Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, matini ya tamko la Ayatullah A‘rafi, Mkurugenzi wa hawza nchini Iran, katika kulaani jinai ya kikatili dhidi ya watu wanyonge wa Sudan, ni kama ifuatavyo:
Bismillahi al-Rahmani al-Rahim
Katika siku hizi ambazo ulimwengu wa Kiislamu unahitaji kwa dharura ushirikiano, uthabiti na utulivu ili kufikia maendeleo ya pande zote, pamoja na umoja na hatua za pamoja za kuwaunga mkono wananchi wanyonge wa Palestina dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel, habari na picha za kutisha kuhusu mauaji ya halaiki dhidi ya watu wanyonge wa Sudan na uhamaji wa makumi ya maelfu miongoni mwao zimeumiza mioyo ya wanadamu wenye dhamiri katika kila kona ya dunia.
Janga hili la kusikitisha ni mfano wa wazi wa miradi mibaya ya maadui wa Umma wa Kiislamu, inayolenga kuchochea migawanyiko, kudhoofisha nchi za Kiislamu, kuzigawa na kupora mali na rasilimali zao. Nyuma ya matukio haya machungu na yenye kuumiza, daima kuna mikono na ushiriki wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja wa ubeberu wa kimataifa na utawala dhalimu wa Israel.
Hawza ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wanazuoni wa Kiislamu, pamoja na kulaani vikali jinai hizi za kikatili, wanazitaka serikali na mataifa ya Kiislamu pamoja na wasomi wa ulimwengu wa Kiislamu, kutonyamaza mbele ya maafa kama haya; bali wachukue tahadhari na utambuzi kuhusu njama na mikono michafu ya nguvu za kibeberu na uzayuni wa kimataifa, na wayalinde malengo ya uhuru, heshima na uadilifu katika nchi za Kiislamu, hususan Sudan.
Tunatarajia pia kwamba jumuiya za kimataifa, Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu, na taasisi za haki za binadamu zitachukua misimamo thabiti mbele ya janga hili la kibinadamu, na kuchukua hatua madhubuti za kukomesha umwagaji damu na uhamaji wa watu wanyonge wa Sudan.
Mwisho, tunatoa pole na rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kwa taifa lenye kudhulumiwa la Sudan, na tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape subira na ushindi, na auhifadhi Umma wa Kiislamu kutokana na fitina na tamaa za utawala wa madhalimu.
Wassalamu ‘alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh
Alireza A‘rafi
Mkurugenzi wa Hawza za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Maoni yako