Shirika la Habari la Hawza - Mojawapo ya maagizo muhimu katika Uislamu ni suala la amana na uaminifu, Qur’ani Tukufu inasema:
{إِنَّ ٱللَّهَ یَأۡمُرُكُمۡ أَن تُؤَدُّوا۟ ٱلۡأَمَـٰنَـٰتِ إِلَىٰۤ أَهۡلِهَا}“Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni muwarudishie watu amana zao.” (1)
Sherehe:
Kuhusu suala muhimu la uaminifu, tunaweza kulitazama katika nyanja mbili:
1. Amana za kidunia ambazo watu hukabidhiana wao kwa wao;
2. Amana za kiroho ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu amemkabidhi mwanadamu.
Amana hizi zote mbili zina hadhi kubwa sana katika Uislamu.
Amana za Kiroho:
{ إِنَّا عَرَضۡنَا ٱلۡأَمَانَةَ عَلَى ٱلسَّمَـٰوَ تِ وَٱلۡأَرۡضِ وَٱلۡجِبَالِ فَأَبَیۡنَ أَن یَحۡمِلۡنَهَا وَأَشۡفَقۡنَ مِنۡهَا وَحَمَلَهَا ٱلۡإِنسَـٰنُۖ إِنَّهُۥ كَانَ ظَلُومࣰا جَهُولࣰا }
“Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na milima; na vyote hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanaadamu akaichukua. Hakika yeye amekuwa dhaalimu mjinga.” (2)
Aya hii huenda inazungumzia ukweli kuhusu mwanadamu, ukweli ambao akili ya binadamu bado haijaufikia. Lakini kutokana na maelezo ya nje ya aya, tunafahamu kwamba Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu sifa na uwezo maalumu, sifa ambazo hakuna kiumbe mwingine mbinguni wala ardhini anazo. Uwezo huu ni amana ya Kimungu na inambebesha mwanadamu jukumu kubwa. (3)
Hata hivyo, wengi wametenda khiyana katika amana hii, wakaitumia kinyume na matakwa ya Mungu. Akili na hiari ambazo zilipaswa zitumike katika kutambua haki na kuichagua ili ziwe sababu ya ustawi na ukamilifu wa mwanadamu, zimeelekezwa katika njia za upotovu.
Katika tafsiri mbalimbali, zimetajwa maana kadhaa za amana hii — ikiwemo: akili, fitra, viungo vya mwili, hiari, neema ya uongozi wa Kiilahi (wilaya), cheo cha ukhalifa, uongofu wa mitume, majukumu ya kidini, neno “La ilaha illa Allah”, siri za Kimungu, na mengineyo.
Hapa tutazungumzia aina moja tu ya amana ya Kimungu iliyoelezwa katika tafsiri hizo, amana kwa maana ya (viungo vya mwili wa binadamu).
Mwanadamu anapaswa kutumia viungo vyake katika njia aliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kuwa viungo hivi ni amana zitakazorejeshwa kwake siku moja.
Imam Khomeini (ra) amesema kuhusu jambo hili:
“Iwapo hamtajiweka sawa, na mkafa huku mioyo yenu ikiwa meusi, macho, masikio, na ndimi zenu zikiwa zimechafuliwa na madhambi, mtamkutanaje na Mungu? Amana hizi za Kimungu alizowakabidhi kwa usafi na utukufu mtazirudishaje kwa uchafu na najisi? Macho, masikio, mikono, ndimi, na viungo vyote mnavyoishi navyo ni amana za Mungu Mtukufu alizowapa kwa usafi na uadilifu. Iwapo vitatumbukia katika maasi, vitachafuliwa; vikijihusisha na haramu, vitadhalilika. Na wakati wa kuzirudisha amana hizi, huenda mkaulizwa: Je, huu ndio uaminifu katika amana? Je, tulikukabidhi moyo huu ukiwa hivi? Jicho tulilokupa lilikuwa hivi? Viungo tulivyokupa vilikuwa vichafu namna hii? Mtawezaje kumkabili Mungu wenu huku mmefanya khiyana katika amana Zake?” (4)
Ushuhuda wa Viungo vya Mwili Siku ya Kiyama
Kinachoongeza umuhimu wa suala hili ni kwamba viungo hivi vitatoa ushahidi dhidi ya mwanadamu Siku ya Kiyama. (5) Kama Qur’ani Tukufu inavyosema:
{ یَوۡمَ تَشۡهَدُ عَلَیۡهِمۡ أَلۡسِنَتُهُمۡ وَأَیۡدِیهِمۡ وَأَرۡجُلُهُم بِمَا كَانُوا۟ یَعۡمَلُونَ}
“Siku ambayo ndimi zao, mikono yao na miguu yao vitashuhudia dhidi yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. (6) ”
Hivyo basi, mwanadamu hugeukia mojawapo ya viungo vyake na kuuliza sababu ya ushahidi wake:
{ حَتَّىٰۤ إِذَا مَا جَاۤءُوهَا شَهِدَ عَلَیۡهِمۡ سَمۡعُهُمۡ وَأَبۡصَـٰرُهُمۡ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا۟ یَعۡمَلُونَ. وَقَالُوا۟ لِجُلُودِهِمۡ لِمَ شَهِدتُّمۡ عَلَیۡنَاۖ قَالُوۤا۟ أَنطَقَنَا ٱللَّهُ ٱلَّذِیۤ أَنطَقَ كُلَّ شَیۡءࣲۚ وَهُوَ خَلَقَكُمۡ أَوَّلَ مَرَّةࣲ وَإِلَیۡهِ تُرۡجَعُونَ }
“Hata watakapo ufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyo kuwa wakiyatenda. Na wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Nazo zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliye kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu mtarejeshwa.’” (7)
Fikiria! Ngozi hii tunayolinda kwa uangalifu, tunayoihifadhi kutokana na joto na baridi — siku moja itashuhudia dhidi yetu. Ngozi hii hii tunayo ipamba kwa krimu na mapambo mbali mbali siku moja itashuhudia dhidi yetu katika mahakama ya haki ya Mungu!
Kwa hivyo, mikono, miguu, ulimi, na viungo vyote vya mwanadamu ni amana zilizo mikononi mwake kwa muda mfupi tu. Iwapo hatavitumia ipasavyo, vitazungumza dhidi yake mbele ya Mola wake na kumsababishia fedheha na aibu.
Lakini jambo la kushangaza ni hili: tunaposema “mimi”, je, huyu “mimi” siyo mkusanyiko wa viungo hivi? Basi kwa nini Qur’ani inasema tutazungumza na viungo vyetu na kuviuliza sababu ya kutoa kwao ushahidi dhidi yetu?
Jibu linaweza kuwa kwamba; ukweli wa “mimi” ni roho ya mwanadamu — viungo vya mwili ni zana tu katika mikono ya roho hii. Kwa maneno mengine, kile tunachoona tunaposimama mbele ya kioo siyo “mimi” wa kweli, bali ni chombo cha kimwili tulichokabidhiwa kwa muda mfupi tu kama amana.
Ni “mwili” huu unaoonekana kwenye kioo ambao utashuhudia dhidi yetu, si “mimi” halisi. Hivyo basi, lazima tutumie mwili huu kwa njia bora katika kufikia malengo ya Kimungu, la sivyo, utatufedhehesha kwa ushahidi wake mbele ya Mola.
Rejea:
1. Sura An-Nisa, aya ya 58.
2. Sura Al-Ahzab, aya ya 72.
3. Tafsiri Nur.
4. Jihadi Akbar, uk. 60.
5. “Ushahidi wa viungo vya mwili siku ya Kiyama daima ni dhidi ya mwanadamu, si kwa niaba yake.” — Tafsiri Nur.
6. Sura An-Nur, aya ya 24.
7. Sura Fussilat, aya za 20–21.
Imeandaliwa na Idara ya Elimu na Utamaduni ya Shirika la Habari la Hawza.
Maoni yako