Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ali al-Mousawi, mwalimu wa Hawza nchini Bahrain, katika mahojiano na mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, akizungumzia kuongezeka shinikizo dhidi ya wafuasi wa madhehebu ya Shia nchini Bahrain, alisema: "Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo wanakabiliwa na hali ngumu na wanaishi chini ya shinikizo kubwa. Hali imefikia hatua ambapo haki zao za msingi katika kuendesha maadhimisho na ibada za kidini, pamoja na kushiriki katika nyanja mbalimbali za kijamii, zinapuuzwa."
Akikosoa mwenendo wa serikali ya Bahrain katika kushughulikia madai ya kidini na kijamii ya wananchi, aliongeza: "Utawala wa Bahrain umechukua mwelekeo na njia isiyo sahihi. Mwelekeo huu si kwamba hausaidii kutatua matatizo yaliyopo pekee, bali pia unasababisha kuongezeka migogoro ya kisiasa na kijamii nchini humo. Aidha, umeathiri vibaya uhuru wa kutekeleza ibada na maadhimisho ya kidini ambayo yamekuwa yakifanyika kwa muda mrefu katika jamii ya Bahrain."
Kukamatwa wanazuoni na kubomolewa misikiti; sababu zilizochochea kutoridhika wananchi wa Bahrain
Mwalimu huyo wa Hawza nchini Bahrain, akizungumzia vikwazo vilivyowekwa dhidi ya shughuli za kidini nchini humo, alieleza: "Kukamatwa na kufungwa wanazuoni na wasomi wa dini, kubomolewa misikiti na Husainiya, kusimamishwa Swala ya Ijumaa na Swala za Jamaa, pamoja na kuzuiwa maadhimisho na shughuli mbalimbali za kidini, ni miongoni mwa hatua zinazotekelezwa na vyombo vya usalama vya Bahrain."
Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Mousawi aliendelea kusema: "Hatua hizi zimesababisha kuongezeka kutoridhika na huzuni miongoni mwa wananchi, kwa sababu wananchi wa Bahrain wanatarajia kuwa na uwezo wa kutekeleza ibada na shughuli zao za kidini kwa uhuru na kufurahia haki zao za kidini na kijamii. Hata hivyo, kwa masikitiko, haki hizi zimekabiliwa na vikwazo vikubwa."
Akisisitiza umuhimu wa kusitishwa ukiukwaji dhidi ya uhuru wa kidini, alibainisha: "Kumaliza mgogoro huu kunahitaji kusitishwa kila aina ya ukiukwaji dhidi ya uhuru wa kidini, kuzingatiwa wajibu na mikataba ya kimataifa inayohusu haki za binadamu na haki za uraia, pamoja na kufutwa ubaguzi miongoni mwa wananchi wa Bahrain."
Kuweka vikwazo dhidi ya uhuru wa kidini ni ukiukwaji wa Kifungu cha 18 cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa
Mwalimu huyo wa Hawza nchini Bahrain, akizungumzia Kifungu cha 18 cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, alisema: "Uhuru wa dini na madhehebu, pamoja na haki ya watu kueleza imani zao na kutekeleza ibada na maadhimisho yao ya kidini, ni miongoni mwa haki zinazotambuliwa katika nyaraka za kimataifa. Kwa msingi huo, kila aina ya ukiukwaji dhidi ya uhuru wa kidini inapaswa kusitishwa."
Aliongeza: "Kusisitiza utawala wa Bahrain kuendelea kuweka vikwazo dhidi ya uhuru wa kidini na kuendeleza sera za kibaguzi kunamaanisha ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu na uhuru wa kutekeleza ibada za kidini. Hatua hizi, mbali na kuharibu taswira ya Bahrain katika medani ya kimataifa, zinaweza pia kudhoofisha mshikamano wa kijamii na kusababisha kuvunjika mshikamano wa kitaifa nchini humo."
Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Mousawi alisisitiza: "Hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha hatua, matamshi na sera zinazoipeleka nchi katika mwelekeo wa migogoro, tofauti na mifarakano. Hatua za aina hiyo ni ukiukwaji wa haki za uraia, kudhalilisha heshima ya ibada za kidini na kukiuka waziwazi sheria na haki za wananchi."
Kulaani hukumu za kifo na vifungo dhidi ya wanazuoni na wasomi wa dini nchini Bahrain
Mwalimu huyo wa Hawza nchini Bahrain, huku akilaani hukumu kali zilizotolewa dhidi ya baadhi ya wanazuoni na wasomi wa dini nchini humo, alisema: "Leo tunashuhudia kutolewa hukumu za kifo, vifungo vya maisha na adhabu za vifungo vya muda mrefu dhidi ya kundi la wanazuoni na viongozi wa dini nchini Bahrain. Tunazilaani vikali hukumu hizi."
Alizitaja hukumu hizo kuwa ni za kidhalimu na hatua za kulipiza kisasi dhidi ya wanazuoni na Hawza za kielimu, kisha akaongeza: "Inaonekana kuwa msimamo wa wanazuoni na wananchi wa Bahrain dhidi ya sera za utawala wa Al Khalifa, kukosoa utendaji wa serikali na kudai kuondoka kwa vikosi vya Marekani nchini humo, ni miongoni mwa sababu zilizosababisha kutolewa hukumu za aina hii dhidi ya baadhi ya viongozi wa dini."
Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Mousawi, huku akisisitiza kuwa wanazuoni na wasomi wa dini wamekuwa daima pamoja na wananchi na madai yao, alisema: "Hatua za kimahakama na kiusalama dhidi ya viongozi wa dini, pamoja na kutolewa hukumu kali dhidi yao, haziwezi kufuta madai halali ya wananchi. Badala yake, hatua hizo zinaongeza kiwango cha kutoridhika wananchi na kuzidisha matatizo yaliyopo."
Kuondoka vikosi vya Marekani na Saudi Arabia na kuachiliwa wanazuoni waliofungwa; Madai mawili muhimu ya wananchi wa Bahrain
Akiendelea kuzungumzia madai ya wananchi wa Bahrain kuhusu uwepo wa vikosi vya kigeni nchini humo, alisema: "Leo wananchi wa Bahrain wanataka vikosi vya Marekani na Saudi Arabia viondoke mara moja katika ardhi ya nchi yao. Wananchi wanaendelea kudai jambo hili sambamba na madai yao mengine ya msingi."
Mwalimu huyo wa Hawza nchini Bahrain, akifafanua madai mengine ya wananchi wa nchi hiyo, alibainisha: "Kuachiliwa wanazuoni waliofungwa, kukomeshwa vitendo vya ubaguzi dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, kuheshimiwa haki za kidini za wananchi na kuwekwa kwa mazingira yatakayowawezesha kuendesha uhuru maadhimisho na ibada zao za kidini, ni miongoni mwa madai muhimu zaidi ya wananchi wa Bahrain."
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ali al-Mousawi, akihitimisha mahojiano yake, alisisitiza: "Kuheshimiwa haki za wananchi wote, kuhakikishwa uhuru wa kidini, kusitishwa hatua za kiusalama dhidi ya wanazuoni na wasomi wa dini, pamoja na kukomeshwa ubaguzi wa kidini, ni mambo ya lazima. Utekelezaji wa mambo haya unaweza kuweka mazingira ya kupunguza mvutano, kuimarisha umoja wa kitaifa na kuleta utulivu nchini Bahrain."
Maoni yako