Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hawza za wanawake za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimetoa tamko la kulaani ukandamizaji na kutolewa hukumu kali dhidi ya wanazuoni wa Kishia nchini Bahrain.
Yafuatayo ndiyo yaliyomo katika tamko hilo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
“Wala msiwaelekee wale waliodhulumu, la sivyo Moto utawagusa.”
(Surat Hud, aya ya 113).
Katika kipindi ambacho ulimwengu wa Kiislamu unahitaji zaidi ya wakati mwingine wowote umoja, mshikamano na kusimama imara dhidi ya upande wa dhuluma na ubeberu, kutolewa hukumu kali za kimahakama dhidi ya kundi la wanazuoni mashuhuri wa Bahrain, akiwemo Ayatullah Sheikh Isa Qassim na Sheikh Hussein al-Daihi, ni hatua inayotia wasiwasi na inayokwenda kinyume na misingi ya uadilifu, uhuru wa kidini na haki za msingi za mataifa. Mwelekeo huu unaweza kutazamwa kuwa sehemu ya sera za kutaka kutawala na kuingilia mambo ya wengine zinazofuatwa na madola ya kibeberu na mkondo wa Uzayuni wa kimataifa.
Hawza za wanawake za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku zikilaani hatua hiyo na kutangaza mshikamano wao na wanazuoni wanaodhulumiwa pamoja na wananchi Waislamu wa Bahrain, zinasisitiza kuwa; kuwatetea wanaodhulumiwa na kusimama dhidi ya dhuluma ni wajibu wa kidini na kibinadamu. Kama ambavyo Qur’ani Tukufu inavyosema:
“Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki.”
(Surat An-Nisaa, aya ya 135).
Misimamo ya wanazuoni wa Bahrain katika kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na watu wa Ghaza, kulaani jinai za utawala wa Kizayuni na kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni, ni mfano wa wazi wa kutekeleza wajibu huo wa kidini na kibinadamu.
Bila shaka, kuwaunga mkono wanaodhulumiwa na kupinga ukaliaji wa ardhi za wengine pamoja na uchokozi si kosa la jinai, bali ni dhihirisho la dhamiri iliyo hai ya Umma wa Kiislamu. Hakuna mamlaka yoyote inayoweza kuizima sauti ya wanazuoni wa dini wanaotetea haki kwa kutumia hukumu kali au shinikizo za kisiasa.
Kwa upande mwingine, uwepo wa kijeshi wa madola kutoka nje ya eneo hili, hususan Marekani, katika ardhi za Kiislamu, pamoja na nafasi ya kambi zao za kijeshi katika mipango ya kiusalama ya eneo hili, ni miongoni mwa masuala ya msingi yanayopingwa na wananchi wa eneo hili.
Wananchi wa Bahrain pia wana haki ya kuhoji uwepo wa Kikosi cha Tano cha Jeshi la Wanamaji la Marekani katika nchi yao, na kudai uhuru, uwazi na kulindwa kwa mamlaka ya kitaifa.
Hakuna nchi inayopaswa kuruhusu ardhi na rasilimali zake kutumiwa kwa ajili ya kufanya mashambulizi dhidi ya nchi nyingine, hususan nchi za Kiislamu. Hii ni kwa sababu usalama wa kudumu wa eneo hili unategemea uhuru wa mataifa na kukomeshwa kwa uingiliaji wa kibeberu wa wageni.
Katika mazingira haya, ukimya na misimamo ya pande mbili ya baadhi ya serikali za Kiarabu, madola ya Magharibi na taasisi za haki za binadamu kuhusu shinikizo za kisiasa na kimahakama dhidi ya wanazuoni wa Bahrain, vinaonesha tena mkanganyiko uliopo kati ya madai ya kutetea haki za binadamu na matendo ya wale wanaodai kutetea uhuru na demokrasia. Haiwezekani kudai kutetea haki za binadamu na uhuru wa imani, huku ukikaa kimya wakati haki hizo hizo zinapokiukwa katika nchi washirika wako.
Tunatarajia kuwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa zinazotetea haki za binadamu zitawajibika ipasavyo katika kulinda haki za wananchi wa Bahrain na kufuatilia hali za wanazuoni waliokamatwa.
Wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa Hawza za wanawake katika maeneo mbalimbali nchini Iran, huku wakitangaza upya mshikamano wao na wanazuoni wanaodhulumiwa pamoja na wananchi Waislamu wa Bahrain, wanataka hukumu zilizotolewa zipitiwe upya, uhakikishwe uwepo wa mchakato wa haki na huru wa utoaji haki, na zisitishwe hatua za kiusalama na kimahakama dhidi ya shughuli za kidini na kiraia zinazofanyika kwa njia ya amani.
Vilevile, wanataka kulindwa uhuru wa imani na kujieleza, kuzuiwa matumizi ya rasilimali na uwezo wa nchi za eneo hili katika kufanya mashambulizi dhidi ya nchi za Kiislamu, pamoja na kukabiliana na uingiliaji wa madola yanayotaka kutawala na kuyadhibiti mataifa mengine.
Mwisho, tunawakumbusha watawala wa Bahrain maneno yenye nuru ya Qur’ani Tukufu, ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
“Wala chuki ya watu fulani isiwapelekee kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu, kwani huo ndio ulio karibu zaidi na uchamungu.”
(Surat Al-Maaidah, aya ya 8).
Bila shaka, kuwaongezea dhuluma wanazuoni na viongozi wa dini wa Bahrain, kutoa hukumu zisizo za haki na kuwanyima uhuru wao, ni mambo yanayokinzana na mafundisho ya wazi ya Qur’ani Tukufu pamoja na mwenendo wa Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu (saww). Hatua hizo zitakuwa na dhima nzito mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Uadilifu ni kanuni ya Mwenyezi Mungu inayohusu watu wote, na hakuna tofauti yoyote ya kimadhehebu, kisiasa au kiitikadi inayoweza kuwa sababu ya kuhalalisha dhuluma na ukiukaji wa haki za binadamu.
Kwa msingi huo, tunatoa wito wa dhati wa kufutwa mara moja hukumu hizo za kidhalimu, kukomeshwa hatua za ukandamizaji na kuachiliwa huru wanazuoni na viongozi wa dini wa Bahrain wanaopambana na dhuluma na wanaodhulumiwa.
Bila shaka, heshima na usalama wa kudumu hupatikana kupitia uadilifu, uhuru na kukabiliana na utawala wa mabavu, si kwa vitisho, vifungo na kuzima sauti za wanaotetea haki.
Sauti ya wanazuoni wanaotetea haki haiwezi kunyamazishwa kwa hukumu za mahakama, na azma ya kusimamia uadilifu haiwezi kufungwa nyuma ya kuta za magereza.
Wassalaamu alaykum warahmatullahi wabarakaatuh.
Wanafunzi, walimu na uongozi wa Hawza za wanawake nchini Iran.
Maoni yako