Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Jiji la Daresalamu jana lilishuhudia umati mkubwa wa waislamu ambao ni waumini wa madhehebu ya kishia wakimiminika barabarani kwa ajili ya matembezi ya amani, huku wakiomboleza kutokana na maswaibu ambayo yalimpata Imam Husein (as) katika ardhi ya Karbala
Katika maombolezo hayo ambayo yaliandaliwa na mashia wenye asili ya kihindi wajulikanao kama Khoja, umati mkubwa wafuasi wa Ahlulbyt (as) walihudhuria huku akiwepo Sheikh Jalala ambae ni Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), pamoja na sura nyengine mashuhuri kama vile msimamizi mkuu wa Taasisi ya Almusta nchini Tanzania Dkt Ali Taqavi, pamoja na waumini wengine wengi.
Kwenye muendelezo wa matembezi hayo Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania, alitoa ujumbe rasmi wa matembezi hayo kwa kusema kwamba: Sababu kubwa ambayo imepelekea umati huu mkubwa leo uonekane barabarani, ni lile jambo ambalo Imam Husein (as) aliuwawa kwa ajili yake, katika muendelezo wa hutuba yake alinikuhu maneno ya Imam Husein (as) yasemayo:
ان كان دين محمد لم يستقم الا بقتلي فيا سيوف خذيني
Katika kuyaelezea maneno hayo Sheikh huyo alisema kuwa: Unapoyarejea maneno ya mtukufu huyu unabaini kwamba, sababu kubwa ambayo ilimfanya Imamu Husein (as) atoke na kuelekea katika ardhi ya Karbala ni dini hii ya uislamu, lau kama Imam Husein (as) asingejitolea nafasi yake katika ardhi ya Karbala basi huu uislamu tunao uona leo hii tusingelikuwa nao.
Baadhi ya waumini mbalimbali waliojitokeza kushiriki kwenye matembezi hayo
Vile vile Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), pia alieleza kwamba; Kando na hilo la kuutetea Uislamu, sababu nyengine iliyo mfanya Imam Husein (as) auwawe katika ardhi ya Karbala ni kuhakikisha umati wa Mtume Muhamad (saw) unashikana na kuwa kitu kimoja, katika kulielezea hili pia alinukuhu aya ya Mwenyezi Mungu isemayo:
واعتصموا بحبل الله جميعا ولا تفرقوا
Kwenye kuielezea aya hii alisema kwamba: Unaporejea msafara wa Imam Husein (as) unakutana na majina kama vile John, hii inaonesha dhahiri kwamba Imam Husein (as) alijikita zaidi kuhakikisha umma huu unashikamana na kuwa kitu kimoja, hivyo basi nasi pia yatupasa kuhakikisha juhudi hizi alizo zionesha Imam Husein hatuziachi bali tunazidumisha kwa vitendo.
Leo hii pia kunatarajiwa kufanyika matembezi mengine makubwa zaidi ya maombolezo ya shahada ya Imam Husein (as), kwenye mikoa mbalimbali nchini humo.
Maoni yako