Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, “Jumuiya ya Familia za Mashahidi Watoto wa Lebanon” imelaani mauaji mapya yaliyofanywa na jeshi la uvamizi la Israel alfajiri dhidi ya familia moja katika mji wa Ansar, kusini mwa Lebanon, yaliyosababisha kuuawa kwa Sayyid Ali al-Hajj Hassan, Sayyida Zaynab Nasruddin na watoto wao Zahra, Hassan, Hussein na Abbas.
Jumuiya hiyo, katika taarifa yake, iliiomba Serikali ya Lebanon kukubali kikamilifu majukumu yake, kurekodi mauaji haya pamoja na uhalifu wote unaowalenga raia na watoto, na kuwasilisha mara moja kesi hizo kwa taasisi za kisheria na za mahakama za kikanda na kimataifa, kwa namna ambayo itahakikisha uhifadhi wa ushahidi na kufikishwa kwa wahusika mbele ya sheria kwa mujibu wa mifumo ya kisheria iliyopo.
Jumuiya hiyo pia iliitaka serikali kuchukua hatua za kivitendo na madhubuti za kuwalinda raia, na kujenga msimamo wa kitaifa wa kina ambao utailinda haki ya Lebanon na watu wake ya kujilinda dhidi ya uchokozi wa kikatili wa Israel, na kumzuia adui kutumia “makubaliano” yoyote au mfumo wowote uliopo kama sababu ya kuhalalisha kuendelea kuwashambulia raia wa Lebanon.
Jumuiya hiyo iliviomba vyombo vya habari kubeba jukumu lao la kimaadili na kitaaluma, na kuweka suala la watoto mashahidi katika mstari wa mbele wa habari zao, huku vikiandika na kuhifadhi hadithi, majina na nyuso zao. Aidha, ilivitaka vyombo vya habari kuchukua msimamo wa wazi dhidi ya adui mhalifu anayewaua watoto, badala ya kueneza madai yake, hata kwa njia ya dokezo au isiyo ya moja kwa moja.
Jumuiya hiyo, huku ikisisitiza kwamba haki ya Lebanon na watu wake ya kujilinda dhidi ya uchokozi ni haki ya kiasili, na kwamba jukumu la kwanza liko juu ya serikali, vinginevyo itakuwa imeachana na mamlaka yake ya nchi, ilisema: Hatutazoea kuuawa kwa watoto wetu na hatutaruhusu wageuzwe kuwa namba na takwimu. Damu ya watoto wetu iwe msukumo wa kuunganisha nyoyo na matakwa ya Walebanon wote, katika kumlinda mwanadamu, kuilinda Lebanon na kulinda mustakabali wa watoto wote wa Lebanon.
Jumuiya hiyo ilitoa pole za dhati kwa familia za mashahidi na kuzisisitizia kwamba; watoto wao si namba katika daftari la mauaji, bali kila mmoja wao alikuwa na uso, hadithi, ndoto na maisha ambayo yalipaswa kuendelea.
Vilevile, jumuiya hiyo iliwataka Walebanon kuonesha mshikamano na familia za mashahidi, kwa sababu damu ya mtoto wa Lebanon haifungamani na eneo moja tu.
Maoni yako