Jumanne 11 Novemba 2025 - 23:22
Hujjatul-Islam Fadhlallah Atoa Onyo kwa Serikali ya Lebanon

Hawza/ Mwanazuoni mashuhuri wa kidini nchini Lebanon, Hujjatul-Islam Sayyid Ali Fadhlallah, amesisitiza kuwa serikali ya Lebanon inapaswa kusimama imara dhidi ya masharti au matakwa yoyote yatakayohatarisha mamlaka na umoja wa ardhi ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Sayyid Fadhlallah alibainisha kuwa; mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na Israel kusini mwa Lebanon na vitisho vinavyozidi kuongezeka dhidi ya mamlaka ya taifa ni jambo linalohitaji msimamo thabiti wa serikali.

Ameitaka serikali ya Lebanon kupinga masharti yeyote yanayokiuka uhuru wa taifa, akisisitiza umuhimu wa kulinda hadhi na mamlaka kamili ya nchi.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa Lebanon kuacha tofauti za ndani na kushikamana ili kukabiliana na lengo kuu la adui — ambalo ni kulazimisha matakwa yake na kudhoofisha taifa kwa ujumla.

Mashambulizi ya kijeshi na lengo la kuishinikiza serikali

Hujjatul-Islam Fadhlallah alisema kuwa; mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel kusini mwa Lebanon, mauaji ya raia, na uvunjaji wa mamlaka kupitia ndege za kivita na ndege zisizo na rubani (drone), yote haya yanakwenda sambamba na vitisho vya viongozi wa Kizayuni vya kupanua vita hadi katika mji mkuu wa Lebanon.

Akasema kuwa ni wazi adui anajaribu kuiwekea serikali shinikizo kubwa ili ikubali masharti yake, hatua ambayo inalenga kudhoofisha nguvu za ndani za upinzani na kuongeza migawanyiko ya kijamii na kisiasa.

Wito kwa serikali na wananchi

Sayyid Fadhlallah alihimiza serikali kudumisha msimamo wake wa kutokukubali masharti yoyote yanayolenga mamlaka au ardhi ya Lebanon. Alisisitiza kuwa Lebanon imekuwa ikiheshimu masharti ya makubaliano ya kusitisha vita, huku Israel ikichelewesha utekelezaji wa wajibu wake kama vile kuondoa majeshi na kuwaachilia wafungwa. Aidha, alitoa wito wa kuimarisha juhudi za kidiplomasia ili kuzuia vitendo vya kichokozi vipya vinavyofanywa na Israel.

Pia alitoa wito kwa wananchi wa Lebanon kuwa waangalifu zaidi kutokana na njama za adui na kuficha tofauti za ndani, ili wasiweze kudhoofishwa au kulazimishwa kukubali masharti ya udhalilishaji.

Akiashiria kwa masikitiko, alisema kuwa baadhi ya watu bado wanayaona mambo kwa mtazamo wa kisiasa au wa kimadhehebu, ilhali lengo la adui ni kutawala taifa lote, kuharibu mamlaka na kudhoofisha umoja wa kitaifa.

Sayyid Fadhlallah alibainisha kuwa dhana ya mamlaka ni moja isiyogawika, na Lebanon inaweza kuwa na mamlaka kamili tu kwa kulinda ardhi, anga na bahari yake, ikizingatia vipengele vyote vya taifa — kaskazini, kusini, Bekaa na katikati ya nchi.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alizungumzia suala la ujenzi upya wa maeneo yaliyoharibiwa na vita vya Israel, akilisifu jopo la kitaifa lililoundwa kwa ajili hiyo, na kuwataka viongozi kuhakikisha ujenzi huo unakuwa jukumu la kitaifa, si jambo la kimadhehebu au la kikanda, ili adui asitumie fursa hiyo kupata manufaa yoyote kisiasa au kijeshi.

Vilevile, Sayyid Fadhlallah alionyesha wasiwasi wake kuhusiana na vita na mauaji ya kutisha nchini Sudan, akizitaka nchi za Kiarabu zenye ushawishi zichukue hatua za haraka kukomesha umwagaji damu na kulinda rasilimali za taifa hilo.

Kuhusiana na hali ya Ghaza baada ya makubaliano ya kusitisha vita, alisema: Israel bado inaendelea kuyakiuka makubaliano hayo kwa kushambulia miundombinu na kuchelewesha utoaji wa misaada muhimu, akisisitiza kuwa mataifa yanayounga mkono makubaliano hayo yanapaswa kuingilia kati kuhakikisha utekelezaji wake kamili, na kuzuia Giaza isigeuzwe kuwa uwanja wa ugaidi wa utawala wa Kizayuni unaolenga kuuharibu kabisa Ukanda wa Ghaza na kuwafukuza wakazi wake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha