Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Hashim Husseini Bushehri, katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa mjini Qom, zilizotolewa katika Musalla Quds tarehe 15 Aban 1405 (6 Novemba 2026), amesema: Hongereni wananchi kwa kusimama kwenu pamoja na Mapinduzi, marafiki na maadui wanawafuatilia na kuwachunguza katika medani zote.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Qom, huku akizungumzia maadhimisho ya tarehe 13 Aban, amesema: Katika maandamano ya tarehe 13 Aban mlijitokeza kwa namna nzuri sana. Mmevumilia na kufanya Muqawama kwa muda wa miezi nane, na mmeendelea kusimama imara katika kuyaunga mkono Mapinduzi, Kiongozi Shahidi na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameendelea kusema: Katika siku ya tarehe 13 Aban, kutokana na Muqawama wenu, dalili za kushindwa adui zilidhihirika waziwazi, kiasi kwamba wao wenyewe walikiri kuwa kama kusingekuwa na vita dhidi ya Iran, Trump asingeshindwa kwa mfululizo na kwa kiwango kikubwa kama tsunami. Leo hii wameanza kutafutana na kutaka kumtoa kafara mmoja wao, huku kila mmoja akitafuta kujua ni nani aliyesababisha kushindwa kwao huko.
Khatibu huyo wa Swala ya Ijumaa mjini Qom amebainisha kuwa; baada ya tukio la Ashura, wakati Ahlul-Bayt (a.s) walipopelekwa Sham wakiwa mateka, Imam Sajjad (a.s) alisema: Mtambue muuaji wa baba yangu. Shimr, Khuli na Sinan walisema kuwa; hawakuwa wao waliomuua, hapo Shimr alimwelekea Yazid na kumwambia kuwa mhusika mkuu alikuwa ni wewe mwenyewe. Kama usingewachochea watu kupigana vita kwa kutumia fedha za Baytul-Mal, tukio hili lisingetokea. Akizungumza na Trump, amesema: Wewe mwenyewe ndiye mwenye hatia ya kushindwa leo, Waziri wako wa Vita anafuata maagizo yako na hawezi kutekeleza jambo lolote kinyume na amri zako.
Imam wa Swala ya Ijumaa mjini Qom, akieleza kuwa kwa sasa ushindi mkubwa wamepata wananchi wa Iran, amesema: Kwa mujibu wa kauli ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, mabadiliko ya serikali nchini Marekani hayana athari yoyote kwetu, kwa sababu zote zinafanana na tumepata madhara kutoka kwa pande zote mbili. Kwa hiyo, Democrats wasidhani kwamba wao ndio walioshinda, bali wananchi wa Iran ndio waliopata ushindi dhidi ya serikali ya Marekani na Trump.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Elimu ya Qom ameongeza kuwa; adui alikuwa hajawafahamu Mashia, Iran na wapiganaji wetu, walitaka kutujaribu lakini leo wamefanya jaribio hilo na kujionea wenyewe matokeo yake.
Amesema: Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi amesema kuwa; sisi hatutambui mipaka ya kijiografia, kauli hii ni hatua moja mbele zaidi ya dhana ya vita vya kikanda ambayo Kiongozi Shahidi aliizungumzia. Vita vya kikanda ambavyo Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi alivitaja vilikuwa ni msingi wa hatua ambayo leo tunasema kwamba hakuna tena suala la mipaka ya kijiografia, na kwamba kutoka katika eneo lolote lile ambako hatua dhidi ya Iran itachukuliwa, tutajibu mashambulizi hayo.
Ayatullah Husseini Bushehri amekumbusha kwa kusema: Ninawashauri muusome mara kwa mara ujumbe wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, katika ujumbe huo, Kiongozi amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa ndani ya nchi, amewakumbusha viongozi kuhusu wajibu wao wa kuhudumia wananchi katika masuala ya maisha na mahitaji yao ya kila siku, na pia amesisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na viongozi wao.
Ameeleza kuwa; kwa kuzingatia masharti saba yaliyotajwa na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa katika mkutano wake na Rais wa Urusi, tuko tayari kuchukua hatua zinazohitajika. Masharti hayo saba ni kama ifuatavyo:
1. Kusitishwa vita na uvamizi wa kijeshi.
2. Kuondolewa vikwazo.
3. Kurejeshwa mali za Iran zilizozuiliwa.
4. Kulipwa fidia ya hasara zilizosababishwa.
5. Kusitishwa vitisho.
6. Kuondolewa vikosi vya kijeshi vya Marekani katika eneo hili.
7. Kuondolewa vikwazo vilivyowekwa katika usafiri wa majini.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom amekumbusha kuwa, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, adui atalazimika kusalimu amri mbele ya Iran.
Aidha, akitoa salamu za rambirambi katika siku za maombolezo ya Fatimiyya, amesema: Enyi madhehebu na waimbaji wa tenzi za maombolezo, wahadhiri na wengineo, tambueni kwamba kila tulichonacho tumekipata kutokana na Ahlul-Bayt (a.s) na msimamo wa Muqawama wa Bibi Fatimah Zahraa (s.a), tunapata msukumo kutoka kwao na kupitia mfano wao tunavumilia magumu. Hakikisheni kwamba shughuli hizi za maombolezo zinaendelea kuwa na uchangamfu na hamasa kubwa, sambamba na uwepo wa wananchi mitaani.
Hotuba ya kwanza
Ayatullah Husseini Bushehri, katika hotuba yake ya kwanza, amesema: Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Aya ya 201 ya Suratul-A'raf:
«إِنَّ الَّذِینَ اتَّقَوْا إِذَا مَسَّهُمْ طَائِفٌ مِنَ الشَّیْطَانِ تَذَکَّرُوا فَإِذَا هُمْ مُبْصِرُونَ»
“Hakika wale wanaomcha Mwenyezi Mungu, wanapopatwa na vishawishi kutoka kwa Shetani [vinavyowavuta katika madhambi, maasi na uchafu wa nje na wa ndani], humkumbuka Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama, na mara moja huwa na utambuzi [na hivyo kuokoka katika mtego wa vishawishi vyake].”
Ameendelea kusema: Katika zama hizi tunakabiliwa na mashambulizi mengi kutoka kwa maadui, na ili kukabiliana nao tunapaswa kutumia mwenendo wa maisha ya Mtume (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt (a.s) katika namna walivyokabiliana na maadui zao.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Qom, huku akizungumzia mwenendo wa Mtume (s.a.w.w) katika kukabiliana na maadui amesema kuwa; kuondoa ushirikina, kusimamisha uadilifu, kuonya, kuvunja nguvu na mamlaka ya adui, pamoja na kujenga heshima na hadhi ya jamii, ni miongoni mwa misingi aliyokuwa nayo Mtume (s.a.w.w).
Akizungumzia msingi wa kuondoa ushirikina, amesema: Katika hatua yake ya kwanza, Mtume (s.a.w.w) alilenga kuondoa ushirikina katika jamii na kueneza mafundisho ya Tauhidi. Hii ni kwa sababu jamii inapokuwa na imani sahihi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, haitapambana na Mtume (s.a.w.w) wala mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s), kwani ni washirikina pekee wanaosimama dhidi ya Mtume (s.a.w.w) na mafundisho ya Tauhidi.
Imam wa Swala ya Ijumaa mjini Qom, akirejea Aya ya 25 ya Suratul-Anbiya, amesema:
«مَا أَرْسَلْنَا مِنْ قَبْلِکَ مِنْ رَسُولٍ إِلَّا نُوحِی إِلَیْهِ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ»
“Hatumtumi Mtume yeyote kabla yako isipokuwa tulimshushia wahyi kwamba: Hakuna Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mimi, basi niabuduni Mimi pekee.”
Ameongeza kuwa ujumbe mkuu wa Mtume wa Uislamu (s.a.w.w) pamoja na Mitume wengine ulikuwa ni kupambana na ushirikina, ili kuubadilisha mazingira yasiyo na Tauhidi na yaliyochafuliwa na ushirikina kuwa mazingira safi na mema.
Amebainisha kuwa kwa mujibu wa Aya za Qur'ani, Mtume (s.a.w.w) alikuwa akijitahidi kueneza Tauhidi katika ibada ndani ya jamii, ili wanadamu wakue wakiwa ni wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu mwanadamu mwenye imani ya Tauhidi hufanya mambo kwa uaminifu na huwa amepambika kwa maadili mema.
Imam wa Swala ya Ijumaa mjini Qom, akibainisha kuwa Mwenyezi Mungu amesisitiza ibada na kumpwekesha katika Aya nyingi za Qur'ani, ameongeza kuwa; mazingira yanapaswa kusafishwa ili jamii yenye Tauhidi iweze kuishi na kupumua katika mazingira safi, na ili watu kama Ammar na wengineo wasipate madhara. Kwanza, jamii inapaswa kusafishwa kutokana na maovu na mambo yaliyokatazwa, kisha mambo mema na yanayopaswa kufanywa yawekwe badala yake.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Qom amesema kuwa Imam Ali (a.s) anasema:
«فَبَعَثَ اللَّهُ مُحَمَّداً (صلی الله علیه وآله) بِالْحَقِّ لِیُخْرِجَ عِبَادَهُ مِنْ عِبَادَةِ الْأَوْثَانِ إِلَی عِبَادَتِهِ وَ مِنْ طَاعَةِ الشَّیْطَانِ إِلَی طَاعَتِهِ، بِقُرْآنٍ قَدْ بَیَّنَهُ»
“Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad (s.a.w.w) kwa haki, ili awatoe waja wake katika ibada ya masanamu na kuwaingiza katika ibada Yake, na awatoe katika kumtii Shetani na kuwaingiza katika kumtii Yeye, kupitia Qur'ani ambayo ameibainisha na kuweka wazi maana zake.”
Ameeleza kuwa Mtukufu Muhammad (s.a.w.w) hakulenga tu kumshinda adui ili siku nyingine adui huyo aweze kurejea tena na kuanzisha mapambano, bali Mtume (s.a.w.w) alilenga kutatua tatizo kuanzia kwenye mizizi yake, kwa kurekebisha misingi ya fikra na itikadi ya jamii.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom amesisitiza kuwa; iwapo mtu ataongozwa katika njia sahihi, hatasimama tena kupambana na haki. Lakini iwapo imani na itikadi ya mtu au jamii haitarekebishwa kuanzia kwenye mizizi yake, basi siku nyingine atarejea tena katika mapambano.
Maoni yako