Alhamisi 1 Januari 2026 - 02:00
Palestina yalaani mswada wa Israel kuhusu kuzuia adhana misikitini

Hawza / Baraza Kuu la Fatwa nchini Palestina limelaani muswada uliowasilishwa na utawala haramu wa Israel unaolenga kuweka vikwazo vikali kuhusu kuadhiniwa misikitini.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, baraza hilo lilitangaza katika taarifa yake kuwa; hatua hizi za kichochezi na za kudhalilisha zinazofanywa na utawala wa Kizayuni kwa ujumla zinalenga misikiti, na hususan Msikiti wa Al-Aqsa, na kulielezea mswada huo kuwa ni uhalifu mpya katika muktadha wa sera ya kuwabana na kuwanyanyasa Waislamu na wananchi, kuingilia masuala yao ya kidini, na kushambulia alama na nembo za Kiislamu katika ardhi yote ya Palestina.

Katika taarifa hiyo imeelezwa kuwa: Sauti ya adhana kutoka kwenye minara ya misikiti haitanyamazishwa, hata kwa kuwepo ulazima wa kulipa faini na adhabu, kwa sababu adhana ni sehemu isiyotenganishwa na dini ya Uislamu na matendo ya kidini ya sisi Waislamu. Tunauchukulia mswada huu kuwa ni jaribio lililoshindikana la kufifisha historia na uhalisia wa Kiislamu, na la kulazimisha mpango wa kurasimisha Uyahudi maeneo haya; na tunatoa onyo kali kuhusu hilo.

Baraza hilo lilitaja mswada huu kuwa ni wa kibaguzi na unaokiuka sheria na kanuni za kimataifa, na likaitaka jumuiya ya kimataifa, serikali mbalimbali pamoja na taasisi husika kuchukua hatua za dharura kusitisha aina hizi za mashambulizi ya kitamaduni na ya kivita dhidi ya misikiti, na kuwazuia Israel katika kuingilia ibada za Waislamu.

Chanzo: WAFA NEWS

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha