Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Mtoto imewadia huku mamilioni ya watoto katika maeneo yenye mapigano wakipitia hatua moja ya hatari zaidi katika historia ya kisasa; kiasi kwamba Ukanda wa Ghaza, Sudan, Syria na Yemen ziko mbele kabisa katika orodha ya maeneo yanayokiuka haki za watoto, huku kukiwa hakuna msaada wa kutosha, na idadi ya wahanga, mayatima na wakimbizi ikizidi kuongezeka.
UNICEF katika Siku ya Kimataifa ya Mtoto inakumbusha kuwa mamilioni ya watoto hawaishi maisha yao halisi, bali wanakabiliwa kila siku katika mapambano ya kupata haki zao za msingi kabisa: maji safi, makazi salama, lishe ya kutosha na huduma za afya.
Takwimu za hivi karibuni kutoka kwenye ripoti ya “Hali ya Watoto Duniani 2025” zinaonesha kuwa watoto zaidi ya milioni 417 katika nchi zenye kipato cha chini na kipato cha kati wanakosa takriban mahitaji mawili muhimu ya msingi.
Watoto wa Ghaza wanakabiliwa na hali isiyokuwa na mfano, kwani vita vya Israel vimesababisha maelfu ya watoto kutawanywa na kupoteza imma mzazi mmoja au wazazi wote wawili. Wakati huohuo, ripoti za Umoja wa Mataifa zinarejea viwango vya kutisha vya utapiamlo na ongezeko la idadi ya watoto wanaopata athari za kisaikolojia (msongo na mshtuko) kutokana na vita, uharibifu na mzingiro.
Siku ya Kimataifa ya Mtoto huko Ghaza imegeuka kuwa kumbukumbu ya maumivu; kumbukumbu ambayo wakazi wake hawaishereheki, bali wanapitia picha za wahanga waliopoteza maisha chini ya mabomu au wakati wakijaribu kufikia misaada.
Katika miaka miwili iliyopita, Sudan imekuwa kileleni mwa nchi ambazo ukiukwaji wa haki za watoto umeongezeka, kwa kuwa huduma nyingi muhimu katika maeneo makubwa ya nchi hiyo zimekatwa.
Huko Yemen, mateso ya watoto yanaendelea kutokana na utapiamlo mkali, uhaba wa chakula na kupungua kwa upatikanaji wa huduma za afya na elimu, kiasi kwamba mashirika ya kimataifa yameiweka hali ya watoto katika nchi hiyo miongoni mwa mbaya zaidi duniani. Watoto wengi wanaishi katika maeneo yasiyo na maji safi wala huduma za usafi, huku vifo vya watoto kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuiwa vikiendelea kuongezeka.
Ama huko Syria, maelfu ya watoto hadi leo, miaka mingi baada ya vita na kutawanyika, wanaendelea kufanya kazi katika mazingira hatari, huku hali ya kuacha shule ikienea na huduma za afya na elimu zikizidi kudidimia. Mandhari ya watoto wanaofanya sehemu zisizostahiki au katika karakana ndogo ndogo inaonesha kwa uchungu jinsi mifumo ya ulinzi wa kijamii ilivyoporomoka, na wakati huohuo idadi ya mayatima na watoto wanaoishi bila elimu wala uangalizi mwafaka ikiendelea kuongezeka.
Katika Siku hii ya Kimataifa ya Mtoto, hadithi za Ghaza, Syria, Sudan na Yemen zinakutana katika kiini kimoja: Watoto ambao badala ya kupata elimu na ulinzi, wanakabiliwa na vita, njaa na kutawanywa; na ahadi za kimataifa ambazo bado hazijageuka kuwa uhalisia utakaohakikisha haki yao ya kuishi kwa heshima.
Wakati wito wa kuwalinda watoto ukiendelea kutolewa, hali halisi bado imesimama katikati ya matumaini na kusahaulika, na inasubiri wakati ambao watoto hawa watatengeneza mustakabali ulio tofauti na leo uliojaa misiba.
Maoni yako