Jumapili 19 Oktoba 2025 - 00:10
Hakuna jukumu lolote linalopaswa kumtenga mwanafunzi wa Hawza na tabligh/ Tabligh ni risala ya kimungu, si ajira

Hawza/ Katibu wa pili wa Baraza Kuu la Hawza, Ayatullah Jawad Marvi, amesisitiza kwamba hakuna jukumu au cheo chochote kinachopaswa kumtenga mwanafunzi wa Hawza na kazi ya tabligh, akibainisha kuwa katika historia yote ya Shia, wanazuoni na viongozi wa dini wameutazama ulinganiaji kuwa ni risala takatifu ya kimungu, si kazi ya ajira.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza,, hotuba hiyo ilitolewa katika hafla ya ufunguzi wa kozi ya mafunzo na utambulisho kwa viongozi wa kitaasisi na wa utekelezaji wa tabligh na shughuli za kitamaduni, iliyofanyika katika ukumbi wa Ghadir wa kituo cha Yavaran Mahdi mjini Qom Iran. Hafla hiyo iliandaliwa na Idara ya Tabligh na Masuala ya Kitamaduni ya Hawza, kwa ushiriki wa wasaidizi wa tabligh wa mikoa, wilaya na waratibu wa shule zinazoshiriki katika mpango wa Amin.

Tabligh ni nguzo ya kudumu na uhai wa dini

Ayatullah Marvi alisema: “Uislamu, ambao ni sheria kamili na kamilifu zaidi miongoni mwa sheria za mbinguni, ulianza kwa tabligh, ukaendelea kwa tabligh, na umedumu hadi leo kwa nguvu ya tabligh. Uhai na uimara wa dini umetokana na juhudi za wahubiri wakubwa walioyatoa maisha yao kwa ajili ya kueneza fikra za Ahlul-Bayt na kuwaongoza waja wa Mungu.”

Akaongeza kuwa ueneaji na upanuzi wa madhehebu ya Shia katika pembe zote za dunia ni matokeo ya kazi kubwa ya maulamaa na wahubiri waliobeba jukumu hilo kwa dhati.
“Leo tunaona wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s.) wapo duniani kote, na yote haya ni kwa baraka za kazi ya tabligh,”.

Lengo kuu la dini ni kufikisha maarifa kwa watu

Mjumbe huyo wa Jami‘at al-Mudarrisin ya Hawza ya Qom alisema kwamba; kufikisha mafundisho ya dini kwa watu ndilo lengo la mwisho la dini.
Akinukuu maneno ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (Mola amuhifadhi) alisema: “Utume wa Mtume (s.a.w.w), jihadi, vita katika njia ya Allah, na kuunda serikali ya Kiislamu – yote haya ni maandalizi ya kufikisha ukweli wa dini katika nyoyo safi za watu.”

Tabligh ni risala, si kazi ya kupata riziki

Ayatullah Marvi alisisitiza kuwa wanazuoni wakubwa wa Shia daima wameichukulia tabligh kuwa ni jukumu la kimungu na si taaluma ya kimaisha.
“Katika historia ya Shia, hakuna mwanazuoni aliyeliona tabligh kuwa ni kazi ya kulipwa, bali ni risala ya kupokezwa kutoka kwa Mitume na Maimamu,”.

Umuhimu wa kulea wahubiri kamilifu

Akisisitiza haja ya kupanga programu za kulea wahubiri kamilifu, alisema: “Mhubiri anapaswa kuwa na ukamilifu wa kielimu na kimaadili, kwa sababu watu hutegemea kupata majibu ya maswali yao ya kidini na kijamii kutoka kwake.”
Akaongeza kuwa kuboresha uwezo wa kielimu wa wahubiri ni jambo la msingi, na akahimiza wadau wa tabligh kutoa mapendekezo yao kwa Baraza Kuu.
“Baraza Kuu liko tayari kupokea maoni na ukosoaji wenu, kwani sera haziwezi kubuniwa bila ya kitu”.

Nahjul-Balagha na Sahifa Sajjadiyya – mihimili miwili mikuu ya tabligh kwa Shia

Ayatullah Marvi aliitaja Nahjul-Balagha na Sahifa Sajjadiyya kuwa ni mihimili mikuu miwili kwenye ulinganiaji wa Shia baada ya Qur’an Tukufu.
Akinukuu mitazamo ya wanazuoni wakubwa wa Shia na Sunni kuhusu thamani ya vitabu hivyo, alisema:
“Kwa msaada wa Nahjul-Balagha na Sahifa Sajjadiyya, Ushia unaweza kufungua mioyo ya watu duniani. Ni lazima tuzidishe mazoea na ukaribu na vitabu hivi viwili vya kiroho.”

“Mhubiri ni kielelezo cha dini kwa vitendo”

Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatullah Marvi alisisitiza kuwa hakuna jukumu lolote linalopaswa kumtenga mwanafunzi wa Hawza na tabligh, akiwahimiza wahubiri kuwa mfano wa maadili wanayoyahubiri.
Alisema: “Katika tabligh, kuitakasa nafsi na kutenda yale mnayoyasema ni jambo lenye athari kubwa. Watu kwanza huangalia tabia na nuru ya kiroho iliyo ndani yetu kabla ya kusikiliza maneno tunayoyasema.”

Kozi hii ya mafunzo kwa viongozi wa tabligh inalenga kuboresha uwezo wa kielimu, kiroho, na kimuundo kwa wahubiri na wasimamizi wa shughuli za kidini katika maeneo mbalimbali nchini.

Maoni yako

You are replying to: .
captcha