Ijumaa 23 Januari 2026 - 06:00
Serikali ya Pakistan ichukue msimamo wa wazi dhidi ya vitisho vya Marekani dhidi ya Iran

Hawza/ Seneta Raja Nasir Abbas Jafari, katika hotuba yake, alikosoa msimamo wa tahadhari wa serikali ya Pakistan mbele ya vitisho vya Donald Trump, Rais wa Marekani, dhidi ya Iran, na akataka kuwepo kwa radi amali ya wazi na ya dhahiri.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Seneta Raja Nasir Abbas Jafri, Spika wa Bunge la Umoja wa Waislamu wa Pakistan, katika hotuba yake alikosoa vikali msimamo wa tahadhari wa serikali ya Pakistan dhidi ya vitisho vya Donald Trump, Rais wa Marekani, dhidi ya Iran, na akasisitiza umuhimu wa kuchukuliwa msimamo wa wazi.

Katika hotuba yake bungeni, alisema: “Ni nani aliyempa Donald Trump mamlaka ya kuamua kuhusu hatima ya mataifa mengine?”

Spika wa Bunge la Umoja wa Waislamu wa Pakistan aliongeza kusema; kuwa hakuna sheria yoyote, kanuni ya kimaadili wala taratibu za kimataifa zinazoruhusu mwenendo wa kinyonyaji na wa uvamizi wa aina hiyo.

Katika kuendelea na hotuba yake, alisisitiza kuwa, ukimya katika mazingira nyeti ya sasa duniani ni kinyume na maslahi ya kitaifa ya Pakistan. Aliitaka serikali kuchukua jukumu la uongozi katika ngazi ya kidiplomasia kwa kuitisha mkutano wa dharura wa nchi jirani za eneo hilo, ili kuendeleza misingi ya amani, uhuru wa mataifa na heshima ya pande zote.

Seneta Raja Nasir Abbas, huku akipinga sera ya kuwasilisha “vitisho, mabavu na uvamizi” kama suluhisho la matatizo ya kimataifa katika mgogoro wa sasa, alisema: Dunia ya leo inahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote uongozi wa busara, si watu waliozama katika ulevi wa madaraka.

Aidha, alilaani vikali “propaganda za uongo” zinazofanywa na vyombo vya habari vya Magharibi dhidi ya Iran, na akavitaka vyombo vya habari vya Pakistan kuweka kipaumbele kwa taarifa zinazotegemea ukweli, badala ya kutegemea upofu vyanzo vya Magharibi.

Mwisho, aliitaka jumuiya ya kimataifa kukuza “lugha ya akili, sheria na mazungumzo badala ya lugha ya mabavu”, kwa kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha amani na ustawi wa kudumu katika ukanda na duniani kote.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha