Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Hussein al-Matouq, katika hafla ya kumuenzi iliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Idara Kuu ya Uenezi wa Kiislamu ya Mkoa wa Qum Iran, akizungumzia mafanikio ya Muqawama katika eneo hili, alisema: Kutokana na ushindi wa mfululizo wa Muqawama, na licha ya kujitolea na kujitoa mhanga kwa kiwango kikubwa kulikofanyika katika njia hii, leo Muqawama uko katika nafasi ya maendeleo na nguvu kubwa.
Akizungumzia mabadiliko ya kihistoria na nafasi ya sasa ya Mashia nchini Lebanon, aliongeza: Tukitazama hali ya zamani na nafasi ya wananchi katika mabadiliko ya eneo hili, tutabaini tofauti kubwa sana ikilinganishwa na hali ya leo. Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa akilizungumzia mara nyingi suala hili kwamba; katika kipindi cha Mkataba wa Sykes-Picot, Mashia wa Lebanon hawakuwa na nafasi wala utambulisho muhimu wa kijamii na kisiasa, na hawakupewa nafasi yoyote katika mizania ya kikanda. Hata hivyo, leo Mashia hao hao wanasimama dhidi ya utawala wa Kizayuni na wamegeuka kuwa miongoni mwa wadau wenye ushawishi katika mabadiliko ya eneo hili.
Sheikh Hussein al-Matouq, akisisitiza upana wa mafanikio ya Muqawama katika eneo hili, alieleza: Mafanikio ya Muqawama nchini Lebanon, Palestina, Iraq na Yemen, na juu ya mafanikio hayo yote, maendeleo na ushindi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, leo yamejitokeza na kudhihirika zaidi kuliko hapo awali. Mabadiliko haya yanaonesha kwamba harakati ya Muqawama imefanikiwa kuathiri mizania ya eneo hili na kuinua nafasi ya mataifa ya Kiislamu.
Maadui wa Uislamu wana wasiwasi kuhusu kuamka na kupata nguvu kwa Umma wa Kiislamu
Akizungumzia kujipanga maadui dhidi ya Umma wa Kiislamu, alibainisha: Leo, maadui wa Umma wa Kiislamu wamekusanyika pamoja kwa kutumia nguvu, vifaa na uwezo wao wote ili kuiondoa harakati hii; kwa sababu wamechoshwa na kuamka, kupata uelewa na kuimarika kwa nguvu Mashia na Umma wa Kiislamu, na hawawezi kuvumilia nguvu na ushawishi wa harakati hii.
Mwanazuoni huyu wa Hawza, akizungumzia mabadiliko yaliyotokea nchini Yemen, alisema: Ikiwa miaka michache iliyopita mtu angesema kuhusu nguvu na uwezo wa Muqawama nchini Yemen, huenda watu wengi wasingeamini kwamba uwezo wa aina hiyo ungeweza kujitokeza katika nchi hiyo. Hata hivyo, leo wananchi wa Yemen wapo katika medani wakiwa na izza, heshima na nguvu, na wamefanikiwa kuimarisha nafasi yao katika mizania ya kikanda.
Akielezea kwamba kuendelezwa mafanikio ya Muqawama kunahitaji umoja na mshikamano, alisema: Leo tunahitaji umoja zaidi kuliko wakati mwingine wowote, Ushindi ambao umepatikana hadi sasa usingewezekana bila ya kujitolea, kutjioa mhanga, kuwa na msimamo thabiti na kuvumilia matatizo. Hivyo, ili kuendelea na njia hii, tunapaswa kudumisha moyo huo huo wa kujitolea.
Kuuawa kishahidi kwa Imam Khamenei kumeufanya Umma kuwa imara zaidi
Sheikh Hussein al-Matouq, akizungumzia shakhsia na nafasi ya Imam Khamenei Shahidi, alisema: Imam Khamenei Shahidi alikuwa mwendelezo wa njia ya babu yao mtukufu, Mtukufu Sayyid al-Shuhadaa Imam Hussein (as). Mtu ambaye hataifahamu ipasavyo shakhsia ya Imam Hussein (as), Maimamu Watoharifu (as) na Imam wa Zama (aj), hataweza kunufaika kikamilifu na baraka na maarifa yote ya madhehebu haya.
Akizungumzia athari na matokeo ya kuuawa kishahidi kwa Imam Khamenei, aliongeza: Baada ya kuuawa shahidi Imam Khamenei, tulishuhudia namna Umma wa Kiislamu ulivyokuwa na nguvu zaidi, mshikamano mkubwa zaidi na msimamo thabiti zaidi. Tukio hili lilionesha kwamba yeye alikuwa amefanikiwa kuulea Umma, kuliongoza taifa na kuwalea viongozi ambao leo wamebeba jukumu la kuiendeleza njia hii.
Mwanazuoni huyu wa Hawza, akisisitiza nafasi ya malezi na uongozi ya Imam Khamenei Shahidi, alibainisha: Viongozi waliolelewa katika madrasa yake wataendeleza njia na malengo yake. Miongoni mwa viongozi hao ni Imam Sayyid Mujtaba Khamenei, ambaye ataendeleza njia hii.
Njia ya Muqawama haisimami kwa kuuawa kishahidi viongozi
Sheikh Hussein al-Matouq, akizungumzia kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na kuendelea njia ya Hizbullah ya Lebanon, alisema: Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah ametutoka, lakini Ayatullah Naim Qassem anaendeleza njia na mwelekeo uleule ambao Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa ameuchora, ukweli huu unaonesha kwamba njia ya Muqawama haifungamani na mtu mmoja pekee, na haisimami hata kwa kuuawa kishahidi shakhsia na viongozi.
Aliendelea kusema: Viongozi wa Muqawama wamefanikiwa kulea vikosi na shakhsia ambazo, kwa kuifahamu misingi ya malengo na madhumuni ya harakati hii, wanaweza kubeba jukumu la kuendeleza njia yake. Kwa hiyo, kuuawa kishahidi kwa kiongozi hakumaanishi mwisho wa njia, bali harakati ya Muqawama itaendelea na safari yake kwa kutegemea nguvu zilizolelewa na kushikamana na malengo yake.
Kukosoa misimamo ya baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu dhidi ya Muqawama
Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Matouq, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akikosoa utendaji wa baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu kuhusiana na mabadiliko ya eneo hili, alisema: Yale ambayo baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu wanayafanya leo, kwa hakika ni mwitikio wao dhidi ya ushindi wa Muqawama katika maeneo mbalimbali ya dunia. Badala ya kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa na kutetea haki za Umma wa Kiislamu, wao wanapanua uhusiano wao na Marekani na kuingia katika mahusiano na makubaliano ya kibiashara na nchi hiyo.
Akikosoa kuhusu mwelekeo wa baadhi ya serikali za eneo hili kuhusiana na utawala wa Kizayuni, aliongeza: Kwa masikitiko, baadhi ya watawala wa nchi za Kiislamu, badala ya kusimama pamoja na wananchi wanaodhulumiwa, wanachukua njia ambayo matokeo yake ni kuimarisha nafasi ya maadui wa Umma wa Kiislamu.
Kukosoa hatua za kimahakama nchini Kuwait dhidi ya wanaowaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa
Mwanazuoni huyu wa Hawza, akizungumzia hali iliyopo nchini Kuwait na namna baadhi ya watu wanavyokabiliwa na hatua za kisheria kwa sababu ya misimamo yao ya kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa, alisema: Kwa masikitiko, nchini Kuwait kuna watu wanaokabiliwa na hukumu na adhabu za kidhalimu kwa kisingizio cha kuwatetea wanaodhulumiwa na kuunga mkono ukweli.
Akikosoa mfumo wa mahakama na kisiasa wa baadhi ya nchi za eneo hili, alieleza: Kwa masikitiko, katika baadhi ya nchi hizi, hakuna kile kinachojulikana kwa maana halisi kuwa ni mfumo huru wa mahakama na mgawanyo wa mihimili ya dola. Katika mazingira kama hayo, hakuna uhuru halisi wa mhimili wa kutunga sheria, wala mhimili wa mahakama hauwezi kutekeleza majukumu yake kwa uhuru; bali mamlaka yote yamekusanywa katika kundi moja.
Sheikh Hussein al-Matouq, akifananisha hali ya mfumo wa mahakama katika nchi hizi na kutokuwepo kwa uhuru wa hakimu, alibainisha: Katika mfumo wa aina hii, badala ya hakimu kutoa hukumu kwa mujibu wa uadilifu na sheria, anageuzwa kuwa chombo cha kutekeleza matakwa ya wenye mamlaka. Mtawala anapotaka kulipiza kisasi dhidi ya mtu au harakati fulani, hutoa amri, na hukumu ya mahakama hutolewa kwa mujibu wa matakwa na matamanio yake. Huu ndio ukweli ambao, kwa masikitiko, unapatikana katika baadhi ya nchi zetu.
Mustakabali ni wa mataifa yenye msimamo thabiti na yaliyoamka
Akieleza matumaini na uhakika wake kuhusu mustakabali wa Muqawama, alisema: Licha ya shinikizo zote, vikwazo na uhasama, tuna uhakika kwamba tupo katika hatua nyeti na kubwa sana ya historia; hatua ambayo ndani yake tutashuhudia ushindi na maendeleo zaidi.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin al-Matouq, akizungumzia nafasi ya kihistoria ya Imam Khomeini (ra) katika kuyaamsha mataifa ya Kiislamu, alisema: Wakati Imam Khomeini (ra) alipoanzisha harakati yake, aliwafungulia wananchi upeo mpana. Aliwaokoa watu kutoka katika ujinga na kutofahamu ukweli; hususan aina ile ya ujinga inayomfanya mwanadamu ajisalimishe mbele ya madhalimu, akubali dhuluma na kutoa visingizio vya kuhalalisha uvamizi na uonevu.
Aliongeza: Imam Khomeini (ra) aliyaalika mataifa katika izza, heshima na uhuru, na akayalea katika njia hiyo hiyo. Ujumbe wa Imam ulikuwa kwamba Waislamu hawapaswi kujisalimisha mbele ya dhuluma na uvamizi, wala hawapaswi kuruhusu madola yenye kutaka kutawala wengine yaamue matakwa na hatima yao.
Madrasa ya Maimamu wawili wa Mapinduzi ni madrasa ya izza na heshima
Mwanazuoni huyu wa Hawza ya Kielimu, akizungumzia nafasi ya Imam Khamenei Shahidi katika kuendeleza njia ya Imam Khomeini (ra), alisema: Imam na kiongozi wetu, Shahidi Imam Sayyid Ali Khamenei (ra), pia alitufundisha izza na heshima, na akayalingania mataifa kusimama imara dhidi ya dhuluma na utawala wa mabavu.
Akisisitiza kwamba mataifa ya Kiislamu hayatarudi nyuma mbele ya shinikizo, alisema: Wananchi wetu hawatadhalilika wala hawatarudi nyuma; bali, Mwenyezi Mungu akipenda, kwa kutegemea imani, uelewa, umoja na Muqawama, wataendelea na njia ya maendeleo, ushindi na saada.
Sheikh Hussein al-Matouq, mwishoni akisisitiza kuendelea malengo ya Muqawama, alibainisha: Mataifa yenye msimamo thabiti, kwa kupata msukumo kutoka katika madrasa ya Imam Khomeini (ra), Imam Khamenei Shahidi na utamaduni wa Ashura, yataendelea kufuata njia ya izza na heshima mpaka siku tutakaposhuhudia kuangamizwa utawala wa Kizayuni.
Maoni yako