Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hassan Rashid Jawad al-Ubayji, msimamizi wa Imam Husayn Shrine, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa Uwanja wa Mtume Mtukufu (Swalla Allahu ‘alayhi wa Aalihi wa Sallam) — mradi unaotekelezwa katika mfumo wa upanuzi mkubwa wa Uwanja Mtukufu wa Husseini — alisisitiza kwamba; miradi ya upanuzi ni miongoni mwa kazi ngumu zaidi ambazo Ataba Tukufu ya Husseini imechukua jukumu la kuzitekeleza katika pande mbalimbali.
Al-Ubayji alisema: Idadi ya wafanyakazi wanaohudumu chini ya sekretarieti ya Ataba Tukufu ya Husseini, kwa kiwango cha ukuaji wa kila mwaka kinachozidi asilimia 86, imeongezeka kutoka watu 1,600 mwaka 2004 (1382 Shamsia) hadi kufikia watu 27,000 mwaka 2026 (1404 Shamsia).
Alifafanua kuwa; wastani wa ukuaji wa jumla wa sekretarieti ya Ataba Tukufu ya Husseini katika kipindi cha miaka 2004 hadi 2026 (1382 hadi 1404 Shamsia), ukijumuisha miradi ya kibinadamu kama vile vyuo vikuu, hospitali, vituo vya watoto wenye tawahudi (autism) na vituo vya ushauri wa familia, umefikia asilimia 1,650 — kiwango kisicho na mfano kinachoonesha ukubwa wa juhudi hizo.
Mkurugenzi wa Ataba Tukufu ya Husseini aliongeza kuwa; miradi hii imetekelezwa kwa ushirikiano na msaada wa serikali kuu kupitia Ofisi ya Mkuu wa Diwani ya Wakfu wa Kishia pamoja na taasisi nyingine zinazosaidia, zikiwemo mamlaka ya mkoa wa Karbala na vyombo vyake husika.
Al-Ubayji aliendelea kusema kuwa; miongoni mwa miradi muhimu inayoendelea ni awamu ya tatu ya upanuzi iitwayo Uwanja wa Mtume Mtukufu (Swalla Allahu ‘alayhi wa Aalihi wa Sallam), ambao una eneo la ardhi lenye ukubwa wa mita za mraba 95,000 na eneo la majengo lenye ukubwa wa mita za mraba 300,000; na huu ni sehemu ya mradi mkubwa zaidi wa upanuzi katika historia ya Ataba Tukufu ya Husseini.
Alikumbusha kuwa; miradi ya upanuzi ni miongoni mwa kazi ngumu zaidi ambazo Ataba Tukufu ya Husseini imekubali kuwajibika kuzitekeleza katika nyanja zote.
Aidha, Al-Ubayji akieleza kuwa; awamu ya mwisho ya upanuzi itajumuisha Uwanja wa Imamu Hujjah (Mwenyezi Mungu aharakishe faraja yake tukufu), alifafanua kwamba; utekelezaji wa miradi hii mikubwa umekumbana na changamoto nyingi, zikiwemo upatikanaji wa rasilimali za kifedha, mazungumzo na wamiliki wa majengo na ardhi, pamoja na utekelezaji wa miundombinu kwa ushirikiano na serikali.
Aliongeza kuwa; mradi wa Uwanja wa Mtume Mtukufu (Swalla Allahu ‘alayhi wa Aalihi wa Sallam) utajumuisha hospitali maalumu ya dharura iitwayo Safir yenye ukubwa wa mita za mraba 5,000, pamoja na ukumbi wa mikutano ya kitamaduni na kidini wenye uwezo wa kuchukua watu 1,000, na huduma za afya zenye takribani vitengo 4,000 vya usafi katika sehemu mbalimbali za uwanja huo, ili kukidhi kikamilifu mahitaji ya mazuwari.

Maoni yako