Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mkusanyiko wa mada za mahdawiya ulio na anuani isemayo “Kuielekea Jamii Bora”, kwa lengo la kusambaza mafundisho na maarifa yanayohusiana na Imam wa Zama (a.s.), unawasilishwa kwenu wasomi kama ifuatavyo.
Imani juu ya mwokozi ni miongoni mwa mada ambazo zinakubaliwa na kushirikishwa miongoni mwa dini za Kiyahudi-Kikristo (za Ibrahimu) na zisizo za Ibrahimu. Migogoro na matatizo mazito yaliyohatarisha uwepo wa mwanadamu, na ambayo binadamu kwa uwezo wake mwenyewe hakuweza kuyakabili, ndiyo sababu kuu ilizosababisha kuundwa kwa wazo la mwokozi katika dini mbalimbali. Uhusiano uliopo kati ya kudhihiri kwa mwokozi na sifa kama kuenea kwa haki, kupinga dhuluma, na kadhalika, umesababisha wanadamu wa dini na itikadi zote daima kuwa na hamu ya kudhihiri kwa mwokozi wao. Ni dhahiri kwamba kiwango cha mapenzi na matarajio ya kudhihiri kwa mwokozi kinatokana na sababu mbalimbali. Katika muktadha huu, vyombo vya habari ni miongoni mwa sababu zenye athari kubwa zaidi katika kuibua hamu na shauku hii. Vyombo vya habari ni miongoni mwa zana zenye ushawishi mkubwa zaidi katika dunia ya leo; mbali na athari ya moja kwa moja wanayoiacha kwa watu, vinaweza pia kuathiri utamaduni, kaida, vigezo na viashiria ambavyo hadhira hujenga juu yake misingi ya mwenendo wao wa kimaisha.
Dunia ya vyombo vya habari ya Hollywood pia, tangu mwaka 1990, kwa mabadiliko ya taratibu lakini yanayoonekana, imeelekeza mwelekeo mkuu wa kazi zake kuelekea mada za uokozaji na za mwisho wa dunia.
Hollywood na kuunda hisia ya dharura ya kumhitaji mwokozi (1)
Kuibua hisia ya uhitaji na dharura ya mwokozi ni miongoni mwa mambo ambayo sinema ya Hollywood imeyategemea katika bidhaa zake nyingi za mwisho wa dunia.
Filamu "The Creator" iliyotengenezwa mwaka 2023, inajaribu kuonesha mgongano kati ya wanadamu na akili bandia.
Katika muktadha huu, katika moja ya mandhari ya filamu hiyo, tunaona kwamba wigo wa uhitaji wa mwokozi hauishii kwa wanadamu pekee, bali hata aina ya akili bandia inaoneshwa kuwa yenye uhitaji na shauku ya kudhihiri kwa mwokozi.
Hollywood na kuunda hisia ya dharura ya kumhitaji mwokozi (2)
Watayarishaji wa sinema ya Hollywood hutumia mbinu mbalimbali ili kuunda hisia ya uhitaji wa mwokozi miongoni mwa watazamaji. Mojawapo ya mbinu muhimu zaidi ni kugawa mambo katika pande mbili: mema na mabaya. Katika mbinu hii, nguvu za uovu katika filamu huonyeshwa kuwa na nguvu kiasi kwamba kuwashinda katika hali za kawaida kunaonekana kuwa haiwezekani. Uonyeshaji huu wa nguvu hufikia kiwango ambacho mtazamaji hushawishika kuwa njia pekee ya kuokoka katika hali iliyopo ni uwepo wa mwokozi.
Filamu ya "World War Z" iliyotengenezwa mwaka 2013 ni mfano dhahiri wa aina hii ya kazi. Katika filamu hii, mazombi kama nguvu za uovu, kwa kasi kubwa huiteka dunia nzima na kupunguza matumaini ya wokovu hadi kiwango cha chini kabisa. Katika hali hii, kudhihiri kwa mwokozi katika simulizi kunadhihirika kuwa jambo la lazima.
Kukithiri kwa kukutana kwa mtazamaji na mbinu hii katika bidhaa za sinema ya Hollywood kunasababisha yeye katika maisha halisi pia kufikia hitimisho kwamba njia pekee ya kuokoka kutoka kwa maovu ya dunia hii ni uwepo wa mwokozi.
Hollywood na kuunda hisia ya dharura ya kumhitaji mwokozi (3)
Miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na Hollywood ni kuonyesha kujitoa muhanga bila mipaka kwa waokozi wa Hollywood katika juhudi za kuwaokoa wanadamu. Katika mbinu hii, mwongozaji hujaribu kwa kuunda mazingira ya kihisia na ya kusisimua, kuonyesha kilele cha kujitoa kwa mwokozi kwa ajili ya ubinadamu.
Ni dhahiri kwamba mtazamaji wa sinema ya Hollywood, kutokana na kukutana mara kwa mara na waokozi na mashujaa wa aina hii, atavutiwa nao sana na katika maisha halisi pia daima atakuwa na shauku ya kuja kwa mwokozi wa aina hiyo.
Filamu ya "Interstellar" iliyotengenezwa mwaka 2014, ambayo ni mojawapo ya filamu bora zaidi za Hollywood zenye mhimili wa mwokozi, ni mfano wazi wa matumizi ya mbinu hii. Ndani yake, mwongozaji amejaribu kuonyesha kujitolea na kujitoa muhanga kwa mwokozi katika mandhari nyingi, shujaa ambaye yuko tayari, kwa ajili ya kuwaokoa wanadamu wote, hujitenga kwa huzuni kubwa na familia yake na binti yake wa pekee, na kuyatoa kafara maslahi yake binafsi kwa ajili ya maslahi ya kijamii.
Ufanisi-kazi wa sinema ya mwisho wa dunia ya Hollywood
Kazi ya Kwanza: Kujaribu kuonyesha matukio ya mwisho wa dunia kama mfumo uliopangwa
Katika sehemu mbalimbali za Injili ya Wakristo, tunaona kwamba katika kuelezea matukio ya mwisho wa dunia kabla ya kudhihiri kwa Issah Masih (a.s.), matukio mabaya na ya kutisha yametajwa, ambayo kila moja kwa namna yake ni tishio kwa wanadamu.
Kwa msingi huu, mojawapo ya dhima za filamu za mwisho wa dunia za Hollywood ni kwamba kwa kuonyesha matukio machungu ya mwisho wa dunia, zinajaribu kumfahamisha mtazamaji kwamba katika mchakato wa kufikia zama za dhahabu na ustawi wa kipindi cha kudhihiri kwa mwokozi, kutokea kwa matukio ya kutisha ya mwisho wa dunia ni sehemu ya mzunguko wa kiasili unaotokea kwa mpangilio maalumu, na hakuna njia ya kuyakwepa.
Kazi ya Pili: Kuamsha na kuonya kuhusu hatari za mwelekeo wa sasa wa jamii ya wanadamu
Kwa kuchunguza kazi za sinema za mwisho wa dunia za Hollywood, tunaona kwamba idadi kubwa ya uzalishaji huu ina mada za ukosoaji dhidi ya aina ya maisha ya sasa ya wanadamu. Matukio ya kutisha ya mwisho wa dunia yanayoonyeshwa katika kundi hili la kazi ni matokeo ya mtindo wa maisha ya kibinadamu na yana asili ya kibinadamu.
Kwa mfano, katika filamu za mwisho wa dunia kama vile mfululizo wa "Terminator" au "The Creator" (2023), tunaona kwamba akili bandia ambayo wanadamu wenyewe wameiunda, sasa imegeuka kuwa tishio kubwa kwa uendelevu wa maisha yao na imesababisha kuangamia kwa sehemu kubwa ya ustaarabu wa mwanadamu.
Kazi ya Tatu: Kutumia lugha ya ucheshi ili kupunguza hofu ya matukio ya mwisho wa dunia
Filamu za mwisho wa dunia zenye mwelekeo wa ucheshi ni miongoni mwa uzalishaji ambao umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni. Filamu kama "This Is the End" au "The World’s End" (2013) ni miongoni mwa kazi za mwisho wa dunia za Hollywood ambazo ndani yake matukio ya mwisho wa dunia yameoneshwa kwa lugha ya mzaha.
Miongoni mwa kazi za kutumia lugha ya ucheshi katika filamu za aina hii ni kupunguza hofu na msongo wa mawazo kuhusu matukio ya kutisha ya mwisho wa dunia. Kwa hakika, kurudia kukutana kwa mtazamaji na picha za aina hii pamoja na mzaha unaoambatanishwa na matukio ya kutisha ya mwisho wa dunia, husababisha polepole mtazamo wa watu kuelekea matukio haya kuwa wa kupuuzia na wa kichekesho, na hivyo kupunguza hofu ya jumla dhidi ya matukio hayo.
Juhudi za kuunda mfano wa mwokozi wa Kiislamu
Mfululizo wa tamthilia "Messiah" uliotengenezwa mwaka 2020 ni miongoni mwa kazi za kuigiza za Hollywood zilizosababisha mjadala mkubwa katika miaka ya hivi karibuni.
“Mehdi Dehbi” ni jina la muigizaji Mwislamu aliyebeba jukumu la mhusika wa Masihi katika mfululizo huu. Ingawa waandishi wa simulizi hili, katika muonekano wa nje wa tamthilia, wanamwonesha mhusika wa “al-Masih” kuwa zaidi ya mwokozi wa dini moja maalumu na wanajaribu kumuachia mtazamaji jukumu la kuamua mafungamano yake ya kidini, lakini kwa uwazi kabisa taswira ya Kiislamu ya mhusika huyu inatawala juu ya dini nyingine.
Mwokozi ambaye katika mandhari mbalimbali uungu wake unakataliwa, katika kipindi chote cha mfululizo hakatai kamwe vyeo vitakatifu anavyoitwa navyo; majina kama: al-Masih, Nabii, Imam, Mwana wa Mungu, Isa.
Yeye ambaye ni mhitimu wa sayansi ya siasa kutoka Massachusetts, Marekani, kwa akili yake ya juu hujinasua kwa ujanja kutoka katika vikwazo vyote anavyowekewa na huendeleza malengo yake ya kidanganyifu hatua kwa hatua. Ingawa katika kipindi chote cha mfululizo wamejaribu kwanza, kutuonesha wazi mhusika huyu kama mwokozi wa Kiislamu, na pili, kutompa mtazamaji taswira hasi iliyo wazi, lakini katika tabaka za ndani za kazi hii, mambo haya mawili yanaonekana kwa uwazi.
Sayansi, mwokozi pekee wa wanadamu
Katika filamu za mwisho wa dunia za sinema ya Hollywood, aina mbalimbali za waokozi huoneshwa kwa mbinu tofauti za uokoaji.
Mfululizo wa "3 Body Problem" ambao msimu wake wa kwanza ulionyeshwa mwaka 2024, na unaotajwa kama mfululizo wenye gharama kubwa zaidi kwenye jukwaa la Netflix, ni mfano kamili wa mwisho wa dunia unaozingatia sayansi. Katika mfululizo huu, ambao umejengwa juu ya tatizo la kifizikia (pamoja na mchanganyiko wa masuala ya kisiasa), viumbe wa anga wanatarajiwa kufika duniani baada ya miaka 400 na kuangamiza wanadamu.
Katika hali hii, kundi la wanadamu linawasubiri viumbe wa anga kwa shauku na linawaita kuwa miungu yao, ilhali kundi jingine linajitahidi kwa nguvu zote, kwa kutegemea kikamilifu maarifa na sayansi ya hali ya juu ya kibinadamu (kwa kukataa kabisa nguvu za kiungu na zisizo za kawaida), kuzuia kutokea kwa tukio hili la mwisho wa dunia.
Inapaswa kuzingatiwa kwamba bidhaa zinazosisitiza uokozi wa sayansi pekee na kukataa aina yoyote ya uokozi wa kiungu zina mifano mingi katika sinema ya Magharibi.
Utafiti huu unaendelea….
Kazi hii imeandaliwa na Kituo Maalumu cha Masomo ya Mahdawiya, Hawza ya Qum
Huku ikiwa imefanyiwa marekebisho kiasi
Maoni yako