Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, alihudhuria katika Mkutano wa Kitaifa wa "Ahadi ya Pamoja kuelekea Ustaarabu Mpya wa Kiislamu", uliofanyika katika Chuo cha Hawza cha Feiziyeh, mjini Qom Iran. Mkutano huo uliandaliwa katika kuadhimisha Wiki ya Basij na kumbukumbu ya mwaka wa amri ya kihistoria ya Imam Khomeini (q.s.) ya kuanzishwa Basij ya wanafunzi wa Hawza na vyuo vikuu, huku ukihudhuriwa na viongozi na watu mashuhuri kutoka katika taasisi za Hawza na vyuo vikuu.
Akizungumzia umuhimu wa nafasi ya Hawza na vyuo vikuu katika mabadiliko ya kijamii na mifumo ya utawala, alisema: "Hawza inapaswa kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu mifumo ya kijamii na iweze kuandaa mafaqihi wenye uelewa wa kimuundo kuhusu mifumo hiyo, ili waweze kusimamia jamii kwa misingi ya fikra za Kiislamu."
Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu alisema kuwa, dira hii inaweza kuwa msingi wa kuundwa na kuimarishwa Basij ya wasomi sambamba na Hawza na vyuo vikuu, kisha akaongeza: "Mojawapo ya maeneo muhimu ya ushirikiano kati ya Hawza na vyuo vikuu ni kushiriki katika kubuni mifumo ya kijamii na kutoa mifano inayolingana na misingi ya Kiislamu kwa ajili ya kusimamia jamii."
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran aliendelea kusema kuwa, vyuo vikuu navyo, katika eneo la sayansi za kibinadamu na kwa kuhusiana na mifumo ya utawala na mifumo ya kijamii inayoshirikisha wananchi, vinapaswa kuchunguza na kubainisha kwa usahihi elimu iliyopo duniani, kutofautisha yaliyo sahihi na yasiyo sahihi, na kwa kushirikiana na Hawza, kuwasilisha maudhui ya fikra za kidini kwa namna inayofaa na yenye uthabiti wa kielimu.
Basij: Uhalisia Unaovuka Jina na Cheo
Ayatollah Arafi, akifafanua dhati ya Basij na roho inayoiendesha, alisema kuwa; Basij si jina la kawaida au cheo kinachotumiwa tu, bali ina maana pana zaidi.
Alisema: "Uhalisia wa mtu mwenye roho ya Basij tangu mwanzo umekuwa ni uhalisia wenye mwanga unaong'aa. Roho ya Basij ni ileile roho ya kusimama imara katika njia ya Uislamu na Mapinduzi, kuambatana na uongozi na taifa la Iran, pamoja na kushiriki katika miamko mikubwa ya zama mpya."
Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu, akisisitiza umuhimu wa kufanya upya ahadi katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu, aliongeza: "Leo, tukiwa pamoja, tunaweka ahadi kwamba katika njia ya Uislamu na Mapinduzi, tutaendelea kuwa pamoja na Kiongozi Mkuu na taifa la Iran, na tutasimama imara katika harakati mpya iliyoanza kwa ajili ya kuandaa mustakabali tofauti."
Tofauti ya Kimsingi Kati ya Mapinduzi ya Kiislamu na Harakati Nyingine za Kisiasa na Kijamii
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akizungumzia tofauti ya kimsingi kati ya Mapinduzi ya Kiislamu na harakati nyingine za kisiasa na kijamii, alisema kuwa; kujenga upya ustaarabu mpya wa Kiislamu ndilo jambo linaloyatofautisha Mapinduzi ya Kiislamu na harakati nyingine zote, na ndilo lengo lake kuu.
Alisisitiza: "Tofauti ya Mapinduzi ya Kiislamu na harakati zote nyingine imo katika nukta hii muhimu, yaani kuujenga upya ustaarabu mpya wa Kiislamu."
Akibainisha kuwa haipaswi kuchanganya masuala ya muda mfupi na malengo ya msingi ya Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: "Suala kuu linalotukutanisha na madhalimu na wenye kiburi duniani si mjadala wa Mlango-Bahari wa Hormuz wala nishati ya nyuklia. Bali kuna suala jingine ambalo kambi ya ubeberu wa kimataifa haiwezi kuvumilia, nalo ni kuujenga upya ustaarabu wa dunia kwa misingi ya ustaarabu wa Kiislamu."
Ayatollah Arafi alieleza kuwa lengo hili linavuka tofauti za kisiasa na masuala ya kawaida yanayojadiliwa katika uwanja wa kimataifa, kisha akaongeza: "Kama suala lingekuwa ni mambo mengine tu, kungekuwa na uwezekano wa kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano. Lakini kuujenga upya ustaarabu na kubadilisha mfumo wa kiutendaji na mifumo ya kidhulma inayotawala dunia ni jambo ambalo kambi ya ubeberu wa kimataifa haiwezi kulikubali."
Kubadilisha Mifumo ya Dunia Ndiyo Kiini cha Makabiliano ya Mapinduzi ya Kiislamu na Mfumo wa Ubeberu
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akizungumzia kuundwa mifumo ya kimataifa baada ya vita vikubwa na kuimarishwa kwa mifumo inayotawala dunia, alisisitiza kuwa: "Kubadilisha mfumo wa kiutendaji na mifumo ya kidhulma iliyotawala dunia baada ya Vita vya Pili vya Dunia ndilo lililokuwa jambo kuu katika kilio na wito wa Imam Khomeini (q.s.) mwaka 1342 Hijria ya Shamsi. Jambo hili, katika mwendelezo wa njia ya Mapinduzi ya Kiislamu, liligeuka kuwa mojawapo ya malengo makuu ya kupambana na mfumo wa utawala wa kibeberu."
Akizungumzia mabadiliko na vita vya hivi karibuni, aliyataja matukio hayo kuwa na mchango katika kubadilisha mifumo ya kimataifa, na kusema: "Vita vya kujihami vilivyodumu miaka minane, Vita vya Pili vya Kulazimishwa na tukio la kishujaa la kujihami katika Vita vya Tatu vya Kulazimishwa, vyote vimekuwa na nafasi katika kuibua suala hili. Mabadiliko ya hivi karibuni yameonesha kwamba Mapinduzi ya Kiislamu, katika njia ya kubadilisha mfumo unaotawala dunia, yameleta uwezo na vipaji vya aina tofauti katika uwanja wa mapambano."
Mtu Mwenye Roho ya Basij Ana Ahadi Kubwa na Matarajio Madogo Kutoka kwa Mapinduzi
Ayatollah Arafi, akiendelea kufafanua sifa kuu za fikra za Basij, aliashiria kujitoa kwa kiwango cha juu na kuwa na matarajio madogo kuwa ni miongoni mwa sifa muhimu zaidi za roho hiyo.
Alisema: "Basij ni mfano wa kujitoa kwa kiwango cha juu na kutarajia machache kadiri iwezekanavyo. Mtu mwenye roho ya Basij ni yule anayejitoa kwa ajili ya Uislamu kutoka ndani kabisa ya moyo wake, ana kiwango cha juu cha kujitolea, lakini ana matarajio madogo kabisa kutoka kwa Mapinduzi."
Mjumbe wa Baraza la Mafiqihi la Baraza la Kulinda Katiba, huku akisisitiza kwamba roho hii inapaswa kujidhihirisha kwa kina na kwa namna inayolingana na majukumu ya Hawza na vyuo vikuu, aliongeza: "Roho ya Basij ndani ya Hawza na vyuo vikuu inapata maana mpya na pana zaidi. Maana yake ni kudhihirisha kiwango cha juu cha kujitolea, jihadi, Muqawama na kuwajibika katika kiwango cha juu zaidi."
Nyanja Saba za Nguvu Zinazohitajika kwa Ajili ya Ustaarabu Mpya wa Kiislamu
Ayatollah Arafi, akifafanua mahitaji ya kutimiza ustaarabu mpya wa Kiislamu, aliutaja uzalishaji wa nguvu katika nyanja mbalimbali kuwa ni miongoni mwa mahitaji ya msingi ya kujenga ustaarabu. Alisema: "Ikiwa tunataka kuwa na mtazamo kuhusu ustaarabu mpya katika dunia hii iliyojaa misukosuko, tunapaswa kufahamu kwamba ustaarabu unahitaji kuundwa kwa nguvu katika sehemu saba:
1. Nguvu za kijeshi na kiusalama;
2. Nguvu za kiuchumi;
3. Nguvu za kielimu;
4. Nguvu za kijamii;
5. Nguvu za kiutamaduni;
6. Nguvu za kisiasa;
7. Nguvu za kiteknolojia.
Nyanja zote hizi zinahitaji tabaka la chini na la msingi linalozijenga, ambalo ni nguvu za kimaarifa na kiitikadi."
Nafasi ya Msingi ya Maarifa na Fikra
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akisisitiza nafasi ya msingi ya maarifa na fikra katika kuunda nyanja nyingine za nguvu, alibainisha: "Nguvu za kimaarifa na kiitikadi ndizo msingi wa nguvu nyingine zote. Bila kuundwa kwa mfumo wa fikra na maarifa ulio na mshikamano na mpangilio madhubuti, haiwezekani kufikia maendeleo na kustawi kwa kudumu katika nyanja nyingine."
Wajibu wa Basij ya Hawza na Vyuo Vikuu ni Kushiriki Katika Uwanja wa Utendaji na Kuzalisha Elimu na Fikra
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akizungumzia umuhimu wa ushiriki hai wa Basij ya Hawza na vyuo vikuu katika nyanja za kijamii, wananchi na mapinduzi, alisisitiza: "Basij ya Hawza na vyuo vikuu inapaswa kuwa pamoja na wananchi, kushiriki katika uwanja wa utendaji na kuwa na nafasi ya kuleta mabadiliko. Hata hivyo, jukumu maalumu la makundi haya mawili ni kuzalisha maarifa ya kielimu na fikra katika nyanja za elimu, teknolojia, utamaduni na itikadi ya msingi ya Mapinduzi ya Kiislamu."
Ijtihadi Inayojenga Ustaarabu
Ayatollah Arafi, akisisitiza umuhimu wa kuleta mabadiliko katika mfumo wa kielimu wa Hawza, aliitaja ijtihadi inayojenga ustaarabu kuwa ni miongoni mwa mahitaji ya msingi ya siku zijazo.
Alisema: "Hawza na vyuo vikuu vinapaswa kutumia uwezo wao wa kielimu na wa wasomi ili kujibu mahitaji mapya ya jamii, kuzalisha fikra na kubuni mifumo ya kijamii inayolingana na misingi ya Kiislamu. Katika njia hii, haipaswi kupuuza umuhimu wa ushirikiano na kuunganisha nguvu kati ya taasisi hizi mbili."
Ayatollah Arafi, katika hitimisho la hotuba yake, akisisitiza umuhimu wa kuweka mipango kwa ajili ya vizazi vijavyo, alisema: "Ni lazima tuwe na mipango kwa ajili ya kizazi kijacho, na njia ya maendeleo, elimu, teknolojia na kutimiza ustaarabu mpya wa Kiislamu iendelee kupitia mikono ya vizazi vijavyo. Kwa hiyo, jukumu la Hawza, vyuo vikuu na Basij ya wasomi katika kuandaa kizazi chenye uwezo na kinachoweza kujenga ustaarabu ni jukumu la msingi na lenye umuhimu mkubwa katika kuamua mustakabali."
Maoni yako