Kwa mujibu wa kitengo cha habari za kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, wiki iliyopita, sambamba na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Bibi Zaynab (as), Msikiti na Kituo cha Kitamaduni cha Zainabiyya kilifunguliwa rasmi katika hafla ya kimataifa. Sherehe hiyo ilihudhuriwa na wageni kutoka ndani na nje ya Uturuki, na ilisisitizwa juu ya dhana za umoja, udugu na imani.
Hafla ilianza kwa kisomo cha aya takatifu za Qur’ani Tukufu kilichosomwa na msomaji mashuhuri kutoka Iran, Abu al-Qasimi. Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na Naibu wa Rais wa Uturuki, Cevdet Yılmaz, na Mwenyekiti wa Chama cha "Republican People’s Party", Özgür Özel.
Aidha, wawakilishi mashuhuri kutoka vyuo vya kiislamu na taasisi za kidini za nchi mbalimbali walishiriki katika hafla hiyo, akiwemo:
Mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Ali Qazi Askar;
Mwakilishi wa Ayatullah Makarim Shirazi, Dkt. Masoud Makarim Shirazi;
Mwakilishi wa Ayatullah Jawadi Amoli, Hujjatul Islam Sayyid Suleiman Mousavi;
Mwakilishi wa Ayatullah Bashir Najafi, Hujjatul Islam Muhammad Tarfi;
Mwakilishi wa Ayatullah Yaqubi, Sheikh Nasrullah;
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa ya Utafiti wa Ushia, Dkt. Ayat Peyman;
Na mwakilishi wa Ayatullah Safi Golpaygani, Hujjatul Islam Mirdamadi, na wengineo.
Wageni kutoka Iraq na Lebanon, wawakilishi wa vyama vya kisiasa, viongozi na wakurugenzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, pamoja na maelfu ya wapenda Ahlul-Bayt (as) pia walihudhuria hafla hiyo.
Hujjatul Islam wal-Muslimin Qazi Askar, mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alisema katika hotuba yake:
“Kama mnavyojua, nchi hizi mbili rafiki na ndugu — Iran na Uturuki — zimekuwa na uhusiano wa karibu na mafungamano madhubuti katika historia yao. Mtazamo wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi pamoja na wanazuoni na wakubwa wengine ni kuendeleza na kuimarisha zaidi mafungamano haya ya kindugu. Aya za Qur’ani, hadithi na mwenendo wa Ahlul-Bayt (as) vinaonesha kwamba misikiti ni vituo vya malezi ya maadili na ufundishaji wa thamani za kibinadamu.”
Katika hafla hiyo pia, ujumbe wa pongezi kutoka kwa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, ulisomwa.
Jengo la msikiti huo, lililojengwa kutokana na kumbukumbu ya mashahidi 72 wa Karbala, lina eneo la mita za mraba 72,000 lililofunikwa, na likihesabiwa pamoja na uwanja wake (sahn), lina uwezo wa kuruhusu watu elfu arobaini (40,000) kuswali kwa wakati mmoja.
Ujenzi wa msikiti huu ulianza mwaka 2009, na taasisi mbalimbali zimeshirikiana katika hatua za ujenzi wake.
 
             
                
Maoni yako