Jumanne 20 Januari 2026 - 17:00
Trump afahamu kwamba Mapinduzi ya Kiislamu hayawezi kulinganishwa na serikali au kundi lolote duniani/ Mamilioni ya watu wamesimama hadi tone la mwisho la damu zao kwenye kumlinda Kiongozi

Hawza/ Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran alisisitiza kwamba: Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ana wanajeshi wengi wa jihadi na wa kujitolea ulimwenguni kote, na aina yoyote ya tishio au kuidhalilisha heshima na hadhi yake tukufu kamwe haikubaliki kwa Umma wa Kiislamu, na mamilioni ya watu wamesimama tayari hadi tone la mwisho la damu yao kwa ajili ya kuilinda fikra hii safi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu nchini Iran, katika hafla ya kufunga Tamasha la 31 la Kimataifa la Qur’ani na Hadithi lililo andaliwa na chuo cha Al-Mustafa (s.a.ww) pamoja na hafla ya kumuenzi na kubainisha haiba ya Qur’ani ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, lililofanyika leo katika Ukumbi wa Quds wa Chuo cha Elimu ya Juu cha Imam Khomeini (r.a) mjini Qum Iran, alisema:

Katika uwanja wa Qur’ani Tukufu, kwa masikitiko makubwa, katika historia ya Uislamu tumeshuhudia kuzidisha kupita kiasi na kupunguza kupita kiasi (ifrat na tafrit) nyingi, na kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu na cha uongofu kimepungua nafasi yake katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii ya Umma wa Kiislamu.

Mjumbe wa Mafaqihi wa Baraza la wataalam wa uongizi aliongeza kusema: Kwa upande mmoja, nadharia ya “Hasbunā Kitābullāh” (kinatutosha Kitabu cha Mwenyezi Mungu) iliwekwa mbele ya Ahlul-Bayt, na Qur’ani ikatambulishwa bila mfasiri na mfafanuzi. Nadharia hii potofu ilisababisha machafuko mengi ya kifikra na ya vitendo, kwa hiyo, bila shaka, “Hasbunā Kitābullāh” ilikuwa upotofu mkubwa na mtazamo usio sahihi.

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu aliendelea kusema: Kwa upande wa pili kabisa, baadhi walitoa nadharia ya kuiweka kando Qur’ani na kuarifisha Hadithi kuwa ndiyo chanzo pekee cha mifumo ya Kiislamu; mfano wa wazi wa hilo ni Akhbariyyun, nadharia hizi mbili potofu hutuingiza katika mshangao na upotovu.

Qur’ani Tukufu na Ahlul-Bayt (a.s) ni njia ya wokovu wa Umma wa Kiislamu

Alisema: Tunaamini kwamba si Qur’ani Tukufu peke yake ndio chanzo ambacho hutufanya tusihitaji wafasiri wake, na wala si Hadithi peke yake ndio chanzo kinachotuondolea haja ya Qur’ani Tukufu. Kwa hiyo, "Thaqalayn"—yaani Qur’ani Tukufu na Ahlul-Bayt (a.s)—ndiyo njia ya wokovu kwenye Umma wa Kiislamu.

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu, akirejea ukamilishanaji wa Thaqalayn na Qur’ani kwa ajili ya wokovu na sa‘ada ya binadamu, alisema: Hivi viwili havipingani; si kwamba mmoja aielekee Qur’ani na azifumbie macho Hadithi, na mwingine azielekee Hadithi na aifumbie macho Qur’ani Tukufu.

Ayatullah A‘rafi aliongeza: Qur’ani na Thaqalayn ni amana mbili adhimu za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.ww) ambazo hukusanywa chini ya mwavuli mmoja, kwa masikitiko, baadhi waliifungamanisha Sunna na Sunna ya Mtume (s.a.ww) pekee na wakapuuza mwenendo wa Maimamu watoharifu (a.s), jambo ambalo bila shaka si sahihi. Kwa mantiki sahihi, tunaamini kwamba Sunna ya Mtume (s.a.ww) ina mwendelezo ambao hauonekani isipokuwa kwenye "Nahjul-Balagha", "Sahifa Sajjadiyya" na riwaya za Ahlul-Bayt watoharifu (a.s).

Vyanzo viwili — Qur’ani na Sunna — vinaonesha njia ya sa‘ada

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu alisema: Vyanzo viwili vya Qur’ani na Sunna vinaonesha njia ya sa‘ada. Huu ndio msingi wa ijtihadi yetu ya kifiqhi, ya kiakili na ya kielimu ya itikadi. Sunna ina wigo mpana unaoendelea katika mwenendo wa Ahlul-Bayt (a.s), kwa sababu wameunganishwa na wahyi. Yeyote atakae jinyima uzito huu mkubwa, amejinyima sa‘ada na furaha ya kweli.

Ayatullah A‘rafi alisema: Msingi wa harakati na shughuli zetu kwenye Hawza za Kielimu ni kanuni hizi zenye uwiano; kuzikusanya pamoja kunaweza kuwa mwongozo wa harakati na mwelekeo wa juhudi za kielimu na za vitendo. Jambo jingine ni kwamba tunapaswa kuitegemea Qur’ani.

Mjumbe wa Baraza la mafaqihi, akibainisha kuwa Qur’ani Tukufu imelindwa dhidi ya aina yoyote ya upotoshaji, alisema: Kitabu hiki cha Mwenyezi Mungu kimehifadhiwa dhidi ya kila aina ya tahrif, na hakuna mtu aliyeweza kuleta mabadiliko au upotovu ndani yake.

Tafsīr al-Mīzān ya Allama Tabatabai (r.a) ni kilele cha tafsiri na hatua kubwa ya kihistoria katika fikra za Kiislamu

Aliendelea kusema: "Tafsīr al-Mīzān" ya Allama Tabatabai (r.a) ni kilele cha tafsiri na ni hatua kubwa ya kihistoria katika fikra za Kiislamu na katika uga wa tafsiri. Kazi hii adhimu ni nukta ya mabadiliko na tukio adimu sana. Hata hivyo, leo, ikiwa mtu atakuwa na mtazamo wa ijtihadi na wa kina, anaweza kutoa mara kumi zaidi ya yaliyomo kutoka katika Qur’ani Tukufu kuliko Tafsīr al-Mīzān.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu alisema: Tafsīr al-Mīzān ni nukta ya mabadiliko ya karne nyingi za historia ya tafsiri ya Qur’ani Tukufu. Wajibu wa Hawza za Kielimu ni kusonga kuelekea upeo mpya katika uwanja wa Qur’ani. Uwezo huu upo ndani ya Qur’ani Tukufu, Ndio maana tunamuona Amirul-Mu’minin Imam Ali (a.s) katika Hotuba ya 198 ya Nahjul-Balagha akitaja takriban sifa 50 za kipekee kuihusu Qur’ani Tukufu.

Ayatullah A‘rafi aliongeza kuwa: Imam Ali (a.s) katika hotuba hiyo alisema: “Mwenyezi Mungu amewaaminisha amana hii na akaiteremsha; ni nuru ambayo mwangaza wake hautazimika kamwe, na kadiri dunia itakavyokuwepo na binadamu atakuwapo juu ya ardhi hii, mwanga huu utaendelea kuwaka na kuangaza.”
Kisha akasema: “Qur’ani ni nuru safi katika historia yote na ni bahari ambayo mwanadamu hatafikia kamwe kina chake. Ndani ya Qur’ani kuna tiba ambayo haitamrudisha mtu yeyote akiwa amekata tamaa; na yeyote atakayekusanyika chini ya kivuli cha Qur’ani Tukufu atapata heshima ambayo misingi yake haitaporomoka kamwe.”

Kiongozi wa Mapinduzi amekuwa na usuhuba wa karibu na Qur’ani tangu ujana wake

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu, akirejea haiba ya Qur’ani ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, alisema: Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi tangia ujana wake alikuwa na uhusiano wa karibu na Qur’ani Tukufu; uhusiano huu ulikuwa wa vitendo na wa kimaeneo, pamoja na wa kifikra na wa kinadharia. Kuwa karibu na Qur’ani katika ujana kumesisitizwa sana, na leo thamani ya wanafunzi wa Hawza za Kielimu ni kwamba tangia mwanzo wawe chini ya kivuli cha Qur’ani.

Ayatullah A‘rafi alisema: Ukaribu na mapenzi kwa Qur’ani Tukufu ni ukweli unaohitajika na kila kijana, mwanafunzi wa Hawza na wanafunzi wa vyuo vikuu. Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu tangia ujana wake alikuwa na uhusiano huu na Qur’ani Tukufu, na leo anasisitiza jambo hili.

Mjumbe wa Mafaqihi wa Baraza la uongozi aliongeza kuwa: Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika tafsiri amefuata njia ya kati. Wafasiri wengine hujishughulisha sana na maneno, istilahi na uchambuzi wa kina wa kifasihi na hubaki katika bahari hiyo; na kwa upande mwingine, wapo watu wenye mtazamo hai na mzuri kuhusu Qur’ani lakini hawana msingi imara. Fikra ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi imejengwa juu ya umakini wa maneno na misingi ya aya, na katika uwanja huu yeye hana mfano.

Kiongozi wa Mapinduzi ana mtazamo wa kimfumo wa kitamaduni kuhusu Qur’ani Tukufu

Ayatullah A‘rafi aliendelea kusema: Baadhi wana umakini mkubwa katika kuchambua aya za Qur’ani Tukufu lakini hawatoi tafsiri iliyo wazi; lakini Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ameunganisha mambo yote mawili. Aidha, ana mtazamo wa kimfumo wa kistaarabu kuhusu Qur’ani Tukufu.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu alisema: Mtazamo wa kisaikolojia na wa malezi ni miongoni mwa sifa nyingine za tafsiri ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi. Tafsiri yake ni ya ijtihadi, yaani haina mambo dhaifu na yasiyo na msingi, tafsiri ya Kiongozi ni kamili, hai na ya ijtihadi.

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu alisema: Imam Khamenei ni mfasiri ambaye kwa zaidi ya nusu karne amekuwa katikati ya matukio mbalimbali katika uwanja wa vitendo. Wapo watu wakubwa waliokaa pembeni wakazungumza maneno mazuri, na wapo waliokuwa watu wa medani ngumu; lakini yeye ana kina cha kielimu na pia amekuwapo na bado yupo katika medani ngumu za mapambano.

Tunashuhudia muunganiko wa fikra na medani katika nafsi yake.

Trump afahamu kwamba Mapinduzi ya Kiislamu hayawezi kulinganishwa na serikali au kundi lolote duniani

Ayatullah A‘rafi, akirejea maneno ya ovyo ya hivi karibuni ya Trump dhidi ya Kiongozi mwenye hekima wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: Trump ajue kwamba Mapinduzi ya Kiislamu hayawezi kulinganishwa na serikali hii au ile, wala kundi hili au lile duniani. Taifa la Iran na mkondo wa fikra za Kiislamu ni tofauti na mikondo mingine ambayo Marekani imeingia nayo kwenye migogoro, ikaendesha vita mia moja dhidi yao na ikaangamiza makumi ya nchi.

Mamilioni ya watu wamesimama hadi tone la mwisho la damu kumlinda kiongozi

Mkurugenzi wa hawaza alisema: Hili ni kosa la kimahesabu kulinganisha fikra ya Mapinduzi na uongozi wake adhimu na mikondo mingine duniani. Kwanza, maneno ya ovyo na uongo yaliyosemwa hivi karibuni yanamrudia msemaji wake mwenyewe. Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ana wanajeshi wengi wa jihadi na wenye kujitolea ulimwenguni kote, na aina yoyote ya tishio au kudhalilisha hadhi yake tukufu kamwe hakikubaliki kwa Umma wa Kiislamu, na mamilioni ya watu wamesimama hadi tone la mwisho la damu yao kwa ajili ya kuilinda fikra hii safi.

Ayatullah A‘rafi alihitimisha kwa kusisitiza: Leo, sauti hii inasikika na kuitikisa dunia na katika ulimwengu wa Kiislamu, na tutapita njia hii yenye nuru licha ya matatizo na magumu yote.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha