Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, mwanachuoni wa Kiislamu, Sheikh Hassan Sharifeh, Mufti na Imamu wa Msikiti wa Al-Safa jijini Beirut, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Masuala ya Wakfu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Kishia nchini Lebanon, katika taarifa yake ameeleza kuwa; uchaguzi wa Marekani umebeba jumbe mbalimbali za kisiasa ambazo si sahihi kuzipuuza, hususan zile zinazohusiana na sera za Serikali ya Marekani kuhusu vita dhidi ya Iran.
Sheikh Sharifeh alisema: “Iwapo tunataka kufahamu maoni ya Wamarekani kuhusu vita, tunapaswa kuyasoma kupitia sanduku za kura, badala ya kuridhika na misimamo na matamshi yanayotolewa na Serikali ya Marekani. Uchaguzi ni jukwaa la kidemokrasia ambapo raia hupata fursa ya kueleza kuridhishwa au kupinga sera zinazohusiana na maisha yake, usalama wake na utulivu wake.”
Sheikh Sharifeh aliongeza kuwa; matokeo ya uchaguzi huo, pamoja na kushuka nafasi na ushawishi wa Chama cha Republican kulikofuatana na matokeo hayo, yanaakisi ukubwa wa upinzani dhidi ya mkusanyiko wa sera mbalimbali, ambazo miongoni mwa athari zake kuu ni matokeo ya vita dhidi ya Iran. Hata hivyo, alibainisha kuwa vita hivyo havikuwa sababu pekee iliyoamua matokeo hayo.
Mwisho, alisema: “Mataifa hayataki kulipa gharama za vitendo viovu vya kijeshi kwa kupoteza usalama, uchumi na utulivu wao. Ujumbe unaopaswa kufikishwa katika Ikulu ya White House ni kwamba; nguvu hazipimwi kwa kuchochea vita, na utashi wa wananchi hauwezi kufupishwa na kuwekewa mipaka katika maamuzi ya serikali.
Masanduku ya kura yameshasema neno lake: Msigeuze vita vya nje kuwa chanzo cha kudhuru maslahi ya wananchi wa Marekani na kutishia utulivu wa eneo hili na dunia nzima.”
Maoni yako