lazima, vivyo hivyo ni muhimu kwa viongozi wa serikali kuendeleza na kuimarisha zaidi juhudi zao za kuwatumikia wananchi kwa kujituma, kwa moyo wa jihadi na kwa dhati. Pia wanapaswa kuwa na ukaribu na wananchi, kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ya maisha na ustawi, pamoja na kuendeleza ukuaji wao wa kimwili na kiroho, huku wakilinda heshima na uhuru wao.
Kundi la mbele katika kujenga mustakabali mwangaza na wenye utukufu wa Iran yetu pendwa ni vijana wetu, wanafunzi wa vyuo vikuu na wanafunzi wa shule. Wanapaswa kuendelea kufanya juhudi za kuteka na kubomoa ngome yenye giza ya “kukata tamaa, kukosa matumaini na dhana ya kwamba mambo hayawezekani”, na kuiteka nyumba yenye mwangaza ya “matumaini na imani kwamba sisi tunaweza”.
Sharti la kutekeleza jukumu hili ni kuwa na maandalizi na umahiri wa hali ya juu, kujizatiti kwa silaha mbalimbali za elimu, uchamungu, ujuzi, maadili, azma na juhudi za kipekee, pamoja na kuwa na “ahadi ya pamoja” ya kufikia malengo makuu.
Tunatumai kwamba kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na dua ya Bwana wetu, Imam Mahdi (a.j.f.), taifa la Iran litapata ushindi, mafanikio na maendeleo ya pande zote haraka iwezekanavyo, na kwamba mazingira ya kudhoofika na kuporomoka kwa kasi zaidi utawala wa Shetani mkubwa yataandaliwa.
Hakika wao wanaona jambo hilo kuwa liko mbali, lakini sisi tunaliona kuwa liko karibu.
Sayyid Mujtaba Husaini Khamenei
13 Aban 1405 (4 Novemba 2026).
Maoni yako