Jumamosi 24 Oktoba 2026 - 15:38
Chama cha Mrengo wa Kushoto cha Ufaransa, Chaonya Kuhusu Athari za Kupiga Marufuku Maandamano; Hatari ya Kuongezeka Mapigano Barabarani

Hawza/ Chama cha France Insoumise cha Ufaransa kimekosoa marufuku ya mikusanyiko na kanuni za kutotoka nje zilizowekwa katika miji kadhaa, kikiishutumu serikali kwa kuimarisha mwelekeo wa kimabavu. Chama hicho kimetoa wito wa kufanyika maandamano ya amani kote nchini, kuungwa mkono vyama vya wafanyakazi na kufutwa maamuzi yanayoweka vikwazo.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, chama cha mrengo wa kushoto cha Ufaransa, France Insoumise, kimepinga vikwazo vilivyowekwa baada ya matukio ya vurugu ya Oktoba 17. Chama hicho kimeonya kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na kupiga marufuku maandamano, huku kikisisitiza umuhimu wa kutetea uhuru wa umma.

Siku ya Ijumaa, Oktoba 23, chama cha mrengo wa kushoto cha France Insoumise (LFI) kililaani marufuku ya kufanya maandamano pamoja na kanuni za kutotoka nje zilizowekwa nchini Ufaransa. Chama hicho kimeishutumu serikali kwa kuendeleza sera ya kile ilichokiita “kuharakisha mwelekeo wa kimabavu”, na kutoa wito wa wananchi kushiriki katika uhamasishaji wa amani kwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma na vyama vya wafanyakazi.

Katika taarifa yake, chama hicho kilisema: “Uhuru wa umma hauwezi kugeuzwa kuwa kigezo cha kurekebisha sera za serikali ambayo inazidi kupoteza udhibiti wa hali.” Chama hicho cha mrengo wa kushoto pia kilikumbusha kwamba kuhakikisha uhuru wa umma unalindwa ni “jukumu la kwanza la serikali ya jamhuri”.

France Insoumise kilikosoa marufuku ya mikusanyiko, vikwazo vilivyowekwa dhidi ya waandaaji wa mikusanyiko hiyo, pamoja na kutungwa kanuni za kutotoka nje katika ngazi ya miji au maeneo ya kiutawala. Vilevile, chama hicho kilipinga kuhamasishwa wafanyabiashara na wamiliki wa maduka kutumia huduma za kampuni binafsi zinazotoa ulinzi na usalama.

Kwa mtazamo wa chama hicho, kwa kuchukua maamuzi hayo, serikali “inavuka moja baada ya jingine mipaka inayotenganisha demokrasia na serikali ya kimabavu inayotegemea nguvu za polisi”.

Chama hicho pia kilitilia shaka ufanisi wa hatua hizo, kikieleza kuwa marufuku ya maandamano ni “maamuzi ya kipumbavu yanayoweza kusababisha machafuko”. Kwa mujibu wa chama hicho, maamuzi kama hayo hayawezi kuondoa hasira za wananchi dhidi ya sera za serikali wala kupunguza hamu yao ya kuonesha maandamano yao barabarani; badala yake, yanaweza kusababisha mapigano na vurugu.

Kwa mujibu wa France Insoumise, kutokana na vikwazo hivyo, polisi wanaotumia nguvu kukandamiza maandamano wanaweza kujikuta wakilazimika kukabiliana na mikusanyiko iliyotawanyika na isiyotabirika, badala ya kusimamia maandamano yenye njia maalumu na waandaaji waliotambulishwa mapema.

Taarifa ya chama hicho iliendelea kusema: “Ni nguvu ya pamoja na idadi kubwa ya washiriki vinavyoweza kuishinda mikakati hii ya kuchochea mvutano na kufanya hali iendelee kuwa ngumu kwa muda mrefu.”

France Insoumise kimewataka wananchi kote nchini Ufaransa kushiriki katika maandamano ya amani kwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wanafunzi wa vyuo vikuu na wanafunzi wa shule, pamoja na kushiriki katika kulinda maandamano yanayofanyika kwa pamoja na kwa uratibu.

Chama hicho pia kimeunga mkono hatua za kisheria zinazochukuliwa na vyama vya kiraia na vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kufuta maamuzi ambayo kinayaeleza kuwa “ya kiholela na yasiyokubalika”. Mwishoni, chama hicho kimeitaka serikali kujibu madai ya wafanyakazi na vijana.

Msimamo huo umetolewa baada ya kutokea vurugu na uporaji siku ya Jumamosi, Oktoba 17, pembezoni mwa maandamano yaliyofanyika katika miji kadhaa ya Ufaransa kupinga kupanda bei na kuongezeka gharama za maisha.

Wakati wa matukio hayo, baadhi ya maduka na majengo ya umma yalishambuliwa. Jengo la halmashauri ya jiji la Limoges lilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyoharibiwa sa kutokana na moto.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotangazwa Alhamisi, Oktoba 22, na Gérald Darmanin, Waziri wa Sheria wa Ufaransa, watu 2,700 waliwekwa chini ya ulinzi wa polisi kufuatia vurugu za mwishoni mwa wiki, huku watu wengine 217 wakifungwa gerezani.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha