Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Hassan Qanaatli, Mkuu wa Jumuiya za Ahlul-Bayt nchini Uturuki, katika kikao cha saba cha kimataifa cha “Mwamko Mpya wa Umma wa Muhammad (saww)”, kilichofanyika Jumatano, kwa juhudi za Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun, alisisitiza nafasi ya fikra, tafakuri na kutumia uwezo uliojificha ndani ya jamii za wanadamu katika kufanikisha mabadiliko na maendeleo.
Akizungumzia nafasi ya Mitume wenye azma thabiti katika historia ya mwanadamu, alisema: Kwa mtazamo wa kidini, miongoni mwa sababu kubwa zaidi za kuubadilisha ulimwengu na maisha ya wanadamu ni fikra na tafakuri ambayo Mitume wa Mwenyezi Mungu waliiasisi na kujitahidi kuitekeleza. Mtume wa Uislamu (saww) pia, kwa kuasisi fikra iliyojengwa juu ya uadilifu, kuzingatia sheria na heshima ya utu wa mwanadamu, alifungua njia mpya mbele ya wanadamu.
Qanaatli alifananisha elimu na mbao zinazohifadhiwa ghalani, na kufafanua: Kama ambavyo mbao haziwezi kudhihirisha thamani yake ya kiutendaji mpaka zibadilishwe na kuwa bidhaa yenye manufaa, vivyo hivyo elimu, ikiwa itakusanywa akilini mwa mwanadamu lakini isiwe chachu ya tafakuri na uzalishaji wa fikra, haiwezi kuleta matunda yake halisi kwa mtu binafsi na jamii. Kwa mujibu wa maelezo yake, tafakuri ni njia ya kutoa uwezo uliojificha ndani ya elimu na kuigeuza kuwa mafanikio yenye manufaa kwa wanadamu.
Mkuu wa Jumuiya za Ahlul-Bayt nchini Uturuki, akieleza kwamba kuna uwezo na nyenzo nyingi duniani ambazo kustawi kwake kunategemea fikra na ubunifu wa mwanadamu, aliongeza: Mafanikio mengi ya kisayansi na kiteknolojia ya leo, kuanzia akili mnemba na simu janja hadi ndege, meli na magari, yametokana na kutambua na kuamsha uwezo ambao tayari ulikuwepo duniani hapo awali. Jamii ambazo zimeweza kutumia uwezo huo ipasavyo zimeweza kuibua mafanikio mapya kutokana nao.
Kisha alizungumzia nafasi ya Mitume katika kurekebisha na kujenga upya maisha ya kijamii, akasema: Hata kabla ya Mitume kupewa utume, maisha, kifo, ndoa, biashara na mahusiano mengine ya kibinadamu yalikuwepo; lakini Mitume walijitahidi kurekebisha mahusiano hayo, kupambana na tabia zisizofaa na kufufua tunu kama vile uadilifu, sheria, ubora wa sheria dhidi ya nguvu, uhuru na fikra. Mtume wa Uislamu (saww) hakutosheka tu na kuondoa mila zisizofaa za zama za Ujahiliya, bali alifufua tunu za kibinadamu na kijamii, kisha akajenga mfumo mpya kwa msingi wa tunu hizo.
Qanaatli, akizungumzia mabadiliko yanayotokea nchini Iran na nafasi ya wananchi wa nchi hiyo katika harakati ya Muqawama, alisema: Kwa sasa wananchi wa Iran wako katika njia ya kutimiza harakati ya kidini na kijamii ya kimataifa, na wanashiriki katika kufufua moyo na ari hiyo. Aidha, akirejelea maneno ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu nafasi ya matukio katika kuuchochea Umma wa Kiislamu kuchukua hatua, aliyataja mabadiliko haya kuwa ni mazingira yanayoweza kuchochea mwamko na ushiriki hai wa mataifa.
Pia alisisitiza kwamba ari ya Muqawama na kusimama imara haikomei nchini Iran pekee, bali mifano yake inaweza kuonekana nchini Lebanon na ndani ya Hizbullah, Iraq, Yemen na Harakati ya Ansarullah, pamoja na miongoni mwa wananchi wa Palestina wanaosimama imara. Kwa mujibu wa maelezo yake, mkondo huu unaweza, ndani ya wigo mpana zaidi, kuwajumuisha Waislamu wa maeneo yote duniani.
Mwisho, Qanaatli, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na utambuzi wa kina na uwezo wa kupambanua mambo, alibainisha kwamba Umma wa Kiislamu unapaswa kuwa na uwezo wa kutambua nyenzo zilizopo, kuzitumia ipasavyo na, kwa kutegemea fikra na tafakuri, kuweka mazingira ya kutokea mabadiliko na mafanikio mapya. Alihitimisha hotuba yake kwa kuwatolea salamu na kuwaombea dua waliohudhuria.
Maoni yako