Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, ametoa maelekezo yenye kubainisha majukumu manne kwa taasisi za ulinganiaji wa dini, wanazuoni na wahubiri waaminifu na wenye kujitolea katika medani ya ulinganiaji, kwa mnasaba wa siku za maombolezo ya pili ya Fatimiyyah.
Maandishi kamili ya maelekezo hayo ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
Ewe Mwenyezi Mungu! Tunakuomba kwa haki ya Fatimah, baba yake, mume wake, watoto wake na siri iliyohifadhiwa ndani yake, uunusuru Uislamu na Waislamu, na uwadhalilishe makafiri na wenye kuvuka mipaka.
Ninatoa salamu za rambirambi kwa Umma wa Kiislamu, hususan wananchi wa Iran wenye busara na msimamo thabiti wa kupinga dhuluma, Hawza, wanazuoni wakuu wa dini, wanazuoni na wahubiri waaminifu na wenye kujitolea katika medani ya ulinganiaji, kufuatia kuuawa kishahidi Bibi Siddiqah Tahirah Fatimah Zahra (a.s).
Kwa mnasaba wa siku za ulinganiaji wa dini katika kipindi cha pili cha Fatimiyyah (s.a), napenda kuwakumbusha mambo yafuatayo:
1. Kubainisha nafasi na mfano bora wa mwanamke Muislamu
Kufafanua na kuonesha taswira halisi ya mwanamke Muislamu, mwenye usafi wa tabia na mwenendo mwema, kupitia mwenendo wenye nuru wa Bibi Fatimah Zahra (s.a), pamoja na kutoa ufafanuzi kuhusu mfano wa tatu wa maisha ya mwanamke katika ulimwengu wa kisasa, ni miongoni mwa wajibu wa wanamapambano wote wa kitamaduni na wahubiri wanaojitolea katika medani ya ulinganiaji.
Kwa sasa, sote tunahitaji kurejea katika mwenendo adhimu na wenye kung'ara wa Fatimah (s.a), katika nyanja zote za maisha ya mtu binafsi, familia, jamii na siasa. Wananchi, vijana, wanaume na wanawake katika jamii yetu wanapaswa kunufaika na chemchemi hii isiyokauka ya mafundisho ya Bibi Fatimah (s.a), pamoja na mafundisho ya Uislamu yanayomjenga mwanadamu, Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt wake watoharifu.
2. Kuendeleza na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika mikusanyiko
Kuendelea na kuimarisha zaidi uwepo wa wananchi wetu wapendwa katika mikusanyiko ya mitaani, ambayo inazidi kudhihirisha nguvu na adhama ya mwamko wao, kwa kuzingatia mwongozo wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi (Mwenyezi Mungu aendeleze kivuli chake), na kusisitiza kulipiza kisasi cha damu ya mashahidi na Imam aliyeuawa shahidi (r.a), sambamba na kuipa kipaumbele ajenda ya msingi ya kuijenga upya nchi na kuendeleza maendeleo ya kisayansi, kiuchumi na kijamii, pamoja na kuimarisha uwezo wa kisiasa na kijeshi wa nchi.
Aidha, kuviunga mkono vikosi vyetu vya ulinzi na usalama vyenye uwezo na nguvu, mhimili adhimu wa Muqawama na viongozi wetu waheshimiwa, ni mambo yanayounda msingi na roho ya mfumo wa ulinganiaji wa dini, mjadala wa Kimapinduzi na fikra za Imam Khomeini Mkuu (r.a) pamoja na Kiongozi Mkuu aliyeuawa kishahidi (r.a).
Kwa msingi huo, wahubiri, wanaharakati wa masuala ya kitamaduni, vyombo vya habari vinavyotekeleza majukumu yao kwa juhudi za kujitolea na wanaharakati wa mitandao ya kijamii wanapaswa kuunda mshikamano na uratibu madhubuti ili kuendesha mapambano haya ya kitamaduni kwa pamoja.
3. Kujenga ukaribu na wananchi na kutambua mahitaji ya kizazi cha vijana
Kujenga ukaribu na wananchi watukufu na vijana wetu wapendwa, kutambua kwa usahihi changamoto, maswali, matatizo na mahitaji ya kizazi cha vijana, pamoja na kujenga uhusiano wa karibu, wa maelewano na wenye manufaa pamoja nao, ni miongoni mwa wajibu wetu.
Vilevile, tunapaswa kufahamu changamoto zinazoikabili familia na jamii katika zama hizi, kujipatia elimu, hekima na maarifa yanayohitajika kwa ajili ya kufundisha na kulea kizazi kipya, kuwaongoza watu wenye mahitaji ya kimalezi na kiutamaduni, na kutoa majibu kwa wale wanaotamani kupata maarifa safi na angavu ya Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Kiislamu.
Kadhalika, kuwa na huruma na wananchi, kushirikiana nao katika shida zao, kuwahudumia kwa moyo wa dhati na kusimamia matakwa yao halali ni miongoni mwa majukumu yetu na ya wahubiri wetu wapendwa.
4. Kurekebisha na kuimarisha mfumo wa utawala katika sekta za uchumi na utamaduni
Ili mfumo wa ulinganiaji wa dini, mapambano ya kitamaduni na shughuli za ufafanuzi na uelimishaji uweze kuleta matokeo yanayotarajiwa kwa ukamilifu, ni lazima mfumo wa utawala katika sekta za uchumi na utamaduni ufanyiwe marekebisho na kuimarishwa.
Kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake katika jambo hili, hususan mihimili mitatu ya dola na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya uchumi na utamaduni. Taasisi hizo zinapaswa kuongeza juhudi katika kurekebisha sera, mielekeo na mipango yao, kutatua matatizo na kuondoa vikwazo vinavyowakabili wananchi na vijana, kuendeleza maendeleo ya nchi na kukabiliana kwa ujasiri na hila na mipango ya maadui.
Haifai kuonesha udhaifu wala kusalimu amri mbele ya adui.
Katika njia hii, tunapaswa kuyaweka mbele ya macho yetu na kuyazingatia daima maagizo ya Mwenyezi Mungu yanayosema: «Wala msilegee wala msihuzunike, kwani nyinyi mtakuwa juu ikiwa nyinyi ni Waumini.» Pia kauli yake isemayo: «Na ushindi hautoki isipokuwa kwa upande wa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu na Mwenye hekima.» Na kauli yake nyingine isemayo: «Hakika Sisi tutalipiza kisasi kwa wahalifu.»
Kwa kuwatolea salamu na kuwaswalia Mitume, Mawalii na Mawasii wa Mwenyezi Mungu, hususan Mwisho wa Mitume (rehema na amani ziwe juu yake na Ahlul-Bayt wake), Mtukufu Wali wa Zama (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu autukuze utukufu wake), Imam wetu mpendwa aliyeuawa kkshahidi (r.a), Kiongozi Mkuu (Mwenyezi Mungu amhifadhi), Maraji' wakuu wa dini, vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na mhimili wa Muqawama, huku tukiwaombea afya njema, heshima na mafanikio wananchi wa Iran wenye msimamo thabiti, Umma wa Kiislamu ulioamka na kupata mwamko, viongozi wa kuongoza Umma (r.a) na wanazuoni wetu watukufu wa dini.
Tunatumai kwamba maombolezo yote na juhudi zinazofanywa na wahubiri wenye kujitolea katika medani ya ulinganiaji pamoja na Umma ulioamka, yatapokelewa na kupata uangalizi na upendeleo maalumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kwa mnasaba huu, ninatangaza kusimamishwa masomo ya ngazi za juu na masomo ya nje (Dars-e Kharij), pamoja na shughuli za vituo na jumuiya maalumu za kitaaluma za Hawza zilizoko Qum, kuanzia Jumatano, tarehe 1 Jumadath-Thani (20 Aban), hadi Jumapili, tarehe 5 Jumadath-Thani (24 Aban), kwa muda wa siku tano.
Hatua hii imefikiwa kwa uratibu na Maraji' wakubwa wa dini, Baraza Kuu la Hawza na taasisi nyingine za Hawza, kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa dini na wanazuoni waheshimiwa kusafiri na kushiriki katika shughuli za ulinganiaji wa dini kwa kujitolea na kwa mtazamo wa kijihadi.
Kama ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza cha Fatimiyyah, usimamizi wa masuala yanayohusu mipango ya shughuli za ulinganiaji wa dini, pamoja na likizo katika mikoa na ngazi ya kwanza ya masomo, unakabidhiwa kwa wakurugenzi wanaohusika, kwa uratibu na manaibu wao waheshimiwa.
Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
Alireza Arafi
Mkurugenzi wa Hawza Iran.
Maoni yako