Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano wa Jamaat-e-Islami na Baraza la Wanazuoni wa Harakati ya Kiislamu ya India, ambapo wanazuoni wa dini, viongozi wa kijamii na wataalamu walisisitiza umuhimu wa mipango madhubuti, kuimarisha maadili, maendeleo ya elimu na uchumi, pamoja na shughuli za vitendo na za pamoja ili kukabiliana na changamoto za jamii ya Waislamu.
Maulvi Ilyas Khan Fallahi, mwanafikra wa Kihindi, katika hotuba ya ufunguzi alisema: Mwenyezi Mungu anautaka Umma wetu uonekane kama umma imara ili kheri yake iwafikie wanadamu wote. Umma wetu umepewa dini ya uongofu, na mfano wa dola ya Madina ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ndio mwongozo bora wa kutatua matatizo ya wanadamu.
Aliongeza kuwa; katika hali ya sasa, ikiwa Umma utachagua njia sahihi, unaweza kubadilisha hali ya kijamii na kitamaduni kwa manufaa yake. Pia alisema kuwa; katika mazingira yaliyojaa chuki na mvutano, jukumu la Waislamu si kuwa na mtazamo hasi, bali kueneza kheri na mafanikio kwa wanadamu wote, na kwamba maadili na matendo ya Mtume (s.a.w.w) ni mfano wa kipekee katika kukabiliana na ufisadi na matatizo ya kijamii.
Umuhimu wa hatua za vitendo na maadili
Katika mkutano huo ilisisitizwa kuwa; marekebisho ya maadili na kushikamana na mafundisho ya dini ni nguzo kuu ya kuuwezesha Umma wa Kiislamu. Washiriki walikumbusha kuwa bila maadili, madai yoyote ya Uislamu yatakuwa batili na yasiyo na maana. Pia walisisitiza umuhimu wa mipango ya dhati katika elimu, uchumi na shughuli za kijamii ili Umma uweze kufikia nafasi yake halisi katika hali ya sasa.
Moja ya mihimili muhimu ya mkutano huo ilikuwa kuiga mwenendo wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika kukabiliana na migogoro na matatizo ya kijamii. Wazungumzaji walisisitiza kuwa; mabadiliko chanya katika jamii yanawezekana kupitia kumuamini Mwenyezi Mungu, uhusiano wa karibu na Mola, na juhudi za vitendo ndani ya mpango mpana. Maisha ya Mtume yanaonesha kuwa ;hata katika kilele cha uharibifu wa maadili, marekebisho ya jamii yanawezekana ikiwa njia sahihi ya maadili itafuatwa.
Hali ngumu ya kihistoria na umuhimu wa matumaini na juhudi
Muhandisi Sayyid Saadatullah Husaini, kiongozi wa Jamaat-e-Islami India, akizungumzia hali ya sasa ya Umma alisema: Bila shaka hiki ni kipindi kigumu sana katika historia ya Umma. Hata hivyo, ni lazima kujenga roho ya matumaini katika jamii kwamba hali ngumu inaweza kuwa chanzo cha mabadiliko, maendeleo na kufufuka kwa Umma.
Aliongeza, akimnukuu mhadhiri wa chuo kikuu kwamba; maendeleo ya mataifa hayapatikani katika hali ya kawaida; bali hutokana na changamoto na matatizo. Pale uwepo wa mataifa unapokuwa hatarini, hulazimika kutafuta njia mpya za kuvuka migogoro.
Kiongozi huyo wa Jamaat-e-Islami India aliwaambia vijana: Katika hali ya sasa, si lazima tu kujilinda dhidi ya hatari, bali pia kurekebisha udhaifu, kuimarisha uwezo na kuelekeza nguvu katika njia mpya. Kuacha kukata tamaa na kutafuta suluhisho ni funguo ya kuondoa matatizo yetu.
Aliongeza kuwa; kuamsha ufahamu wa lengo na kuunganisha Umma juu ya lengo hilo kunapaswa kuwa kipaumbele kikuu.
Umuhimu wa elimu na maendeleo ya uchumi
Muhandisi Husaini pia alisisitiza umuhimu wa elimu, akisema kuwa; athari za kuzingatia elimu tayari zimeonekana. Sasa, mtazamo huo huo wa mpangilio unapaswa kufuatwa ili kufikia maendeleo ya kiuchumi.
Aliongeza kuwa; Jamaat-e-Islami India inafanya juhudi kubwa za kuboresha hali ya kiuchumi ya Umma kwa lengo la kuwawezesha Waislamu katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kitamaduni.
Kwa upande wake Shahid Latif, mhariri wa jarida la Inqilab Mumbai, alizungumzia baadhi ya desturi zisizo sahihi katika jamii ya Waislamu na kusema: Mara nyingi tunakuwepo katika maeneo mbalimbali lakini hatuna ufahamu wa kina wa hali halisi, na tunawalaumu maadui bila kuchukua hatua za kivitendo. Alisisitiza umuhimu wa kujua takwimu sahihi, akitaja suala la “talaka tatu”, na kusema kuwa; ukosefu wa taarifa sahihi huzuia kuthibitisha ukweli mbele ya mahakama na jamii.
Zahir Abbas Rizvi, mwanafikra wa Kishia, alisisitiza umuhimu wa maadili katika jamii ya Waislamu, alisema kuwa; jukumu la marekebisho ya maadili si la wanazuoni na maimamu wa misikiti pekee, bali wazazi pia wanapaswa kufuatilia malezi ya watoto wao, ikiwa ni pamoja na kujua wanapokuwa usiku.
Aliongeza kuwa; bila maadili, hata madai ya Uislamu yatakuwa matupu na yasiyo na maana.
Mtazamo wa kihistoria na umuhimu wa mazungumzo na elimu endelevu
Salim Alvar, mwanaharakati wa kijamii wa Kihindi, alisema kuwa; changamoto za sasa za jamii ya Waislamu si jambo jipya, na tangu miaka ya mwanzo ya uhuru wa India, Waislamu katika vijiji na mitaa walikuwa wakifanya doria za usiku kwa hofu ya mashambulizi.
Maulvi Mahmud Daryaabadi pia alisema kuwa; licha ya ugumu wa hali ya sasa, suluhisho lake ni kubadilisha fikra kupitia mazungumzo, elimu na uhamasishaji endelevu. Alisisitiza kuwa; kila tukio la dhulma dhidi ya Waislamu linapaswa kufikishwa mahakamani, hata kama matokeo hayatapatikana mara moja, kwani juhudi endelevu huzaa mafanikio.
Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la kuongeza uelewa, kurekebisha maadili na kuwahamasisha Waislamu kuchukua hatua za vitendo na za pamoja kwa ajili ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni, huku ukisisitiza kuwa; umoja, kujitambua na kufuata mafundisho ya dini, ndiyo njia ya kuvuka migogoro na changamoto za sasa za Umma wa Kiislamu.
Maoni yako