Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, maandishi ya ujumbe wa Ayatullah Arafi, Mkurugenzi wa Hawza, kwa Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, kwa ajili ya kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuawa kishahidi Sayyid wa Mashahidi wa Umma, Sayyid Hassan Nasrullah, na Shahidi Sayyid Hashim Safi al-Din (Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote wawili), ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
﴿مِنَ الْمُؤْمِنِینَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَیْهِ فَمِنْهُمْ مَنْ قَضَی نَحْبَهُ وَمِنْهُمْ مَنْ یَنْتَظِرُ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِیلًا﴾
“Miongoni mwa Waumini wapo wanaume waliosadikisha yale waliyomuahidi Mwenyezi Mungu; miongoni mwao wapo waliotimiza nadhiri yao, na miongoni mwao wapo wanaosubiri, wala hawakubadilisha kabisa.”
(Al-Ahzab, 23)
Ndugu mpendwa na mwanazuoni mashuhuri, mwanamapambano, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon (Mwenyezi Mungu akuhifadhi na akusimamie),
Amani iwe juu yenu kwa sababu ya subira yenu; basi ni mema yaliyoje makazi ya mwisho.
Miaka miwili imepita tangu jioni ile ya tarehe 6 Mehr 1403 [27 Septemba 2024], ambapo adui Mzayuni, kwa msaada wa wazi wa Marekani, alirusha makumi ya tani za mabomu ya kutoboa ngome katika eneo la Dhahiya ya Beirut, akidhani kwamba kwa kuinyamazisha sauti ya Sayyid wa Muqawama, angezima pia taa ya Muqawama.
﴿یُریدونَ لِیُطفِئوا نورَ اللَّهِ بِأَفواهِهِم وَاللَّهُ مُتِمُّ نورِهِ وَلَو کَرِهَ الکافِرونَ﴾
“Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, lakini Mwenyezi Mungu ataitimiza nuru Yake, hata kama makafiri watachukia.”
Sasa, katika kumbukumbu ya mwaka wa pili wa kuuawa kishahidi Sayyid wa Mashahidi wa Umma, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Hassan Nasrullah, na rafiki yake mwaminifu na wa muda mrefu, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Shahidi Sayyid Hashim Safi al-Din (Mwenyezi Mungu awe radhi nao wote wawili), kwa niaba ya Hawza, walimu, wanazuoni na wanafunzi wa Hawza, pamoja na kutoa tena salamu za rambirambi kwako, kwa familia tukufu za mashahidi hao wawili, kwa Hizbullah yenye fahari na kwa wananchi watukufu wa Lebanon, ninawasilisha mambo yafuatayo:
Kwanza: Damu iliyogeuza mlingano
Maadui walidhani kwamba kwa kuwaondoa viongozi, mwili wa Muqawama, Muqawama ungesambaratika; kosa lilelile la kimahesabu walilolifanya hapo awali wakati wa kuwuawa kkshahidi Sayyid Abbas Musawi na Haj Imad Mughniyah, na ambalo wanalifanya leo pia katika kuwauwa kishahidi Imam Shahidi. Lakini miaka miwili imepita, na kile ambacho dunia ilikiona si kusambaratika, bali ni kujengwa upya uongozi, kudumu na kuwa na nguvu katika uwanja, pamoja na kuenea fikra za Muqawama ndani ya nyoyo na fikra.
Hii ndiyo Sunna ya Mwenyezi Mungu isiyobadilika, ambayo huifanya damu ya shahidi kuwa mbegu ya uhai wa Umma:
﴿ولا تَحْسَبَنَّ الَّذِینَ قُتِلُوا فِی سَبِیلِ اللَّهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْیَاءٌ عِنْدَ رَبِّهِمْ یُرْزَقُونَ﴾
“Wala usiwadhanie wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni wafu; bali wao wako hai kwa Mola wao, wanaruzukiwa.”
Na huu ndio ukweli ambao Sayyid Shahidi aliusema mara nyingi: “Sisi hatutashindwa; tukishinda, basi tumeshinda, na tukiuawa kkshahidi, bado tumeshinda.”
Leo, Sayyid Hassan Nasrullah si kumbukumbu tu, bali ni ukweli wa milele wa Ulimwengu wa Kiislamu na ni shule yenye kuhuisha maisha; shule ambayo imevuka mipaka ya Ushia na Lebanon na kupata nafasi katika dhamiri za watu huru duniani.
Pili: Sayyid wa Muqawama, mwanazuoni mwanamapambano na mtu mwenye sifa pana
Shahidi huyo mkubwa alilelewa katika Hawza za Najaf na Qom, na akaonesha kwamba uongozi wa kweli wa maulamaa wa Kishia unaweza kukusanya elimu na vitendo, hekima na ushujaa, pamoja na hali ya kiroho na siasa kwa mtu mmoja.
Alikuwa mfano wa fadhila za kimaadili na alama ya heshima ya Kiarabu na Kiislamu; alikuwa na akili ya kimkakati, uelewa wa kina wa kisiasa, uwezo madhubuti wa kiutawala na ujasiri katika uwanja wa mapambano. Na maneno yake, kutokana na ukweli na uaminifu wake, yalikuwa hoja hata mbele ya maadui zake.
Somo lake kubwa kwetu sote ni kwamba mtu anaweza, akiwa hana rasilimali kubwa lakini akiwa na utashi thabiti, kujenga uwezo mkubwa kutokana na fursa ndogo. Siri ya yote haya ilikuwa ni kushikamana kwake na Wilaya na kujitolea kwa dhati katika mstari wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu autukuze utajo wake) na Imam Shahidi, Hazrat Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu amrehemu).
Hawza zinajivunia mtu huyu na zinamchukulia kuwa mfano ulio wazi wa “mwanazuoni katika uwanja wa mapambano” kwa kizazi cha sasa cha wanafunzi wa Hawza.
Uvumilivu na subira, ujasiri, moyo wa kimapinduzi na jihadi, hekima na busara, elimu na kufikiri kwa kina, kuijua dunia, uwezo wa uongozi na usimamizi katika migogoro, kujenga taasisi za kijamii na kujenga nguvu, akili ya kijeshi, ubunifu na uvumbuzi, kushikamana na Wilaya, kufikiri kwa mtazamo wa dunia na mtazamo wa kistaarabu, mvuto na uwezo wa kuweka mipaka, na roho isiyotulia, yenye juhudi na isiyochoka, ni miongoni mwa sifa zake bora na za kipekee za shahidi huyu wa safu ya Muqawama na mfano wa uthabiti.
Leo tunajivunia kuutambulisha mkondo wa Sayyid Hassan kwa watu wote huru duniani kama kile ambacho mwanadamu wa zama hizi amekikosa katika dunia ya kimaada iliyoathiriwa na ustaarabu wa Magharibi.
Tatu: Msafara wa mashahidi
Tunakumbuka kwa heshima kumbukumbu ya Shahidi Sayyid Hashim Safi al-Din, yule rafiki mwaminifu na mwenza wa daima wa Sayyid wa Muqawama, pamoja na kumbukumbu ya makamanda wote, wapiganaji na watu wasio na hatia waliouawa kishahidi katika njia hii. Msafara huu, kuanzia Shahidi Sheikh Raghib Harb na Shahidi Sayyid Abbas Musawi, hadi Shahidi Haj Imad Mughniyah, Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na Haj Qassem, pamoja na mashahidi wote wa safu ya Muqawama, ni mnyororo unaoendelea wa jihadi, ikhlasi, ukweli na uaminifu, ambao hali yao inaelezwa na maneno haya ya Mwenyezi Mungu:
﴿وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِیلًا﴾
“Wala hawakubadilisha kabisa.”
Nne: Sayyid, wewe ni mbeba bendera wa mwendelezo
Katika siku ngumu zaidi za historia ya Muqawama, wakati adui alipodhani kwamba Hizbullah imebaki bila nahodha, wewe, pamoja na kundi jingine la makamanda wenye nguvu na hekima, kwa kutegemea uzoefu wako wa muda mrefu katika jihadi na uongozi, na zaidi ya miongo mitatu ya kuwa pamoja na Makatibu Wakuu waliouawa kkshahidi, ulichukua jukumu zito mabegani mwako na ukaendelea kuiinua bendera.
Hekima yako katika kulinda mshikamano wa ndani wa Hizbullah na kuujenga upya na kuutia nguvu; katika kulinda umoja wa kitaifa wa Lebanon; katika kuzifelisha njama za kuchochea fitina ambazo adui alikuwa akizitegemea; katika kuifanya upya ahadi thabiti ya kushikamana na Uongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu; na katika kuipanua safu ya Muqawama kuwa safu ya kikanda na kimataifa, inastahili kuthaminiwa na kuheshimiwa.
Hawza zinakutambua kama mwanazuoni msomi, mwandishi mwenye fikra na kiongozi mwenye hekima, na kama tulivyotangaza hapo awali, zimesimama pamoja nawe kwa uwezo wake wote.
Bila shaka yoyote, ushindi, ufunguzi na ushindi wa mwisho dhidi ya maadui, kuangamizwa Israel, kuangamizwa nguvu kubwa ya Marekani na ustaarabu potovu wa Magharibi, ni Sunna ya hakika ya Mwenyezi Mungu na hatima isiyokwepeka ya safu ya Muqawama, taifa kubwa la Lebanon, Hizbullah pendwa na yenye heshima, pamoja na wapiganaji wote.
Tano: Kwa ndugu wapiganaji wa Hizbullah
Tunawasalimu makamanda, viongozi, wawakilishi, wapiganaji na vikosi vya uokoaji, vyombo vya habari na taasisi za utamaduni vya Hizbullah.
Ninyi ni walinzi wa amana ya damu ya Sayyid wa Mashahidi, na kwa imani, nidhamu na uelewa wenu, mmeonesha kwamba Hizbullah haisimami kwa kutegemea watu binafsi, bali inasimama juu ya maarifa, imani, utashi na Wilaya.
Tunatoa heshima kwa mashujaa waliopata majeraha, hususan wale walioathiriwa na jinai ya milipuko ya vifaa vya pager na vita vya hivi karibuni, ambao kwa majeraha ya macho na mikono yao wameonyesha uelewa ulio wazi zaidi na utashi thabiti zaidi.
﴿فَإِنَّ حِزْبَ اللَّهِ هُمُ الْغَالِبُونَ﴾
“Hakika, kundi la Mwenyezi Mungu ndilo litakachoshinda.”
Sita: Kwa wananchi watukufu wa Lebanon na Mashia wake waaminifu
Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa wananchi wakubwa wa Lebanon, hususan watu wenye subira wa Kusini, Dhahiya na Bekaa. Mlivumilia kuwa wakimbizi kwa heshima na uelewa, mkavumilia uharibifu wa nyumba zenu kwa subira na imani, na kwa kurejea katika maeneo yenu, mkauonesha ulimwengu mshikamano usiokatika kati ya wananchi na Muqawama. Mama, baba, wake na watoto wa mashahidi wa Lebanon walisimama kwa namna ya Zaynab, na wakaeleza ukubwa wa Muqawama huu si katika silaha zake, bali katika utashi wa taifa lililo hai.
Mashia wa Lebanon ni warithi wa shule ya Jabal Amil; shule ambayo iliwalea Shahidi wa Kwanza na Shahidi wa Pili, na ambayo kutoka humo walitokea wanazuoni wenye asili ya Lebanon kama Muhaqqiq al-Karaki na Sheikh Baha'i, na hivyo kuweka uhusiano wa kielimu na kiroho kati ya Lebanon na Hawza za Iran, uhusiano ambao leo unaonekana katika ngome ya Muqawama. Vilevile, tunawashukuru watu wote huru wa Lebanon, kutoka katika madhehebu na makundi yote, ambao walisimama pamoja na Muqawama na kuulinda umoja wa kitaifa.
Jueni kwamba ninyi ni miongoni mwa Ansari bora zaidi wa Ahlul Bayt (amani iwe juu yao) katika kipindi chote cha historia, na kwa fadhila ya subira na Muqawama wenu, matarajio ya Mitume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu yanaendelea kutimia.
Dunia iko katika kipindi muhimu cha mabadiliko ya kihistoria na katika hatua yake ya mabadiliko makubwa, na mahusiano ya dunia yanaendelea kubadilika; vita vya kihistoria kati ya haki na batili vinakaribia kufikia mwisho wake, na ustaarabu mpya wa Kiislamu unaendelea kujengwa, nanyi mnashiriki na kuwa sehemu ya mabadiliko yote haya. Leo na kesho ya historia ni yenu, na ina deni la kujitolea kwenu na kwa mataifa yote yaliyojitolea kwa Iran, Iraq na Yemen.
Saba: Nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Wananchi wa Iran katika vita walivyolazimishwa navyo na Marekani na utawala wa Kizayuni, walikumbwa pia na majonzi ya kuuwawa kkshahidi Imam na kiongozi wao; lakini adui ambaye alikuwa akitarajia kusambaratika mfumo wa Kiislamu, kwa mshangao aliona kwamba kwa kuzingatia utaratibu wa kisheria, uongozi ulikabidhiwa kwa Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei (Mwenyezi Mungu amuhifadhi), na wananchi wakakusanyika kwa umoja na kusimama kuzunguka Wilaya.
Jamhuri ya Kiislamu ilitoka katika mtihani huu mgumu ikiwa imara na yenye mshikamano zaidi, na ikaona kuunga mkono Muqawama si mbinu ya muda mfupi, bali ni sera ya kimkakati na ya kimsingi. Hii ndiyo lugha ya wazi ya uhusiano ambao hakuna shinikizo litakaloweza kuudhoofisha.
Leo, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, licha ya kulazimishwa vita vya dunia nzima, mzingiro, vikwazo, dhuluma na vita vya pande zote vyenye mchanganyiko wa kijeshi, kisiasa, kiuchumi, vya vyombo vya habari na vya kiutambuzi, uko katika nguvu kamili ukiwa na wananchi wenye umoja, mshikamano na waliohamasishwa; ukiwa na viongozi wenye azma na utashi; ukiwa na makamanda na vikosi vya kijeshi vilivyo macho na vyenye nguvu; na ukiwa na washirika wengi katika pembe mbalimbali za dunia. Uko karibu na ushindi na kufanikiwa kwa mwisho, na pamoja na wapiganaji wote, utavuka vikwazo na matatizo yote kwa heshima, nguvu na hekima.
Nane: Umoja wa nyanja za Muqawama, ukweli wa kimkakati
Adui amekuwa akijaribu daima kuzitenganisha nyanja za Muqawama kutoka kwa kila mmoja ili kumshinda kila moja ikiwa peke yake. Lakini matukio ya miaka hii miwili yameonesha kwamba nyanja za Muqawama, kuanzia Tehran hadi Beirut, na kutoka Ghaza hadi Sana'a na Baghdad, na kuanzia Mlango-Bahari wa Hormuz hadi Bab al-Mandab, ni sura mbalimbali za safu moja yenye umoja.
Umoja huu si uhusiano wa uwakilishi; bali ni mshikamano unaotokana na imani ya pamoja, adui wa pamoja na lengo la pamoja, ambapo kila uwanja, kwa utashi na uamuzi wake wenyewe, unapiga hatua katika njia moja kwa ajili ya kuhakikisha maslahi ya kimkakati ya kitaifa, maslahi halisi na ya kweli ya kikanda, pamoja na maslahi mapana ya Umma wa Kiislamu. Damu ya makamanda mashahidi wa Iran iliyomwagika kando ya damu ya mashahidi wa Hizbullah ardhini ni ishara ya mshikamano huu.
﴿إِنَّ اللَّهَ یُحِبُّ الَّذِینَ یُقَاتِلُونَ فِی سَبِیلِهِ صَفًّا کَأَنَّهُمْ بُنْیَانٌ مَرْصُوصٌ﴾
“Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wale wanaopigana katika njia Yake wakiwa katika safu, kana kwamba wao ni jengo lililokaza na kuunganishwa.”
Tisa: Ahadi ya Hawza
Hawza, ambazo Sayyid Shahidi alikuwa mtoto wake mashuhuri, zimesimama imara katika ahadi yake ya kufuata njia yake, na ziko tayari kutekeleza wajibu wao katika kulinda na kueleza urithi wa fikra wa shahidi huyo katika nyanja za fiqhi, fikra za kisiasa, uongozi na maadili ya jihadi; katika kutafsiri na kuchapisha urithi huu kwa lugha mbalimbali; katika kupanua uhusiano wa kielimu na Hawza na wanazuoni wa Lebanon; na katika aina yoyote ya msaada wa kielimu, kiroho na wa kimalezi kwa safu ya Muqawama.
Mwishoni, kwa mara nyingine tena tunaiadhimisha kwa heshima kumbukumbu ya Sayyid wa Mashahidi wa Umma na mashahidi wote wa Muqawama, na tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akupe wewe na ndugu wote wapiganaji wa Hizbullah tawfiq, afya, uthabiti na ushindi; tukitumaini siku ambayo, kwa baraka ya damu ya mashahidi hawa, Quds Tukufu itakombolewa na ahadi ya kweli ya Mwenyezi Mungu itatimia.
Salamu, amani, fadhila bora kabisa, neema na rehema pana za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Hizbullah tukufu, juu ya Mashia na Waislamu wenye heshima wa Lebanon, na juu ya Umma wote wa Kiislamu.
﴿وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِینَ قُتِلُوا فِی سَبِیلِ اللَّهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْیَاءٌ عِنْدَ رَبِّهِمْ یُرْزَقُونَ﴾
“Wala usiwadhanie wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni wafu; bali wao wako hai kwa Mola wao, wanaruzukiwa.”
(Al Imran, 169)
Wassalaamu alaykum warahmatullahi wabarakaatuh.
Alireza Arafi
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran.
Maoni yako