Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ahmad Awang, Mwenyekiti wa Umoja wa Kimataifa wa Misikiti katika kutetea Msikiti wa Al-Aqsa, huku akizungumza katika Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa “Mwamko wa Umma wa Muhammad (s.a.w.w.)”, uliofanyika siku ya Jumatano, kwa juhudi za Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun, alirejelea dhana ya mwamko na nafasi yake katika mabadiliko ya kihistoria ya mataifa, kisha akasisitiza umuhimu wa kugeuza mshikamano wa mataifa ya Kiislamu kuwa harakati pana ya kistaarabu.
Alianza hotuba yake kwa kumhimidi na kumsifu Mwenyezi Mungu. Kisha, akirejelea kauli iliyotajwa katika hotuba ya mwisho ya “Imamu Shahidi”, isemayo kwamba tukio litakapotokea kwa nchi hii, Mwenyezi Mungu atauamsha Umma huu, na wananchi wa njia hii wataifikisha kwenye hatima yake, alisema: “Kuchunguza kwa kina dhana ya Bi‘thah, kwa mtazamo wa falsafa na lugha, kunadhihirisha uwepo wa mabadiliko makubwa katika kanuni za kihistoria na kijamii za jamii ya mwanadamu. Kuchaguliwa neno Bi‘thah badala ya istilahi kama vile kuamka au harakati, kunaashiria kuhama kutoka katika hali ya kusimama tuli na kutoshiriki kikamilifu, kuelekea kwenye uhai, uchangamfu na kushiriki katika kuumba historia. Kwa mtazamo huu, matukio makubwa yanaweza kugeuka kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya kihistoria, ambayo huihamisha jamii kutoka pembezoni mwa historia na kuiweka katikati ya mabadiliko na matukio ya kihistoria.”
Sheikh Ahmad Awang, akirejelea tajiriba ya wananchi wa Iran, aliongeza kusema: “Dhana hii imejidhihirisha katika tajiriba ya wananchi wa Iran; tajiriba ambayo inaonesha uwezo wa kistaarabu na uwezekano wa kujinasua kutoka katika hali ya kutoshiriki kikamilifu. Umuhimu wa tajiriba hii unatokana na ukweli kwamba athari zake za kiutambuzi na kiutamaduni hazikubaki ndani ya mipaka ya kijiografia, bali zimejitokeza pia miongoni mwa mataifa mengine.”
Katika muktadha huo, alirejelea tajiriba ya Hizbullah ya Lebanon na Ansarullah ya Yemen, akieleza kuwa mwenendo huu unaonesha uwezo wa mambo yanayofanana katika utamaduni na itikadi wa kuwezesha kuvuka mipaka ya kijiografia.
Katika kuendelea na maelezo yake, alitaja kuwa changamoto kubwa zaidi inayoukabili Umma wa Kiislamu ni namna ya kunufaika na mshikamano huu na kuugeuza kuwa mwamko mpana unaouhusu Umma wa Muhammad (s.a.w.w.). Alisema: “Kuvuka kutoka katika mshikamano unaojitokeza katika medani za utekelezaji na mapambano, kuelekea kwenye mwamko wa kistaarabu ulio imara na endelevu, kunahitaji hatua tatu za msingi:
Kwanza: Kuanzisha mifumo ya pamoja ya maarifa na kuunda dira moja kuhusu utambulisho, hatima ya pamoja, pamoja na uhuru wa kiutamaduni na kiuchumi.
Pili: Kupanga na kuratibu harakati za wananchi ndani ya mfumo wa mradi wa kistaarabu, ambao utauongoza Umma kutoka katika mwitikio wa muda mfupi kwenye migogoro na changamoto, kuelekea kwenye hatua za kimkakati na shughuli za kuijenga na kuendeleza jamii.
Tatu: Kuzitathmini upya na kuzifasiri tena tunu za shahada na kujitolea mhanga, kwa kuzichukulia kuwa ni miongoni mwa sababu zenye mchango katika kuendeleza na kuchochea mwendo wa kihistoria wa mataifa.”
Mwenyekiti wa Umoja wa Kimataifa wa Misikiti katika kutetea Msikiti wa Al-Aqsa alisisitiza kwamba; mataifa hayafikii maendeleo kwa kutegemea ustawi wa kimada pekee. Bali, tunu za juu za kibinadamu na kujitolea mhanga pia zinaweza kutoa nguvu ya kiroho na ya kihistoria inayohitajika ili kuzuia kudumaa na kuimarisha utashi wa pamoja.
Mwisho wa hotuba yake, alisema: “Kufikiwa dira hii si jambo la matamanio ya kihisia tu, bali kunategemea kiwango cha mwamko na juhudi za mataifa, pamoja na uwajibikaji wa wasomi na viongozi wa fikra na siasa. Tunapaswa kujitahidi ili uwezo na vipawa mbalimbali vilivyomo ndani ya Umma wa Kiislamu viunganishwe katika njia moja ya pamoja na hatimaye kuunda mto mkubwa wa mwamko mpana; harakati ambayo itafufua upya nafasi na utume wa Umma wa Kiislamu miongoni mwa mataifa ya dunia.”
Sheikh Ahmad Awang alihitimisha hotuba yake kwa kurejelea Aya ya 143 ya Suratul Baqarah:
﴿وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ وَيَكُونَ الرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا﴾
“Na hivyo ndivyo tulivyowafanya kuwa Umma wa wastani (ulio bora na wenye msimamo wa haki), ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe shahidi juu yenu.”
Maoni yako