Kwa mujibu wa kitengi cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Modarresi, mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Iraq, huku akisisitiza nafasi tendaji ya hawza za kielimu katika kulinda uthabiti wa Umma wa Kiislamu dhidi ya upotovu, alieleza wazi kuwa: taasisi hii imeinua bendera ya harakati na ulinzi wa misingi ya Sheria na maadili ya Kiislamu dhidi ya mikondo ya fikra ngeni.
Katika mkutano wake na wawakilishi wa wanafunzi wa hawza ya kielimu ya mji wa Ahwaz Iran, huku akirejea mizizi ya kihistoria na ya kiroho ya hawza, aliielezea kuwa ni “sehemu hai ya uti wa mgongo wa Umma wa Kiislamu” na kusema: hawza ni mwendelezo wa kiasili wa njia ya wale waliokuwa thabiti katika elimu ya Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.) na mwenendo wa Ahlul-Bayt (a.s.).
Ayatullah Modarresi aliendelea kusisitiza kuwa: hawza ya kielimu ni dhihirisho la “jamii ya kielimu ya Kiislamu” inayohifadhi utambulisho na uhalisia wa Umma.
Katika mwendelezo wa hotuba yake kuhusu malengo na sifa za hawza ya kielimu, mwanazuoni huyu mashuhuri alitaja sifa tatu za msingi ambazo mwanafunzi wa dini na pia taasisi ya hawza zinapaswa kuzitilia maanani kwa upekee:
Kwanza: Kuitafakari Qur’ani Tukufu
Akiainisha kuwa Qur’ani ni msingi wa dini na mpango wa maisha, alisisitiza: ni lazima tuondoke katika usomaji wa juu juu na tufikie kwwnye “kuzitafakari aya za Qur’ani”. Ili Qur’ani iwe mwongozo katika kila undani wa maisha, ni lazima aya zake ziunganishwe na hali halisi ya maisha.
Pili: Kumfuata Mtume Mtukufu na Ahlul-Bayt (a.s.)
Ayatullah Modarresi huku akisisitiza kuwa, uhusiano na Mtume Mtukufu na Ahlul-Bayt watoharifu (a.s.) umejengwa juu ya mapenzi, ufuasi, kuwaiga na kutenda kwa mujibu wa mwenendo wao, alibainisha kuwa: elimu za Ahlul-Bayt (a.s.) ni ngome imara inayolinda akili ya Mwislamu dhidi ya upotovu na kupotea.
Tatu: Uwajibikaji
Alitaja sifa muhimu zaidi ya hawza ya kielimu kuwa ni kumwandaa mtu kukabiliana na “changamoto za kifikra na kisaikolojia”, kumlea kwa misingi ya maadili ya Kiislamu, pamoja na kujitolea kwa taasisi hii katika kutekeleza kuamrisha mema na kukataza maovu. Alisisitiza kwamba: mwanazuoni wa dini ndiye mwenye jukumu la kwanza katika kuwalinda watu dhidi ya mikondo ya kifikra iliyoingizwa kutoka nje.
Katika hitimisho lake, Ayatullah Modarresi aliwafahamisha hadhira kuyafikisha maarifa haya kwenye jamii, akisema: wanafunzi na wanazuoni wa hawza wanapaswa kuwa ndani ya nyoyo za watu, washiriki maumivu na mahangaiko yao. Pia alisisitiza kuwa: nguvu ya hawza hutokana na kushikamana na Vizito viwili na ikhlasi katika kutekeleza risala ya Mwenyezi Mungu kwa Umma.
Maoni yako