Alhamisi 20 Agosti 2026 - 11:49
Ripoti ya kikao cha kuchunguza shakhsia, fikra na shule ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah/ Kwa nini leo tunahitaji kumfuata Sayyid wa Muqawama kama mfano?

Hawzah/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Misbah Yazdi alisema: “Sifa kuu ya Shahidi Nasrullah ni tofauti kati ya ‘kuamini ukweli’ na ‘kufanya ukweli huo udhihirike katika mwenendo wa mtu.’”

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, kikao maalumu cha “Kuchunguza Shakhsia, Fikra na Shule ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah” kilifanyika katika Sekretarieti ya Vyama vya Kisayansi vya Hawza ya Qom, kwa kuhudhuriwa na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ali Misbah Yazdi na Mojtaba Misbah Yazdi, pamoja na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya Kongamano la Kimataifa la “Umanaa al-Rusul”.

Katika kikao hicho, kilichoandaliwa kwa lengo la kufafanua vipengele vya kielimu na kiroho vya shakhsia hii kubwa, vipengele mbalimbali vya fikra, jihadi na kiroho vya Katibu Mkuu shahidi wa Hizbullah ya Lebanon vilichunguzwa kwa kina.

Juhudi za kufafanua shule ya Muqawama

Mwanzoni mwa kikao hicho, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Muhammad-Taqi Rabbani, Mkuu wa Baraza la Kisayansi la Sekretarieti ya Kongamano la Kimataifa la Umanaa al-Rusul, akizungumzia mchakato wa kuanzishwa kwa Kongamano la Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, alisema: “Baada ya kuamua kufanyika kwa kongamano hili, vikao mbalimbali vilifanyika pamoja na viongozi wa Hizbullah ya Lebanon na wanaharakati katika uwanja wa Muqawama. Pia, wakati wa sherehe za mazishi ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, barua rasmi ya Sekretarieti ilitumwa kwa Sheikh Naim Qassem, jambo ambalo lilipokelewa vizuri naye na akaeleza utayari wake wa kushirikiana.”

Alisema kwamba; kwa sasa Sekretarieti imeainisha takribani miradi 10 hadi 12 ya kielimu inayohusu shakhsia na shule ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, na kuongeza: “Miongoni mwa mada hizo ni dhana ya kuleta ukaribu wa madhehebu katika fikra za Sayyid Hassan Nasrullah, mwenendo wa kiroho na kimaadili, namna ya kutumia vyombo vya habari, uwezo wa kushawishi, mtindo wa uongozi na fasihi ya Muqawama.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rabbani alibainisha: “Nyaraka kuhusu vipengele mbalimbali vya shakhsia ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah bado ni chache, na tunahitaji kuingia kwa umakini katika uwanja wa kielimu na utafiti ili tuweze kubainisha tabia, mwenendo na mfumo wake wa kiuongozi, na kuufafanua kwa ajili ya Hawza na vituo vya elimu.”

Umuhimu wa kuifanya shule ya Nasrullah kuwa mfano wa kiutendaji

Katika mwendelezo wa kikao, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Reza Eskandari, Katibu wa Kongamano la Kimataifa la “Umanaa al-Rusul”, akisisitiza umuhimu na uharaka wa kushughulikia vipengele vya kimaadili, kiroho, kimalezi na fikra za kisiasa za Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, alisema: “Jamii yetu ya leo, hususan kizazi cha vijana na wanafunzi vijana wa Hawza, inahitaji sana mifano yenye mafanikio, ya wazi na inayoonekana katika nyanja za kiuongozi na kiroho. Shakhsia pana ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah inaweza kuwa mfano na kielelezo bora katika malezi ya makada, siasa zenye msingi wa tauhidi, usimamizi wa migogoro na uongozi wa Muqawama.”

Katibu wa Kongamano la Kimataifa la “Umanaa al-Rusul”, akizungumzia mapokezi mazuri yaliyotolewa na jumuiya ya kielimu kwa tukio hili, aliongeza: “Hadi sasa, zaidi ya makala 300 za kielimu zimetumwa katika Sekretarieti ya Kongamano zikiwa na mada mbalimbali. Tunatafuta kushirikiana na vituo maalumu vya kielimu ili kuandaa makala na tafiti hizi katika mfumo wa kazi zenye mada maalumu na matumizi ya kiutendaji, ili matokeo ya Kongamano yawekwe kwa watafiti wa ulimwengu wa Kiislamu katika mfumo wa vifurushi vya maarifa vilivyounganishwa na vyenye mtiririko mmoja.”

Pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na Taasisi ya Kielimu na Kiutafiti ya Imam Khomeini (ra), akabainisha: “Uwezo wa kielimu wa taasisi hii kubwa unaweza kuwa na nafasi ya msingi na yenye kuamua katika uandaaji wa mwisho wa kazi hizi, hususan katika kuchambua uhusiano wa kimaarifa kati ya Shahidi Nasrullah na shule ya fikra ya Allamah Misbah Yazdi.”

Kufuata Wilaya ni zaidi ya utiifu

Katika sehemu kuu ya kikao hiki, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ali Misbah Yazdi, huku akitegemea ufafanuzi wa marehemu Ayatullah Misbah Yazdi (ra), alimtaja Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah kuwa mfano wa kipekee wa “imani inayoonekana kwa vitendo”, na kusisitiza: “Sifa kuu ya Shahidi Nasrullah ni tofauti kati ya ‘kuamini ukweli’ na ‘kufanya ukweli huo udhihirike katika mwenendo wa mtu.’”

Akirejea maneno ya marehemu Ayatullah Misbah Yazdi, alisema: “Marehemu Allamah alisisitiza mara nyingi kwamba; Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah hakuwa tu anafahamu misingi ya dini, bali misingi hiyo ilikuwa inaonekana na kuhusika katika maamuzi yake yote, mwenendo wake na hata katika adabu ndogo kabisa za maisha yake.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Misbah Yazdi, akiingia katika tafiti ya “Wilaya”, alieleza mtazamo maalumu wa Shahidi Nasrullah na kusema: “Marehemu Allamah aliamini kwamba kumtii Walii kwake kulikuwa kumevuka kiwango cha utiifu wa nje na wa kutekeleza wajibu. Katika utekelezaji, daima alikuwa akitafuta kuelewa nia na matakwa ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi. Hata katika mambo ambayo hayakutolewa maelekezo ya wazi, yeye, kwa busara yake ya kiwilaya, alikuwa akitambua njia hiyo na kuitekeleza kwa nguvu zake zote. Kwa sababu hiyo, marehemu Allamah alikuwa akisema daima: ‘Nina hakika kwamba Sayyid Hassan Nasrullah ni miongoni mwa wafuasi maalumu wa Hadhrat Wali al-Asr (aj).’”

Uhusiano wa kifikra na kiroho kati ya Ayatullah Misbah (ra) na Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah

Kisha, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mojtaba Misbah Yazdi, huku akirejea kumbukumbu za safari za marehemu Ayatullah Misbah Yazdi kwenda Lebanon, alifichua undani wa uhusiano wa kina wa kifikra na kiroho uliokuwepo kati ya shakhsia hizi mbili kubwa. Alisema kwamba uhusiano kati ya marehemu Allamah na Shahidi Sayyid ulikuwa zaidi ya urafiki wa kawaida; ulikuwa “uhusiano wa kimfumo wa kifikra”, ambao mhimili wake ulikuwa malezi ya wapiganaji wa Muqawama kwa misingi ya maadili, Wilayat al-Faqih na maarifa ya Mwenyezi Mungu.

Akizungumzia safari ya mwaka 1396 Hijria Shamsia ya marehemu Ayatullah Misbah Yazdi kwenda Lebanon, alisimulia kumbukumbu moja na kusema: “Katika safari hiyo, kinyume na taratibu kali za kiusalama, Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah mwenyewe alikwenda mahali alipokuwa akikaa marehemu Allamah kwa ajili ya kukutana naye. Katika mkutano huo, ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi uliwasilishwa kwake; ujumbe ambao ndani yake Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi alisisitiza juu ya dua, msaada wa kiroho na umuhimu wa kuimarisha maarifa ya wanachama wa Hizbullah. Hili linaonesha jinsi Wilaya inavyounda uhusiano usiokatika kati ya kiongozi, wanazuoni na wapiganaji.”

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Misbah Yazdi pia alizungumzia vipengele vya kielimu na tabia ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah ya kusoma, na kuongeza: “Kinyume na dhana ya jumla ambayo inaweza kumfanya mtu amuone kama kamanda wa kijeshi tu, yeye alikuwa mtu aliyependa sana kusoma na mwenye mtazamo wa kina. Alikuwa akisoma kwa mfululizo kazi za kifikra za Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, Imam Khomeini (ra), Shahidi Motahhari na marehemu Allamah Misbah Yazdi, na hata baadhi ya tafiti hizo alikuwa akizifundisha kwa watu wake wa karibu. Usomaji huu wa kudumu ulikuwa sababu kuu ya usafi wa moyo, mtazamo wa mbali na ibada ya kipekee iliyokuwa ikidhihirika katika mwenendo wake.”

Pendekezo la kuandaa kazi ya pamoja ya utafiti

Katika sehemu ya mwisho ya kikao, Dkt. Abdipour, Mkuu wa Vikao vya Ndani na Kimataifa vya Kongamano la Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, huku akiwashukuru watoto wa Ayatullah Misbah Yazdi (ra) kwa juhudi zao za kuchunguza vipengele vya shakhsia ya Katibu Mkuu shahidi wa Hizbullah, aliitaka Taasisi ya Imam Khomeini (ra) iandae kitabu kinachoeleza mitazamo ya Allamah Misbah kuhusu shakhsia na fikra za Shahidi Nasrullah.

Alipendekeza: “Kwa kuzingatia utajiri wa kifikra wa tafiti hizi, kazi hii yenye thamani inaweza kuandaliwa na kuchapishwa kama mradi wa pamoja wa utafiti kati ya ‘Taasisi ya Kielimu na Kiutafiti ya Imam Khomeini (ra)’ na ‘Sekretarieti ya Kongamano la Umanaa al-Rusul’, ili itumike kama waraka wa kielimu na rejea katika kufafanua uhusiano wa kifikra na kiroho kati ya viongozi wa Muqawama na nguzo za fikra za Kiislamu, na itumiwe na watafiti.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha