Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya SShirika la Habari la Hawza, Ayatullah Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, amesafiri nchini Bosnia na Herzegovina kwa mwaliko rasmi wa Sheikh Nedžad Grabus, Rais mpya wa Wanazuoni wa nchi hiyo, ili kushiriki katika hafla ya kuthibitishwa rasmi katika nafasi hiyo.
Katika mkutano huo, ambao hufanyika mara moja kila baada ya miaka saba na kuchukuliwa kuwa tukio muhimu zaidi la kidini nchini Bosnia na Herzegovina, hushiriki viongozi wa ngazi za juu za kisiasa, kiutamaduni na kidini wa nchi hiyo, kuanzia Rais wa nchi, Spika wa Bunge na viongozi wengine mashuhuri, sambamba na viongozi wa kidini kutoka mataifa mbalimbali ya dunia. Katika hafla hiyo, Rais mpya wa Wanazuoni aliyechaguliwa wa Jumuiya ya Kiislamu ya Bosnia na Herzegovina huthibitishwa rasmi katika nafasi yake.
Katika hafla hiyo, Sheikh Nedžad Grabus alitambulishwa rasmi kuwa Rais mpya wa Wanazuoni wa Bosnia na Herzegovina. Kabla ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo, alikuwa Mufti wa zamani wa Slovenia na Mufti wa zamani wa mji mkuu wa Bosnia na Herzegovina, Sarajevo. Aidha, juhudi na huduma za Sheikh Husein Kavazović, Reisu-l-ulema aliyemaliza muda wake, zilitambuliwa na kupongezwa.
Sheikh Nedžad Grabus ni mhitimu wa Shahada ya Uzamivu katika Elimu za Kiislamu kutoka Kitivo cha Elimu za Kiislamu cha Sarajevo, na pia amepata elimu katika fani ya falsafa ya Kiislamu. Amehudhuria programu mbalimbali za masomo katika nchi za Misri, Norway na Saudi Arabia.
Vilevile, yeye ni mjumbe wa Baraza la Uongozi wa Kidini la Ulaya, Makamu wa Shirika la Kimataifa la Dini kwa Ajili ya Amani lenye makao yake nchini Marekani, na Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Viongozi wa Dini mbalimbali lenye makao yake mjini Vienna, Austria.
Grabus alichaguliwa kushika nafasi hiyo katika uchaguzi wa Jumuiya ya Kiislamu uliofanyika mwezi wa Mehr 1405, baada ya kupata kura nyingi zaidi. Alianza rasmi kutekeleza majukumu yake kupitia hafla maalumu iliyojulikana kama “Hafla ya Kukabidhi Hati Rasmi ya Uteuzi”, ambayo ina historia ndefu tangu kipindi cha utawala wa Dola ya Ottoman.
Bosnia na Herzegovina, ikiwa ni nchi yenye Waislamu wengi katika eneo la Balkan na barani Ulaya, ni miongoni mwa maeneo muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya nchi hiyo kupata uhuru kufuatia kuvunjika kwa iliyokuwa Yugoslavia na kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwanzoni mwa miaka ya 1990, ilipata umuhimu wa pekee katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Misaada ya kibinadamu iliyotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuchangia usalama wa Bosnia na Herzegovina na ustawi wa maisha ya wananchi wake imekuwa ikitambuliwa na kusifiwa mara kwa mara na viongozi pamoja na wananchi wa Bosnia.
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran alishiriki katika hafla hiyo iliyofanyika katika Msikiti wa Gazi Husrev-beg, ambako alimpongeza Reisu-l-ulema mpya wa Bosnia na Herzegovina na kumtakia mafanikio katika majukumu yake mapya. Baadaye, alikutana na viongozi mbalimbali wa kidini kutoka Bosnia na Herzegovina pamoja na viongozi wa kidini wa kimataifa.
Maoni yako