Ijumaa 23 Januari 2026 - 00:00
Kusimama dhidi ya haki husababisha mtu na jamii kuangamia/ Msisitizo juu ya kuutibu moyo uliochoka kwa hekima na dhikri

Hawza/ Mtukifu Ayatullah Jawadi Amoli amesisitiza: Yeyote anayesimama dhidi ya haki, bila shaka atashindwa; hata hivyo, kila mwanadamu katika mfumo huu wa uhai ana wajibu wa kutekeleza jukumu lake ipasavyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Jawadi Amoli katika kikao cha kila wiki cha darsa ya maadili la Mtukufu Ayatullah Jawadi Amoli kilifanyika asubuhi ya Jumatano, kwa ushiriki wa makundi mbalimbali ya wananchi, katika Msikiti Mkuu wa Qom Iran.

Katika kikao hicho, Mtukufu Ayatullah Jawadi Amoli, huku akifafanua kauli tukufu ya Amirul-Mu’minin (amani iwe juu yake): “Yeyote atakayejionesha wazi kwenye kuipinga haki, ataangamia,” alisisitiza kuwa haki ni ukweli wenye nguvu, thabiti na usioshindika, na mfumo mzima wa uhai unashuhudia manufaa ya haki. Kwa hiyo, kila mtu au jamii itakayosimama dhidi ya haki, imehukumiwa kuangamia na kushindwa.

Alisisitiza tena kwa kusema: Yeyote anayesimama dhidi ya haki, bila shaka atashindwa; lakini pamoja na hilo, kila mwanadamu katika mfumo huu wa uhai ana wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa usahihi.

Mtukufu huyo, huku akielezea kuwa, hakuna kiumbe katika mfumo wa uumbaji anayepotoka na kufanya dhambi kama binadamu, alisema: Kiumbe pekee ambacho wakati mwingine hutoka katika njia ya haki ni mwanadamu. Kupotoka huku ima kunatokana na ujinga (ujahili), ambao vyuo na hawza zina jukumu la kuuondoa, au kunatokana na upumbavu wa kimaadili wa mtu binafsi, ambao misikiti na husseiniyya zina wajibu wa kuutibu. Lakini jukumu kuu la mfumo wa uimamu na umma ni kuondoa hali ya ujinga wa kijamii (jahiliyyah), ambayo kwa msingi wake jamii huongozwa kuelekea haki.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Mtukufu Ayatullah Jawadi Amoli, huku akirejea hekima tukufu isemayo: “Hakika mioyo huchoka kama miili inavyochoka; basi itafutieni mioyo yenu mambo mapya ya hekima,”
alizungumzia suala la kuchoka na kuchoshwa kwa moyo, na akabainisha: Kama vile mwili huchoka na kuhitaji tiba, mapumziko na usimamizi, vivyo hivyo moyo pia wakati mwingine huchoka. Tiba yake ni kutumia hazina za hekima, mawaidha yenye busara, aya za Mwenyezi Mungu, munajati kama "Munajati ya Sha‘baniyya", na kushikamana kwa karibu na haram za Ahlul-Bayt watoharifu (amani iwe juu yao). Kwa sababu moyo unapochoka, mwanadamu hatanufaika ipasavyo na ibada yake.

Aliongeza kusema: Mkono na ulimi ni vyombo tu, na katika Siku ya Kiyama vitatoa ushahidi: “Siku ambazo ndimi zao, mikono yao na miguu yao itashuhudia dhidi yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”
Lakini moyo ndiyo asili ya mwanadamu, na ukizungumza, hilo huhesabiwa kuwa ni kukiri. Tofauti kati ya mkono na mguu na moyo ni kwamba moyo ni ukweli wa mwanadamu, ilhali mkono na mguu ni vyombo vyake. Kwa hiyo, ikiwa makosa kama rushwa, ufisadi na usaliti yatafanywa kwa mkono, siku ya Kiyama haitaelezwa kuwa mkono ulikiri, bali itasemwa kuwa ulishuhudia; kwa sababu usaliti umetoka moyoni, si mkononi wala ulimini.

Mtukufu huyo, akisisitiza kuwa moyo uliochoka humuingiza mwanadamu katika hali ya uchovu na msongo wa mawazo, alisema: Ubinadamu wa mwanadamu upo katika moyo wake, na kwa kuwa moyo huu hauhusiki isipokuwa na Muumba wa mioyo, ukishughulishwa na asiyekuwa Mwenyezi Mungu huingia katika hali ya kuchoka na mnyong’onyeo. Kwa hiyo, si kila kitu kinapaswa kuruhusiwa kuingia moyoni, ili usije ukaangukia katika ghafla.

Mwisho, Mtukufu Ayatullah Jawadi Amoli alibainisha: Moyo unapopatwa na mnyong’onyeo, una uwezo wa kujitibu, lakini unahitaji kukumbushwa na kutunzwa. Ushauri wa kujihesabu nafsi, pamoja na riwaya na mawaidha haya, yote ni vikumbusho na miito ya kuamsha fahamu, ambavyo ni bishara kwa moyo ili ghafla isipate nafasi ndani yake.

Mwisho wa kikao hiki, Mtukufu huyo aliomba dua kwa ajili ya mafanikio ya jamii, viongozi na mfumo wa Kiislamu chini ya mwongozo wa Qur’ani na Ahlul-Bayt (Atra).

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha