Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Mashia wa mji wa Makhachkala nchini Urusi imetoa tamko lenye kuunga mkono taifa la Kiislamu la Iran. Matini kamili ya tamko hilo ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu!
Sisi, wawakilishi wa Jumuiya ya Mashia wa mji wa Makhachkala, tunatangaza msimamo wetu wa kimsingi pamoja na wasiwasi wetu mkubwa kuhusu kuendelea kwa uingiliaji wa serikali za kigeni katika masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hatua kama hizo zinapingana na misingi ya sheria za kimataifa, zinadhoofisha nguzo za mamlaka ya dola, na zinahesabiwa kuwa tishio kwa uthabiti na amani katika ulimwengu mzima wa Kiislamu na hata nje yake.
Jumuiya ya Mashia wa Makhachkala daima inasisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru, ukamilifu wa ardhi ya nchi, na haki ya mataifa kuamua kwa uhuru njia ya maendeleo yao bila shinikizo au maelekezo ya kigeni.
Vilevile, tunatangaza kuunga mkono kikamili sera za Shirikisho la Urusi na kiongozi wa kitaifa wa nchi yetu, Vladimir Vladimirovich Putin, ambazo zimechukuliwa kwa lengo la kuendeleza mahusiano ya ujirani mwema, ya usawa na yaliyojengwa juu ya heshima ya pande zote na nchi jirani, hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Tunaamini kwamba ushirikiano wa kimkakati kati ya Urusi na Iran unachangia kuimarisha usalama wa kikanda, uthabiti, na kuundwa kwa mfumo wa haki wa dunia wa ngazi nyingi.
Mashia wa Dagestan wanathibitisha imani yao thabiti juu ya hekima ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khamenei, na pia katika mshikamano wa taifa la Iran kwa maadili ya umoja, fahari ya kitaifa na mamlaka ya nchi.
Tuna imani kamili katika nguvu ya kiroho ya mapambano ya taifa la Kiislamu la Iran katika kukabiliana na njama za maadui na nguvu za kibeberu pamoja na washirika wao, wanaotaka kudhoofisha mshikamano wa kijamii na kuharibu jamii ya Iran. Taifa la Kiislamu la Iran, linalofuata amri ya Mwenyezi Mungu ya kumtii Mungu Mtukufu, Mtume Wake (s.a.ww.) na Maimamu kutoka katika kizazi cha Mtume (saww), daima litakuwa chini ya ulinzi wa Imam Mahdi (as).
Msingi huu wa kiroho ni chanzo cha uthabiti, imani na yakini katika haki ya njia iliyochaguliwa. Tunaliombea taifa la Iran mafanikio, amani na maendeleo ya kina, na pia tunaomba kuimarishwa zaidi kwa mahusiano ya kindugu, ya kirafiki na ya kujenga kati ya Shirikisho la Urusi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa manufaa ya mataifa yetu na ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Kwa heshima, kwa niaba ya Jumuiya ya Mashia, Imamu wa Msikiti wa Waislamu Mashia wa mji wa Makhachkala, "Nouri Mohammad Zadeh".
Maoni yako