Jumamosi 22 Novemba 2025 - 23:02
Jibu la wazi la Darul-Iftaa ya Misri kwa maswali mawili yasiyo na msingi

Hawza/ Darul-Iftaa, kwa kutegemea hoja za kisheria, imeeleza kwamba madai ya kutokujuzu kuswali swala ya maiti au swala nyingine yoyote katika misikiti iliyo na kaburi ni batili na hayana msingi.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Darul-Iftaa ya Misri, katika kujibu istiftaa ya kina kutoka kwa mmoja wa wananchi, ilichunguza msimamo wa Sheriah kuhusu baadhi ya vijana wanaoepuka kuswali katika msikiti ambao ndani yake kuna kaburi la masheikh au watu wema, na badala yake huswali swala ya maiti pembeni mwa kaburi baada ya kuzika. Vilevile, watu hawa hupinga kusomwa Qur’ani katika msiba na huwabebesha watu wajibu wa kusimama katika safu na kusema tu: “Muombeni msamaha ndugu yenu, kwani sasa anahojiwa.”

Muulizaji aliomba fatwa rasmi ili kukabiliana na fikra hizi ambazo, kwa kauli yake, zimeanza kuenea katika kijiji chao na vijiji jirani, hasa kuhusu kubomoa kaburi na kuswali swala ya maiti pembeni mwa kaburi.

Darul-Iftaa, kwa kutegemea dalili za kisheria, ilieleza kwamba; madai ya kutokujuzu swala ya maiti au swala nyingine katika misikiti yenye kaburi ni batili na hayana msingi.

Darul-Iftaa ilisisitiza kwamba kuswali katika misikiti hii kumejengeka juu ya Qur’ani, Sunna na Ijmai ya Umma. Qur’ani Tukufu imeeleza kujengwa msikiti karibu na makaburi ya Watu wa Pango (Ashaabul-Kahf), na wanazuoni wa tafsiri wamechukua hili kuwa dalili ya kujuzu kujenga misikiti karibu na makaburi ya watu wema.

Darul-Iftaa pia ilirejea matukio ya katika Sira ya Mtume (s.a.w.w.), kama vile kujengwa msikiti juu ya kaburi la “Abu Basir” mbele ya kundi kubwa la Masahaba bila pingamizi, na hadithi ya Mtume (s.a.w.w.) inayosema kuwa katika Msikiti wa “Khayf” wamelazwa Manabii sabini. Aidha, mazishi ya Nabii Ismail na Hajar (a.s.) huko Hijr na kukubaliwa kwa hilo na Mtume (s.a.w.w.) bila kukataza.

Kwa mujibu wa dalili hizi, Darul-Iftaa ilisisitiza kwamba kuswali swala ya maiti kwenye misikiti yenye dhariih ni swala sahihi, inajuzu, na hata ni yenye kupendekezwa; na kauli ya kuiharamisha ni uzushi usiozingatiwa.

Kadhalika Darul-Iftaa ilisisitiza kwamba kuacha swala ya maiti na kujitoa kushiriki kwa kisingizio cha kuwepo kwa dhariih ni kwenda kinyume na Sheriah moja kwa moja; kwani swala ya maiti ni faradhi ya kifaya, na Sheriah imehimiza kuitekeleza pamoja na kuandamana na jeneza hadi kaburini.

Darul-Iftaa ilibainisha kuwa kuanzisha jamaa nyingine nje ya msikiti au pembeni mwa kaburi kwa kisingizio cha kutokujuzu kuswali katika msikiti wenye kaburi ni kitendo kilichoharamishwa, kwani ndani yake kuna kuleta mgawanyiko katika jamaa ya Waislamu na kunategemea kauli isiyo na elimu, kinyume na maandiko ya Sheriah yanayoamuru umoja na kukataza utengano.

Darul-Iftaa ilihitimisha jibu lake kwa kutaja dalili za Qur’ani na Sunna zinazo himiza jamaa na kuonya mgawanyiko, ikiwa ni pamoja na maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msifarakiane,
pamoja na maneno ya mara kwa mara ya Mtume (s.a.w.w.) kuhusu hatari ya migawanyiko na hitilafu miongoni mwa Waislamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha