Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa masomo katika shule na vyuo vikuu, aliwasalimu kwa heshima wanafunzi wa shule, wanafunzi wa vyuo vikuu, walimu na maprofesa waliouawa kishahidi katika vita vya hivi karibuni vilivyolazimishwa, na akautaja ufunguzi wa shule na vyuo vikuu kuwa ni ishara yenye kutia matumaini ya uchangamfu, matumaini na mwendo wa haraka wa taifa kuelekea mustakabali wenye mwanga. Aidha, aliwashauri wanafunzi wa shule na vyuo vikuu kujizatiti kwenye “elimu, uchamungu, ujuzi na uwezo”, na akiwahutubia akasisitiza: “Ichukulieni shule na chuo kikuu kuwa ni nyumba yenu ya pili, na kwa kuilinda heshima na mipaka yake, pamoja na kujitahidi kuinua zaidi kiwango cha uelewa na mtazamo wenu, na kuboresha tabia na mwenendo wenu, vifanyeni kuwa vituo vya maendeleo ya nchi yenu.”
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, matini ya ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:
بسم الله الرحمن الرحیم
یَرفَعِ اللهُ الَّذینَ آمَنوا مِنکُم وَ الَّذینَ اوتُوا العِلمَ دَرَجات
“Mwenyezi Mungu atawainua walio amini miongoni mwenu, na walio pewa ilimu daraja za juu..”
Mwanzo wa mwaka mpya wa masomo na kufunguliwa tena nyumba za elimu na adabu katika shule na vyuo vikuu, ni wenye kutangaza ujio wa uchangamfu, matumaini na mwendo wa haraka wa taifa kuelekea mustakabali wenye mwanga na utukufu. Ni mustakabali ambao utimizo wake umo mikononi mwa watoto wapendwa wa Iran wenye uwezo na wale waliolelewa katika shule ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu. Hichi ndio kizazi ambacho mara nyingi Imam Khomeini Mkuu na Khamenei mwenye adhama — Mwenyezi Mungu tukuze zaidi cheo cha mashahidi hao watukufu — walieleza matumaini yao waliyonayo juu yao.
Sasa ambapo lango la mwaka mpya wa masomo limefunguliwa mbele ya umati mkubwa wa wanafunzi wa shule na vyuo vikuu, na wasafiri wa njia ya elimu na hekima wanaanza kipindi kipya cha kujipatia elimu, maarifa na ujuzi kwa matumaini ya kupata tawfiki ya Mwenyezi Mungu, inafaa, sambamba na akina mama na baba wenye majonzi, kwa mara nyingine tuadhimishe kumbukumbu ya wanafunzi waliouawa kishahidi katika vita vya hivi karibuni vilivyolazimishwa. Mwaka huu, siku zenye kumbukumbu za mwanzo wa mwaka wa masomo zitatufanya tuhuishwe tena na huzuni ya kutengana na watoto wetu waliotangulia safarini. Katika shule na vyuo vikuu, pengo la baadhi ya wanafunzi wa vyuo, maprofesa na walimu litahisiwa, na huzuni hii itazielekeza akili zetu katika uelewa sahihi wa mapambano kati ya kheri na shari, na vita kati ya haki na batili.
Wajibu wa leo wa wanafunzi wa shule na vyuo vikuu ni kujitahidi kujizatiti kwa elimu na uchamungu, matumaini na maadili, ujuzi na uwezo, na kuondoa pazia la ujinga na giza, ili hatimaye, kwa kuvuka mipaka ya elimu na kufikia vilele vya maendeleo vinavyojenga mustakabali, waweze kutekeleza jukumu lao la kihistoria katika kuikuza Iran. Jambo hili hufanyika katika mahali panapohesabiwa kuwa nyumba yao ya pili, kwa hiyo, ninawaambia vijana hawa wapendwa kwamba ni lazima daima mlinde heshima na mipaka yake kwa namna bora kabisa, na kwa kuinua zaidi kiwango cha uelewa na mtazamo wenu, pamoja na kuboresha tabia na mwenendo wenu, pafanyeni kuwa kituo cha maendeleo ya nchi yenu.
Tumia fursa ya kuwepo kwako miaka kadhaa katika makao haya ya elimu, adabu, uchangamfu na matumaini kwa ajili ya kujijenga zaidi na zaidi; kujijenga katika jambo muhimu zaidi katika maisha ya mwanadamu, nalo ni uhusiano na Muumba Aliyetukuka; kujijenga katika uhusiano na wanadamu wenzako, wananchi wenzako na familia; na kujijenga katika uwanja wa kujipatia elimu na kupata aina mbalimbali za ujuzi.
Katika kipindi hiki, jizoesheni kufikiri kwa usahihi na kuwa wabunifu, na daima kuweni walinzi wa mizizi ya utambulisho wenu wa kitaifa, heshima na uhuru wenu wa kiutamaduni, lugha yenu ya mama, bendera tukufu ya mfumo wa Kiislamu na alama zake nyingine. Hivi karibuni itafika zamu yenu ya kupata nafasi inayowafaa katika jamii; na wakati huo, kwa kuitekeleza kwa namna bora zaidi, mtajenga heshima yenu wenyewe na ya nchi yenu.
Sasa katika zama ambazo ukatili wa mfumo wa utawala wa mabavu, hususan serikali ya kihalifu ya Marekani na mfumo bandia wa Kizayuni, umefikia kiwango kikubwa, nguvu inayotokana na elimu ikiambatana na uchamungu na maadili, ni kama ngao ya chuma na upanga mkali unaoikata mikono ya wavamizi hao na kuwazuia dhidi ya ubinadamu.
Sasa mnahudhuria madarasa ambayo vizazi vilivyowatangulia kwa muda mfupi, vilivyoketi kwenye madawati hayo ya kupendeza, hivi sasa viko katika nyanja mbalimbali za kulinda nchi na heshima kwa ajili ya Iran, vikiumba heshima na nguvu; na watu hao watakuwa mifano na taa za kuwaongoza. Kama ambavyo kabla yao, katika madarasa hayo hayo, walikuwepo watu ambao walihesabiwa kuwa mifano ya kujitolea, alama za ukubwa wa nchi na mashujaa wa adhama na utu.
Neno la mwisho linawahusu walimu na maprofesa. Sisi sote tunawahitajia walimu wetu katika kila hatua ya safari yetu ya kielimu. Tabaka hili pendwa na lenye kuheshimiwa, ambalo mara nyingi hukutana na hisia safi kabisa kutoka kwa wanafunzi wao, linastahili kuheshimiwa na kila mtu katika mikusanyiko na nyakati mbalimbali, ukarimu na kujitosheleza ambavyo kwa kawaida huonekana miongoni mwao, haviwafanyi viongozi wanaohusika kuridhika na hali yao ya sasa ya maisha; na Inshaallah, kwa mipango yenye hekima, watachukua hatua madhubuti za kuiboresha hali hiyo; hususan kwa kuwa suala hili linazidi kuwa utekelezaji wa wajibu wa kisheria, bali ni jambo linalotokana na moyo.
Amani, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya maprofesa, walimu, wanafunzi wa vyuo vikuu na wanafunzi wa shule waliouawa kkshahidi katika vita vya tatu vilivyolazimishwa, na juu yao akiwa katika nafasi ya kwanza Kiongozi wetu mwenye hekima na mlezi wetu mkuu aliyepatashahada — Mwenyezi Mungu akitukuze zaidi cheo chake kitukufu — ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika kasi kubwa ya maendeleo ya elimu nchini; na shukrani kwa walezi, walimu na maprofesa wote katika nyanja za elimu, maarifa na dini; na pongezi pamoja na ukaribisho kwa kila mmoja wa wanafunzi wa shule na vyuo vikuu wenye mustakabali mwema wa taifa la Iran; na tunatumaini kwamba, kwa dua yenye baraka ya Bwana wetu, Imam wetu — Mwenyezi Mungu aharakishe faraja yake tukufu — watafanikiwa zaidi na zaidi katika kufikia vilele vya elimu, adabu na maendeleo, Inshaallah.
Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei
Maoni yako