Ijumaa 23 Januari 2026 - 00:30
Taasisi ya kisheria ya “Hind Rajab” inafuatilia kuwawajibisha wahalifu wa mauaji ya kimbari huko Ghaza

Hawza/ Taasisi ya "Hind Rajab" kwa zaidi ya miaka miwili imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa kisheria na kikatiba duniani kote kwa lengo la kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wahalifu wa mauaji ya kimbari huko Ghaza.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengi cha  tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, licha ya kupita zaidi ya miaka miwili tangia kutokea kwa uhalifu wa kinyama uliofanywa na utawala wa Kizayuni kwa msaada wa Marekani huko Ghaza, taasisi nyingi za kisheria duniani zimekuwa zikifuatilia masuala ya kisheria na kufungua mashauri dhidi ya wahalifu waliohusika na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza.

Licha ya jitihada za taasisi za kisheria duniani kote za kuwakamata na kuwahukumu wahusika wa mauaji ya kimbari na uharibifu wa misikiti pamoja na miundombinu katika Ukanda wa Ghaza, utawala wa Kizayuni kwa kutumia ushawishi wake na shinikizo la kisiasa unajaribu kuwaokoa wanajeshi wake na wahusika wa uhalifu huo.

Taasisi ya "Hind Rajab" ni miongoni mwa taasisi za kisheria zilizoanzishwa baada ya kuuawa kishahidi mtoto wa Kipalestina aitwaye Hind Rajab pamoja na familia yake, mjini Brussels. Hind Rajab lilikuwa jina la msichana wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 5, ambaye pamoja na watu 6 wa familia yake aliuawa shahidi na jeshi la Israel mnamo mwaka 2024, kufuatia shambulio la mabomu dhidi ya gari walilokuwa wamejisitiri ndani yake kusini-magharibi mwa Ghaza.

Taasisi ya Hind Rajab ilianzishwa Februari 2024, na makao makuu yake yako Brussels. Inafanya kazi katika uwanja wa kufuatilia kisheria viongozi na wanajeshi wa Israel kwa kufungua mashtaka ya kisheria dhidi yao duniani kote.

Katika kipindi cha miaka miwili, taasisi hii imeandaa na kuwasilisha malalamiko kadhaa dhidi ya wahusika wa uhalifu na mauaji ya kimbari huko Ghaza, na imefanikiwa kuwawekea vikwazo na matatizo mbalimbali wahalifu hao.

Taasisi ya Hind Rajab ni shirika la haki za binadamu ambalo hivi karibuni limewasilisha malalamiko ya jinai dhidi ya mchekeshaji mmoja wa Israel anayeishi New York, ambaye hapo awali, wakati wa huduma yake katika jeshi la uvamizi, alilipua msikiti mmoja katika Ukanda wa Ghaza. Malalamiko hayo yaliwasilishwa kwa mamlaka ya jiji hilo.

Guy Hochman, mwenye umri wa miaka 34, aliyekuwa kamanda wa kikosi cha 932 cha Brigedi ya Nahal ya jeshi la mauaji ya watoto la utawala wa Kizayuni, alihudumia katika kikosi ambacho kimeua maelfu ya Wapalestina katika Intifada ya kwanza na ya pili, na kushiriki katika vita vilivyoua familia nyingi za Ghaza. Guy huonekana mara kwa mara katika programu za jeshi na kulisapoti kupitia mitandao ya kijamii, lakini wakati wa Kombe la Dunia alijionesha kama Mwisraeli mpenda amani.

Taasisi hiyo ilitangaza katika taarifa yake kwenye tovuti yake ya kielektroniki kwamba jitihada za kisheria dhidi ya Guy Hochman—mchekeshaji na askari wa akiba—kwa kosa la kuhusika katika uhalifu wa kivita katika vita vya Ghaza, zimekumbana na vikwazo.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa katika muktadha huo, taasisi hiyo imeomba kufanyika ufuatiliaji wa haraka wa kisheria nchini Marekani, na imewasilisha jalada lenye ushahidi mpana na uliothibitishwa wa uhalifu wa kivita pamoja na uchochezi wa moja kwa moja wa mauaji ya kimbari huko Ghaza.

Baada ya kuwasilishwa kwa malalamiko ya taasisi hiyo na jalada la uchunguzi kwa serikali, Guy alikamatwa siku ya Jumatatu na kufanyiwa mahojiano marefu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pearson mjini Toronto, Kanada.

Taasisi hiyo ilieleza kuwa hadi kabla ya kuingilia kati ubalozi wa Israel, Hochman alikuwa bado anazuiliwa; lakini baada ya shinikizo la Israel kwa lengo la kuweka vikwazo mbele ya haki na uchunguzi, aliachiliwa huru.

Hochman, katika mazungumzo na Kituo cha Televisheni cha Kiebrania Channel 12, alithibitisha kukamatwa kwake kwa saa sita nchini Kanada, kufanyiwa uchunguzi, pamoja na upatanishi wa ubalozi wa Israel na kuingilia kati Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel katika kuachiwa kwake.

Taasisi nyingi, zikiwemo Hind Rajab, zinafanya juhudi kubwa za kufuatilia na kuwahoji wanajeshi wa Israel kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari dhidi ya raia wasio na hatia wa Ghaza.

Hapo awali pia, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa hati za kukamatwa dhidi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, na Yoav Gallant, Waziri wa zamani wa Ulinzi wa nchi hiyo. Hati hizo zilitolewa kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kivita na kukiuka haki za binadamu katika muktadha wa mapigano ya silaha yanayoendelea kati ya Israel na Hamas.

Mojawapo ya njia za kuwafuatilia wauaji na wahalifu wa Israel duniani kote ni kuandaa mashauri dhidi ya uhalifu mkubwa wa waharibifu wa Kizayuni. Jukumu hili liko juu ya mabega ya mawakili wote na wanaharakati wa sheria za kimataifa, ambao kwa kufungua mashtaka yanayozingatia ushahidi wa kisheria wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kurejesha haki za wananchi waliodhulumiwa wa Palestina.

Hatua hii, sambamba na kuwatambulisha Wazayuni kama wahalifu wa kivita, huweka vikwazo katika maisha na harakati zao katika nchi mbalimbali, na wakati mwingine huwaletea hali ya kutokuwa salama na vitisho wahusika wa uhalifu wa Kizayuni.

Inafaa kukumbushwa kuwa kwa msaada wa Marekani, wavamizi wa Kizayuni walianzisha mauaji ya kimbari huko Ghaza tangia Oktoba 2023, ambapo takribani Wapalestina 70,000 waliuawa kishahidi, na zaidi ya 171,000 walijeruhiwa na kupata ulemavu, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha