Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Msikiti Mtukufu wa Kufa, ukiwa miongoni mwa vituo muhimu zaidi vya ibada na utamaduni kwenye ulimwengu wa Kiislamu, hupokea maelfu ya watu wanaojitenga kwa ajili ya ibada (muta‘akifīn) kutoka pande zote za dunia kila mwaka. Kufuatia maandalizi yaliyofanyika, Ghaith Auwad Muhammad Al-‘Adli, kwa kutuma waraka rasmi wa mwaliko, amewaalika waumini wote wenye mapenzi ya ibada kushiriki katika itikafu ndani ya mazingira tulivu, yenye utulivu wa kiroho na ukaribu na Mwenyezi Mungu.
Katika mwaliko huo, akiwa amemnukuu Mwenyezi Mungu katika aya ya 125 ya Suratul Baqarah, ameeleza kuwa itikafu ni fursa ya kuwa faragha na Mola, kujitakasa nafsi, na kujitenga na kelele na misukosuko ya dunia. Pia amesisitiza kwamba Msikiti Mtukufu wa Kufa umeandaa huduma zote muhimu kwa ajili ya ustawi wa wale watakaoshiriki katika ibada hiyo tukufu.
Matini kamili ya mwaliko huo ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
{وَعَهِدنَا إِلَىٰۤ إِبۡرَ هِـيمَ وَإِسمَـعِیلَ أَن طَهِّرَا بَیتِیَ لِلطَّاىِٕفِینَ وَٱلعَـٰكِفِینَ وَٱلرُّكَّعِ ٱلسُّجُودِ }"Na tulimpa Ibrahimu na Ismaili kiaga kwamba: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa kut'ufu na wanao jitenga huko kwa ibada, na wanao inama na kusujudu.
[Surah Al-Baqarah: 125]
Itikafu ni kituo cha kusafisha roho, ambacho ndani yake mwanadamu humgeukia Mwenyezi Mungu na kujitenga na misukosuko ya dunia. Ni ahadi tukufu kati ya mja na Mola wake; ahadi ambayo anayefanya itikafu hukaa katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu akitafuta radhi Zake, akiwa na matumaini kwamba kama Nyumba ya Mwenyezi Mungu inavyotakaswa kwa ajili ya wanaozunguka na wanaokaa humo, basi moyo wake nao utatakaswa kutokana na uchafu na maovu yote.
Falsafa ya itikafu inajengwa juu ya tafakuri na kujitenga; ni fursa ya kuondoa huzuni moyoni na kujitakasa kwa njia ya kurejea kwenye Qur’ani na dua. Itikafu inatukumbusha kwamba utulivu wa kweli haupatikani ila chini ya kivuli cha Mwenyezi Mungu, na kama vile mwili unavyohitaji chakula, vivyo hivyo roho inahitaji lishe ya kiroho.
Itikafu ni safari fupi lakini yenye kina, yenye lengo la kujenga daraja imara kati ya moyo wa mwanadamu na Muumba wake. Mtu anaerejea kutoka katika safari hii, hurejea akiwa na roho mpya na imani iliyotukuka zaidi, tayari kwa maisha mapya yenye nuru ya kiroho.
Kwa misingi hiyo, Msikiti Mtukufu wa Kufa umeamua kulipa kipaumbele maalumu jambo hili la itikafu, kwa kuwa lina athari kubwa katika nyanja za kidini, kijamii na kimaadili.
Msikiti huu wa kihistoria kila mwaka hupokea maelfu ya mahujaji na wanaojitenga kwa ajili ya ibada kutoka zaidi ya nchi kumi duniani kote.
Msikiti Mtukufu wa Kufa umeandaa huduma zote muhimu kwa ajili ya waumini watakaoshiriki katika itikafu hiyo tukufu.
Kutoka katika eneo hili takatifu, ninawakaribisha nyote kushiriki katika itikafu ya mwaka huu kwenye Msikiti Mtukufu wa Kufa au Msikiti wa Hanana, ili mfaidi baraka za ibada hii. Sisi tupo tayari kuwahudumia, In shaa Allah.
Maoni yako